MRADI WA DAKIO LA MTO MARA KUWAFIKIA WATU 26,368
Na Jovina Massano, Tarime
WILAYA sita mkoani Mara kunufaika na Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la mto Mara utakaochochea maendeleo ya wananchi, unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Asilia (WWF)kwa ufadhili wa Shirika la Kimaendeleo la Kimataifa (USAID).
Hayo yameelezwa Machi 21, 2023 katika ukumbi wa Blue Sky Wilayani Tarime mkoani Mara, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Dakio la mto Mara (Mara river catment-Tanzania).
lengo la mradi huo ni kuhakikisha uhifadhi endelevu katika bonde la mto Mara na Bionuwai yake unasimamiwa vizuri na kuendeleza mfumo thabiti wa Ikolojia ya Uhifadhi ili kuboresha maisha ya jamii katika uhifadhi wa rasilimali za Maji.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mntenjele. Akizindua mradi huo wa Dakio la mto Mara, amesema Tanzania imepata ufadhili kutoka serikali ya Marekani katika kutelekeza shughuli za uhifadhi wa Dakio la mto Mara utakaodumu kwa kipindi cha miaka mitatu katika jamii ya Mara.
" Mradi huu unatarajia kuwafikia watu 26,368 watakaopata elimu kupitia uhifadhi wa rasilimali za Maji pamoja na mifumo bora ya usambazaji Maji katika wilaya sita za mkoa wa Mara ambazo ni Serengeti, Butiama, Tarime,Rorya,Musoma na Bunda ",amesema Kanali Mntenjele.
Ameongeza kuwa utekelezaji utaambatana na utoaji elimu kwa wananchi ili kuelewa miti rafiki kwa mazingira itakayosaidia katika uhifadhi wa rasilimali za maji na kuongeza mtiririko katika maeneo haya.
Meneja wa uhifadhi wa WWF Profesa Lawrence Mbwambo amesema wilaya hizo zitanufaika na mradi huo kutokana na umuhimu wa mto Mara katika uzalishaji wa chakula kwa wananchi kwa kuongeza tija katika Kilimo na malisho ya Mifugo.
"Tutautekeleza kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Mara lakini pia mradi huu utawafikia watu wa rika zote wakiwemo wanawake na watoto sambamba na wadau wa mazingira.
" Wadau wa habari kwa lengo la kupaza sauti zao kwa kutumia vyombo vyao magazeti,mitandao ya kijamii ,radio na runinga kwa kuelimisha,kuhamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi ya mazingira kikamilifu lakini pia kuonyesha jitihada zinazofanywa na WWF katika uhifadhi", amesema Lawrence.
Hakusita kuikumbusha jamii umuhimu wa kutunza na kulinda mazingira kwani mabadiliko ya tabia nchi yanapotokea yanaathiri watu wote kwa kukosa mvua na kuwa na vipindi virefu vya jua hivyo kusababisha ukame.
Ameongeza kuwa changamoto zinazochangia uharibifu na kuathiri mazingira ni uwepo wa shughuli za ardhi kwa maana ya ukataji wa miti hovyo, Kilimo na umwagiliaji holela na uwindaji wa kutumia moto.
Nae mwakilishi kutoka shirika la Kimataifa la Kimaendeleo la msaada la watu wa Marekani( USAID) Boniphace Mwita akimwakilisha Mkurugenzi wa shirika hilo, amesema kuwa wananchi wana wajibu wa kuhifadhi mazingira katika uendelevu wa faida ya vizazi vijavyo utakaobadili mazingira katika Bonde la mto Mara.
Nae mwakilishi kutoka shirika la Kimataifa la Kimaendeleo la msaada la watu wa Marekani( USAID) Boniphace Mwita
"Shirika la USAID linapenda sana ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Marekani katika kuwasaidia wananchi lakini pia utunzaji wa mazingira shirikishi na mtambuka kwa pande zote mbili za Kenya na Tanzania.
" Katika mashirikiano haya yawe ya pande zote mbili aidha kazi inayofanyika ya mazingira lakini tusisahau matokeo yaonekane kwa wananchi wanaoishi na jamii nzima kwa kupata maji safi na salama kutunza mazingira ya mto Mara bila kusahau kushirikisha sekta binafsi,"amesema Boniphace.
Ziada Stanley wa mkono wa maendeleo Vijijini wa wilayani Rorya amewapongeza na kuwashukuru WWF pamoja na USAID kwa kuamua kuwashirikisha na kuwaelimisha wananchi kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti rafiki ili kuleta mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema kwamba kwa kiasi kikubwa wilayani humo wananchi wengi wamejikita katika uchomaji wa mkaa kwa kukata miti pasipo kupanda hali inayosababisha ukame katika maeneo mengi.
Kijiografia Bonde la mto Mara linashirikisha nchi za Tanzania na Kenya, linakadiliwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 13,504 ambapo asilimia 65 za eneo zikiwa nchini Kenya.
Kwa upande wa Tanzania ni asilimia 35 na unakabiliwa kusafiri umbali wa kilomita 395 kutoka kwenye chanzo chake katika misitu ya Mau nchini Kenya kupitia mbuga za Taifa za Maasai Mara na Serengeti kwa Upande wa Tanzania hadi ziwa Victoria.
Post a Comment