DC BUKOBA KUZIKAGUA SHULE KUONA MAZINGIRA WANAYOSOMA WANAFUNZI
Na Alodia Babara, Bukoba
MKUU wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Yohana Siima amesema atafanya ziara ya kukagua shule ili kuona mazingira wanayosomea wanafunzi kama ni rafiki kwao kupata elimu bora.
Siima ameyasema hayo Machi 24, mwaka huu akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera katika mahafari ya kuhitimisha mafunzo mbinu ya walimu kazini wa kozi ya kwanza ya ualimu elimu ya awali kwa mfumo wa Montessori.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Yohana Siima akifunga mafunzo mbinu ya walimu kazini elimu ya awali kwa mfumo wa Montassori, mafunzo ambayo yalitolewa na chuo cha Partage kwa kushirikiana na serikali.
Walimu wapatao 20 wamemaliza masomo yao katika chuo cha Partage na walikuwa wanatoka shule za serikali katika halmashauri nane za mkoa wa Kagera.
Siima amesema kuwa, wanaweza kuwa wanaona wanafunzi wanapendeza barabarani kumbe huko wanakosomea mazingira yao si mazuri kwa ajili yao kupata elimu bora.
Amesema atafika katika shule ya partage Montessori na shule nyingine zilizopo manispaa ya Bukoba ili aangalie mazingira wanayosomea wanafunzi kama ni rafiki kwao kupata elimu bora.
“Nimeona hapa wanafunzi wakiwa na uwezo mzuri wa kuongea kiingereza lakini nitakagua shule zilizopo hapa manispaa ili kuona kule shuleni mazingira yakoje na kama ni rafiki kwa kujifunzia na kwa kupata elimu bora” amesema Siima.
Amesema ana imani kuwa walimu waliohitimu elimu ya awali kupitia mafunzo ya miezi sita waliyoyapata wataweza kutatua changamoto mbalimbali na ilivyokuwa awali ikawe tofauti.
Ameongeza kusema ifikapo mwaka 2025 wanatarajia walimu 120 walioko kazini watakuwa wamepata mafunzo ya elimu ya awali na idadi hiyo itaongezeka iwapo walimu waliopata mafunzo watatekeleza yote waliyojifunza na aliwahimiza wazazi kuendelea kupeleka wanachuo wenye sifa za kujiunga na mafunzo hayo.
Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Partage ambacho pia kina shule ya Montessori Phillipe Krynen amesema mwaka 1990 walianzisha shule hiyo na baadae walianza kutoa mafunzo ya chuo cha ualimu elimu ya awali kama Partage.
Anasema mwaka jana 2022 walianza ushirikiano na serikali na mwezi Oktoba ndipo walimu 20 kutoka halmashauri nane za mkoa huo walianza mafunzo yao na kuhitimu jana.
Amesema wilaya ya Muleba walimu 4, Bukoba vijijini 3, Biharamlo 3, Karagwe 2, Kyerwa 2, Ngara 2, Misenyi 2 na manispaa ya Bukoba 2.
Kwa upande wake Mthibiti Ubora wa shule toka Wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia Mwl Augusta Lapokela amesema kuwa, wizara itaendelea kufuatilia na kusimamia elimu inayotolewa ngazi zote.
Mmoja wa wahitimu Edmond Dominick amesema kuwa, baada ya kupata masomo hayo wanaenda kuondoa changamoto zilizokuwepo na kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa awali ili waweze kuelewa zaidi.
Post a Comment