HEADER AD

HEADER AD

MRAJIS, MUFILISI WAZUNGUMZA KUHUSU SACCOS YA UMAWANYA ILIYOKUFA


 >>>Mufilisi kufuatilia Madeni

>>>Chama chafutwa baada ya kushindwa kujiendesha

 >>>Chanzo ni Halmashauri kushindwa kulipa madeni


Na Dinna Maningo, Butiama

MUFILISI wa wilaya ya Butiama ambaye pia ni Afisa Ushirika Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Emmanuel Rutatora amesema Chama cha Walimu cha kuweka na kukopa UMAWANYA kilishafutwa kwenye daftari la usajili baada ya kushindwa kujiendesha.

Mufilisi amesema hayo baada ya Mwandishi wa Habari wa DIMA Online kutaka kufahamu juu ya hatma ya madai ya Chama hicho kinachodai fedha Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Tsh. 16,971,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Tsh.3,195,768.

Fedha hizo ni makato ya mishahara ya watumishi walimu waliyokuwa wakikatwa na halmashauri hizo kwa ajili ya kuziweka kwenye SACCOS wanachama waweze kukopeshana  fedha ili kusaidiana na kujiinua kiuchumi lakini hazikuwekwa.

Mufilisi huyo anayeshughulika na Vyama vya Ushirika vilivyofutwa kwenye daftari la usajili la Serikali amesema "Hicho Chama ni miongoni mwa Vyama vilivyofutwa, shughuli yangu ninayoifanya ni kwenda kuangalia madeni, madai kutafuta wadau wote husika na kupata taarifa zilizopo.

"Walishakuja mkoani walileta madai yao wakasema wamekatwa fedha zao na Mkurugenzi makato ya mshahara kwamba fedha zilikuwa zikija Mkurugenzi anazikata na kuzipeleka kwenye vyama husika lakini hakuwapatia fedha hizo"amesema Emmanuel.

Amesema kuwa baadhi ya Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri walikuwa wazito kutoa fedha hizo kwenye Vyama vya Ushirika.

Amesema wanachama hao waliombwa waende hazina ili kuona namna walivyokuwa wanakatwa fedha zao kwakuwa baadhi ya Wakurugenzi waligoma kulipa wakidai hawafahamu madeni hayo.

" Mufilisi kazi yake ni pamoja na kufuatilia Vyama vilivyofutwa kujua mikopo yao,madeni ili mwisho wa siku kinachodaiwa na wanachama wapate haki zao, Mufilisi inatamatisha shughuli za Chama.

Mufilisi amesema moja ya shughuli ya Mufilisi ni kufuatilia madeni ya Vyama vilivyofutwa kwenye daftari la usajili na kwamba atafuatilia kujua wanaodaiwa kuhakikisha wanarejesha fedha.

"Nitafuatilia kujua kwanini huyu hajalipwa na kwanini huyu hajalipa, hatua ya mwisho nihakikishe napata taarifa sahihi, kama Mkurugenzi anadaiwa atahakikisha analipa hizo fedha ili wanachama wapate haki zao.

"Nipo Kwenye hatua za awali za ufuatiliaji kuna barua nimetuma ili kupewa kibali cha kufuatilia kazi zote maana ili ufuatilie vyama hivyo vilivyotamatishwa natakiwa niwe na barua ambayo imetangazwa kwenye gazeti la serikali, ikishatoka hiyo barua kazi hiyo itaanza ya kufuatilia haki zote za wananchama" amesema Emmanuel.

  Kauli ya Mrajis

Aliyekuwa Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Mara Kija Maheda mbaye amestafu utumishi mwaka huu amesema moja ya sababu ya SACCOS ya UMAWANYA kushindwa kujiendesha ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kwa wakati huo kushindwa kutoa fedha kwenye Chama ambazo ni makato ya mishahara ya watumishi.

Amesema madai ya watumishi wa Chama hicho yalichangia Chama kushindwa kupata fedha za kukopa na kuweka hali iliyopelekea Chama kufutwa kwenye daftari la usajili baada ya kushindwa kujiendesha.

"Chama hicho nakifahamu kilianzishwa wakati wilaya ikiwa moja wilaya ya Musoma, wakati huo wilaya ya Butiama ilikuwa bado haijaanzishwa, ilipoanzishwa wilaya ya Butiama Halmashauri ziligawanywa Butiama na Musoma, watumishi wakagawanyika.

"Chama hicho kimefutwa mwaka jana kwenye daftari la usajili la Serikali baada ya kushindwa kujiendesha. Pia Butiama kulikuwa na changamoto afisa ushirika wa Butiama alifariki, hawakuwa na afisa ushirika kamili wa kuwasikiliza na kuwashauri jinsi ya kufuata taratibu za kisheria katika kufuatilia madai yao.

"Mimi nilipokuwa kazini nilimwandikia barua Mkurugenzi wa halmashauri kujua kwanini hajarudisha fedha za hao watu lakini sikupata majibu, nilichokifanya nilipeleka orodha kwa Mrajis Taifa kwamba SACCOS hiyo na zingine za Bunda, Musoma Wakurugenzi wamegoma kulipa maana wale walimu walikatwa fedha zao" amesema Kija.

Ameongeza kusema " Kwa Sasa mimi nimeshastaafu kazi sijui ya ofisini. Butiama Vyama vingi vimefutwa vilishindwa kujiendesha, tuliona hatuwezi kuwa na Vyama jina tu kinaitwa Chama alafu hakitoi huduma kwa wanachama, hakuna mikutano, hakuna gawio.

"Hao Wakurugenzi ipo mamlaka yao mimi mrajis siwezi kuwalazimisha, Serikali ina mgawanyo wake, watu wa TAMISEMI washughulikie maana hizo fedha ziliendelea kukatwa zikawa zinaingia ofisi ya Mkurugenzi sasa zilitumikaje hilo ni suala lingine na si kwa hao Wakurugenzi waliopo sasa ni waliopita.

"Mrajis Taifa alitutumia barua akatutaka tutume orodha ya Vyama ambavyo vina matatizo waajiri wamegoma kulipa fedha zao nakumbuka niliandika barua Dodoma, na si kwamba Mara tu ndiyo vyama vimefutwa ni nchi nzima, kwasababu kuna maeneo mengi"amesema Kija.

Ameeleza " Kuna Wakurugenzi hawakulipa fedha nakumbuka nilipeleka taaifa ya wilaya ya Bunda zilikuwa SACCOS 4, Musoma vijijini 3, Butiama na Tarime, tulimpelekea Mrajis Taifa apeleke TAMISEMI.

"Kwakuwa TAMISEMI ni bosi wa Wakurugenzi ambao amewateua kusimamia shughuli na wametumia pesa za SACCOS wakashindwa kulipa wazilipe, sasa nilipotoka sijajua kilichoendelea kwasababu sipo ofisini" amesema Kija.

Mrajis huyo mstaafu amesema pamoja na kwamba Chama kimefutwa wanachama hao wana haki ya kulipwa fedha zao kwa wakati kwakuwa ni makato ya mishahara yao iliyokatwa na Halmashauri.

"Kuna mtu anaitwa Mufilisi Chama kikifutwa huwa anateuliwa Mufilisi ambaye kazi yake ya kwanza ni kuainisha ni mali gani Chama kilikuwa kinamiliki, nani alikuwa anadai, nani alikuwa anadaiwa huyo ndiyo anashughulikia vyama vilivyofutiwa usajili.

"Kwasababu chama kikikufwa kusipokuwa na utaratibu ile mali ya wanachama itapotea, ni kama ilivyokuwa Mara Cooperative Union ilipofutwa aliteuliwa Mufulisi akashughulikia, hivi karibuni zile mali zimekabidhiwa na madeni ya wanayodai watalipwa" amesema.

Kija ameeleza kuwa Wilaya ya Butiama haina afisa Ushirika wanakaimu maafisa kilimo na kwamba walimteua Emmanuel Rutatora ambaye ni afisa ushirika wilaya ya Rorya kuwa afisa Mufilisi wilaya ya Butiama na Rorya.

"Mufilisi ni mtu anayeteuliwa na Serikali kufuatilia madeni ya Chama cha Ushirika kilichofutwa kwenye daftari la Serikali (Mtu anayefuatilia vitu viliyofilisika), na sababu mojawapo ya UMAWANYA kufutwa ni baada ya kushindwa kujiendesha kwa sababu ya hayo madeni.

" Maafisa waliokuwepo kwa wakati huo walipaswa kuwabama Wakurugenzi wakati ule zilipogawanywa wilaya wangelipa kwa wakati sasa Wakurugenzi walishahama zaidi ya sita, hicho Chama ni cha zamani na wilaya ziligawanywa zamani" amesema Kija.

Mrajis aahidi kufuatilia 

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Mara Lucus Kiondele ambaye ameshika nafasi ya Mrajis aliyestaafu kazi amesema ana siku tatu tangu aingie ofisini na ameahidi kufuatilia na akishapata mwelekeo wa suala hilo atatoa majibu sahihi.

"Leo ni siku yangu ya tatu tangu nimeingia ofisini, hili suala nitalifuatilia nikishapata mwelekeo wake nitatoa majibu sahihi, lakini kwa utaratibu wa kisheria hivyo vyama ambavyo vimefutwa huwa anateuliwa Mufilisi ambaye anasimamia mali na madeni.

"Yeye ndiye anaratibu kwenye ukusanyaji wa taarifa za fedha kama zipo nje na baadae akikamilisha zoezi lake waliokuwa wanadai wanalipwa kwa mujibu wa taratibu na Kanuni"amesema.

Ameongeza "Sasa kwakuwa sina taarifa na hiki Chama ngoja nifuatilie aliyeteuliwa kusimamia kama yupo na amefikia hatua gani, kama kilishafutwa yawezekana alishateuliwa Mufilisi kwahiyo nitafuatilia nipate picha kamili hatua alizofikia" amesema Lucus.

Viongozi wa UMAWANYA wameiambia DIMA Online kuwa hawana taarifa ya chama kufutwa na hawajapokea barua yoyote kutoka Serikalini ikieleza kufutwa kwa Chama hicho na kwamba Chama chao kimekufa baada ya kushindwa kujiendesha kutokana na fedha wanazodai Halmashauri.

Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Msalika Makungu alipoelezwa kuhusu madai ya watumishi hao ameowaomba wafike ofisini kwake waonane ana kwa ana ili awasikilize.

Aprili,7, 2023 DIMA Online iliripoti habari kuhusu Chama cha Ushirika cha kuweka na kukopa cha Walimu (UMAWANYA) Wilayani Butiama ambacho kimekufa baada ya kushindwa kujiendesha.

Viongozi wa Chama hicho walieleza kuwa sababu ya SACCOS kushindwa kujiendesha ni baada ya Halmashauri ya wilaya ya Butiama na Halmashauri ya wilaya ya Musoma kushindwa kulipa madeni zaidi ya Tsh. Milioni 20, fedha ambazo ni makato ya mishahara ya walimu 61 wakiwemo wastaafu 29.

Kwa mujibu wa viongozi wa Chama hicho walieza kuwa halmashauri ya Wilaya ya Butiama kila mwezi ilikuwa ikiwakata mishahara wanachama walimu 57 kwa ajili ya kuwawekea fedha zao kwenye SACCOS hiyo kama Akiba yao lakini mwaka 2018-2020 ilishindwa kuweka licha ya kuendelea kuwakata mishahara jumla ya Tsh. 16,971,000.   

Katika Halmashauri ya wilaya ya Musoma Walimu wanne wanadai fedha jumla ya Tsh. 3,195,768 fedha ambazo ni madeni ya mwezi Agosti, 2011- Desemba, 2019, deni lote katika halmashauri hizo likiwa na jumla ya Tsh. 20,116,768 ambazo hadi sasa walimu hao hawajalipwa.

Madeni hayo ya walimu ni makato ya akiba na marejesho ya mikopo yaliyokuwa yakikatwa kupitia Hazina ya Watumishi na fedha kuwekwa katika akaunti za Halmashauri hizo kwa lengo la kuwawekea akiba kwenye SACCOS lakini halmashauri hazikufanya hivyo. 

Walimu hao ambao wengine kwa sasa ni wastafu wamekuwa wakichapa mwendo hadi ofisi mbalimbali za Serikali kufuatilia hatma ya malipo yao lakini imekuwa ndoto kwao kitendo wanachodai huwenda Halmshauri hizo zimekula fedha zao na kuwadhulumu haki yao halali itokanayo na makato ya mishahara yao.


No comments