SERIKALI IMESEMA MATUMIZI YA TEHAMA NI MUHIMU
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imesema matumizi ya TEHAMA katika suala la ulinzi na usalama wa Maliasili ni suala lisiloepukika huku ikisisitiza kuwa mfumo fungamanishi wa kieletoniki wa ufutiliaji matukio ya ujangili ni muhimu kwa mazingira ya Dunia ya sasa.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Takwimu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi ametoa kauli hiyo Jumatano Aprili 12, 2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao kazi kilichowakutanisha Wadau mbalimbali wa Uhifadhi.
Lengo likiwa ni kuboresha na kudhibitisha nyaraka za mahitaji ya mfumo fungamanishi wa kielektoniki utakaosaidia katika ufuatiliaji wa matukio ya ujangili na udhibiti wa maeneo yaliyohifadhiwa nchini.
Amesema kuwa matukio ya ujangili wa wanyamapori na misitu yaliyokusanywa na Wataalamu ni sehemu ndogo tu ya mfumo mzima wa kielektroniki wa uhifadhi utakaokuwa na mambo mengine fungamanishi katika usimamizi na ufuatiliaji wa bioanuwai na matumizi ya maliasili.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt.Kohi amewataka wajumbe wa kikao hicho kutumia weledi wao kutoa michango chanya na maoni ya kujenga yatakayosaidia kutengeneza mfumo utakaosaidia Serikali katika masuala ya uhifadhi.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia kupata tathmini na taarifa kwa usahihi na haraka ili kurahisisha huduma za uhifadhi.
Kikao hicho kilichofadhiliwa na Mradi wa Kuzuia na Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori na Biashara haramu ya nyara na mazao ya Misitu ( IWT) mbali ya kuwakutanisha Wadau wa Uhifadhi, pia kimewakutanisha Wataalamu wa TEHAMA, Wataalamu wa Inteligensia na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Post a Comment