HEADER AD

HEADER AD

DIWANI : SIKUFANYA MAKOSA KUMTAMBULISHA MSIBANI MJUMBE

Na Dinna Maningo , BUTIAMA

KUMEKUWEPO na sintofahamu kwa Wananchi na viongozi wa serikali ya Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa, wilaya ya Butiama mkoani Mara, juu ya mjumbe wa halmashauri ya Kijiji kukaimishwa kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji. 

Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Mirwa kikiongozwa na Mwenyekiti Moris Onyango Odhiambo na Patrick Roche Pius wanadaiwa kumkaimisha Daud Sarurya kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji hicho baada ya kumsimamisha uenyekiti wa Kijiji Magige Mahera Msyomi Novemba, 10,2022.

Chama hicho kilimsimamisha Mwenyekiti Magige kikimtuhumu kuhusika na makosa saba likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka huku yeye akikana kuhusika na tuhuma hizo kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari siku chache zilizopita.

Hivi karibuni DIMA Online ikiwa katika Kijiji hicho ilikuta sintofahamu hiyo ya ofisi ya Serikali ya Kijiji kukaimishwa mjumbe kusimamia nafasi hiyo kama Kaimu Mwenyekiti wa kudumu katika nafasi hiyo hadi pale maamuzi mengine ya Chama yatakapofanyika dhidhi ya Mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi.

Imebainika kuwa mjumbe huyo alikaimishwa nafasi hiyo huku wananchi wakiwa hawana taarifa ya wazi ya kusimamishwa Mwenyekiti wa Kijiji na kutofahamu makosa yaliyosababishwa asimamishwe uongozi na kutotambulishwa mjumbe huyo kama Kaimu Mwenyekiti kupitia mkutano mkuu.

Kinachowakwaza wananchi ni baada ya Diwani wao wa Kata ya Mirwa Willy Brown kumtangaza msibani mjumbe huyo kwamba ndiye kaimu Mwenyekiti wa Kijiji kitendo kinachopingwa na wananchi wakidai kama yupo kihalali alipaswa kutangazwa kwenye mkutano mkuu wa wananchi na sio msibani.

       Diwani wa Kata ya Mirwa Willy Brouwn 

Mwandishi wa DIMA Online akafika nyumbani kwa Diwani huyo kufahamu sababu ya kumtambulisha mjumbe msibani kuwa ndiye Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji hili hali hajapendekezwa na wananchi wala halmashauri ya kijiji?.

Diwani huyo anasema " Mwenyekiti wa Kijiji alisimamishwa na Chama, kazi yangu ni kusimamia maendeleo ya Kata, suala la kumtangaza mjumbe kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji mimi nilifanya hivyo kwakuwa ndiyo mtu niliyepewa kufanya nae kazi.

"Mimi sibagui kufanya kazi na watu, hata nilipoletewa Polisi Kata nifanye nae kazi sikukataa kwahiyo huyo mjumbe kumtambulisha msibani sikufanya makosa.

"Huyo Mwenyekiti wa Kijiji analalamika wakati hajawahi kusoma taarifa ya mapato na matumizi, yeye ameshindwa kusimamia ujenzi wa maabara na fedha zilichangwa hadi sasa Maabara haijakamilika" anasema.

Akizungumzia kukwama kwa miradi ya maendeleo licha ya fedha kutolewa anasema.

"Nenda kwa Mtendaji wa Kijiji ndiyo anajua mapato na matumizi yeye ndiye anayekusanya mapato, mnada kila jumamosi tozo inakusanywa inakwenda halmashauri.

"Maguga tulipewa fedha Milioni 9 na halmashauri za ujenzi wa choo lakini ujenzi haujaendelea kwasababu Mwenyekiti wa Kijiji alikataa kuondoa banda lake la biashara.

Kuhusu Machinjio inayomilikiwa na Katibu wa CCM Kata ya Mirwa amesema.

"Machinjio siyo ya Kijiji siyo eneo la Serikali  ipo eneo la mgodi wa dhahabu wa Wachimbaji wadogo, na mmiliki wa machinjio analipa ushuru" amesema Willy.

Mwandishi wa DIMA Online alifika ofisi ya Kijiji ili kuzungumza na Mtendaji wa Kijiji hicho Lucus Kagina lakini haikufanikiwa kumpata hivyo akampigia simu ili kuzungumzia suala la mapato na matumizi katika miradi ya maendeleo kijijini.

Hata hivyo hakuwa tayali kuzungumza kwani kila alipopigiwa simu alipokea na kisha kukata simu alipopigiwa mara kadhaa alipokea nakusema  betri la simu ni bovu kisha akakata simu.

Majukumu na Kazi ya Diwani

Miongoni mwa majukumu na kazi ya Diwani ni pamoja na ;

Kudumisha na kuendeleza udumishaji  wa amani, usalama na utawala Bora.

Kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo la mamlaka yake na Taifa kwa ujumla kwa kuzingatia Sera za Taifa.

Kutekeleza upelekaji wa madaraka ya kisiasa, kiuchumi, kifedha na utawala kwenye ngazi zote za Halmashauri na hasa ngazi za chini za vijiji, vitongoji na mitaa.

Kutafuta na kudumisha vyanzo vya mapato vya kutosha ili kuwezesha kutekeleza majukumu na kazi  zake.

Kuendeleza na kuhimiza afya bora, elimu na burudani na kukuza maisha ya watu ya kijamii na kitamaduni.

Kuwa karibu sana na wapiga kura na kupata ushauri wa wananchi katika mambo yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye Halmashauri.

Diwani atateuwa angalau siku moja kila mwezi kukutana na wananchi katika eneo lake la uwakilishi ili kupata maoni yao na kuwajulisha maamuzi ya jumla ya Halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wananchi wa eneo lake la uchaguzi.

Diwani ana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi na hutoaji wa huduma katika eneo analoliwakilisha, kukosoa hatua za utekelezaji au hutoaji wa huduma za kupendekeza.

Je Wananchi, Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Magunga wanasema nini Kusimamishwa Mwenyekiti wa Kijiji na changamoto za kusuasua kwa miradi ?.

Endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza.




No comments