SABABU ZILIZOMWIBUA NICOLAUS CHICHAKE KUUSAKA UBUNGE JIMBO LA TARIME VIJIJINI
Na Dinna Maningo, Tarime
MTIANIA wa ubunge Jimbo la Tarime Vijijini ambaye ni mkazi wa Nyamongo , wilayani Tarime mkoa wa Mara , Nicolaus Mgaya kwa jina maarufu Chichake ,amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea ubunge huku akieleza sababu za kuutaka ubunge.
Nicolaus amesema kuwa lengo lake la kutiania ni kutaka kufikia adhima ya maendeleo katika jimbo hilo na taifa kwa ujumla.
" Kila mtu anayo haki ya kutia nia kwa nafasi yoyote anayohitaji ilimradi ana vigezo na sifa za kutiania ya kugombea ubunge " amesema Nicolaus.
Jimbo lina fursa ila watu ni maskini
Amesema kwamba Jimbo la Tarime vijijini lina fursa kubwa lakini watu wake walio wengi ni maskini huku likiwa na changamoto nyingi ambazo zinaweza kubadilishiwa na kuwa fursa.
" Kuna fursa ambazo haziwafikii wananchi ndio maana sehemu nyingine kuna umsikini mkubwa . Tunahitaji kiongozi anayeweza kusaidia Tarime yetu ili watu wetu waweze kubadilika katika maisha halisi .
" Tarime vijijini tuna fursa kubwa lakini je ni namna gani tunaweza kunufaika ,hii imekuwa ni changamoto kubwa sana ambayo inawafanya wananchi kuendelea kubaki katika umaskini .
" Changamoto hii inasababishwa na kukosa mtandao wa namna gani watu waweze kufikia sehemu moja na sehemu nyingine" amesema Nicolaus.
Amesema ni wakati wa kupata kiongozi ambaye ni sahihi kwa ajili ya jimbo hilo ili aweze kubadilisha taswira ya jimbo na liendane na mazingira halisi ya fursa zilizopo na kwamba mtu sahihi wa kuivusha Tarime ni yeye Nicolaus.
Nicolaus ameeleza sababu zinazozozifanya watu wa jimbo hilo kuendelea kuwa masikini kwamba ni pamoja na ;
" Watu wengi wamekuwa maskini kwasababu ya kukosa elimu. Vijana wengi, vikundi vingi vikiwemo vya akina mama , wajane, wajawazito na watu wenye ulemavu hawashirikishwi vuzuri kwenye mikopo hiyo, hawana elimu nzuri ya namna gani ya kurejesha marejesho, pia ni kwasababu wamekosa elimu nzuri namna gani wafanye biashara na nidhamu ya hela.
" Nikipata fursa ya ubunge nitahakikisha natengeneza vijana , natengeneza jamii ili watu waweze kuzifikia fursa zilizopo Tarime vijijini zikiwemo fursa za biashara , kilimo na uwekezaji" amesema Nicolaus.
" Nikipata ubunge nitashirikiana na jamii ili kuweza kutengeneza jamii moja, kuwaunganisha watu , mtu wa Kemambo ajue fursa zinazopatikana Muriba, mtu wa Itiryo akienda Bumera ajue fursa ziko wapi ili aweze kunufaika nazo" amesema Nicolaus.
Ameongeza kuwa , serikali imefanya mambo mengi lakini haiwezi kuyamaliza yote lazima na wabunge wafanye kazi na wananchi wafanye kazi katika uzalishaji mali.
" Mtu asome akimaliza arudi kujiajiri sio amsubiri ajira ya serikali kwasababu serikali ina ajira chache haziwezi kuendana na kiwango ambacho wanafunzi wanahitimu shule.
" Tuchangamane kwa kuoneshana fursa ili watu waje waseme Jimbo la Tarime ni la kuigwa. Kiongozi lazima uwe balozi kwa watu wote " amesema .
Ametoa wito kwa jamii kutofanya maamuzi kwa mihemko na badala yake wafanye maamuzi ambayo yatasaidia jamii .
" Tutazame mtu mwenye uwezo wa fikra, uelewa, nia ya mtu pasipokutafsiri nini alicho nacho au nini asicho nacho kwa maana ya uchumi wake wa fedha.Tarime vijijini tufanye mabadiliko mazuri tuchague mtu ambaye ni sahihi" amesema.
Amewaomba vijana kuchukua fomu kutiania ubunge na kusema kuwa vijana wengi ni waoga kwasababu ya kuwa na nidhamu ya uoga na hawajitokezi kugombea hilihali wana uwezo wanaweza kutiania na kugombea na kufanya mambo makubwa.
" Tabu yetu kubwa ni uoga , nitoe wito kwa vijana wenzangu na wasomi wenye uelewa wenye nia wajitokeze kuchukua fomu kutia nia ubunge nafasi ambayo ipo kwa ajili ya watu wote.
" Kila Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kugombea ubunge, cha msingi awe ni mtu ambaye ana vigezo. Tunahitaji mtu ambaye atawaunganisha watu wa Tarime , tunahitaji mtu ambaye anawiwa na maendeleo ya Tarime vijijini .
" Tunahitaji mtu ambaye anasikiliza na kuelewa changamoto za vijijini, tunahitaji mtu ambaye atajua kutafsiri na kuifanyia kazi Ilani ya chama cha Mapinduzi na mtu huyo si mwingine bali ni Nicolaus Chichake " amesema.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama cha Mapinduzi ( CCM), tarehe ya kuchukua na kurejesha fomu ni kuanzia tarehe 28/06/2025 mpaka tarehe 02/07/2025.
Kuteua majina matatu (03) ya wagombea ubunge na udiwani wa Kata ni tarehe 09/07/2025 mpaka tarehe 19/07/2025.
Kujitambulisha kwa wagombea ubunge wa majimbo kwenye Kata na wagombea Udiwani kata ni kuanzia tarehe 27/07/2025 mpaka tarehe 01/08/2025.
Zoezi la kupiga kura za maoni ndani ya chama ni tarehe 02/08/2025 kwa wagombea udiwani wa kata na ubunge wa majimbo kwenye kata.
Uteuzi wa wagombea (mmoja mpeperusha bendera wa chama) Udiwani wa kata ni tarehe 11/08/2025.
Uteuzi wagombea (mmoja-mpeperusha bendera wa chama) Ubunge kila jimbo ni tarehe 20/08/2025 ambao ndio watakaogombea kuchuana na wagombea wengine wa vyama vya upinzani ili kupigiwa kura na wananchi katika uchaguzi mkuu, utakaosimamiwa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ( INEC ) utakaofanyika mwaka huu.
Post a Comment