HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI WA KIJIJI ADAIWA KUMPIGA MWANANCHI NA KUMSABABISHIA KIFO

>>Chanzo ni saruji Marehemu alitaka kujilipa deni

>>Ni baada ya Marehemu kufuatilia deni lake Tsh 80,000 bila mafanikio

Na Dinna Maningo, Tarime 

MWENYEKITI wa Kijiji cha Kewanja Kata ya Kemambo Nyamongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, Bunini J. Bunini anadaiwa kufanya kitendo cha ukatili kwa kumpiga vipigo vikali mwananchi wake Joseph Wambura Philipo mwenye umri wa miaka 17 mkazi wa Kitongoji cha Sukube na kumsababishia kifo.

Pia anadaiwa kumtembezea kipigo Mandera Linus anayeendelea kupata matibabu Kituo cha Afya Nyangoto maarufu Sungusungu.

Familia ya Marehemu imesema kuwa Mwenyekiti huyo alifika nyumbani kwa marehemu Ijumaa, Mei, 05,2023 majira ya saa nne usiku na kumchukua Marehemu na kuondoka nae na kisha kumpiga na kumsababishia maumivu makali na hivyo kupoteza maisha.

Babu wa Marehemu Nyageta Mwita Nyageta amesema" Marehemu ni mkulima na anafanya vibarua vya ujenzi alikuwa anamdai bosi wake Jastini Gikaro Tsh. 80,000 pesa aliyomfanyia kibarua cha ujenzi baada ya kuifuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio.

      Babu wa Marehemu Nyageta Mwita Nyageta

"Yeye na mwenzake walienda kwa Jastini wanaemdai wakachukua saruji mifuko miwili wakiwa njiani walikutana na Ogunya Chacha Ogunya aliwashauri warudishe watapewa fedha wakarudisha lakini hakupewa.

" Kesho yake siku ya Ijumaa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja alikuja saa nne usiku nyumbani kwa marehemu akamchukua na kuondoka nae akampiga sana kisha akamwamuru arudi nyumbani kulala.

"Mwenzake aliyekuwa amelala nae Elias Masiaga Mwita ndiye aligundua kuwa amefariki, baba yake akuwepo alikuwa Dutwa na mama yake alikuwa Sirari nyumbani walikuwa watoto tu watatu yeye na wenzake.

Nyageta ameongeza kusema kuwa mbali na manyanyaso yanayotendwa na Mwenyekiti huyo wa Kijiji pia amekuwa akionesha hadharani Bastola anayoimiliki kwa lengo la kutishia watu hasa pindi anapokuwa amelewa.

"Mwenyekiti wa Kijiji alishaua pia watu wengine kwa vipigo vikali alishaua kwa vipigo mtoto wa Mwikwabe mzee wa mila na mtoto wa Sariro na hakuwahi kuwajibishwa" amesema Nyageta.

Baba wa Marehemu Wambura Philipo amesema kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti ni cha kinyama hivyo Serikali ichukue hatua kali ili kukomesha vitendo vya viongozi kujichukulia sheria mkononi na kufanya vitendo vya kinyama.

   Baba wa Marehemu Wambura Philipo akiwa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya wilaya ya Tarime kuliko hifadhiwa mwili wa mtoto wake 

"Mwenyekiti wa Kijiji alikuja nyumbani kwa marehemu akiwa ameongozana na watu watatu bila hata kuwa na Mwenyekiti wa Kitongoji wakamchukua mwanangu na kuondoka nae.

"Yule mwenzake Mandera amepanga nyumba kwa Bebi Linus kwao ni wilaya ya Serengeti anajishughulisha na kazi ya kuuza maji kwa kusafirisha kwa baiskeri ambao wote walipigwa na Mwenyekiti"amesema.

Baba wa Marehemu ameongeza kusema" Akampiga mwanangu vipigo vikali kisha mida ya saa tano usiku akamrudisha nyumbani, alifariki usiku akiwa amelala, mwenzake Elias aliyekuwa amelala nae aliamka saa 12 asubuhi akamwamsha ndipo akagundua ameshakufa.

"Unachukua mtu hata Mwenyekiti wa Kitongoji hajui alafu wanasingizia kuwa aliiba saruji na kwamba amekufa kwa kunywa dipu (sumu) yeye alijuaje kanywa sumu? Jumamosi asubuhi walifika manesi wawi wa Kituo cha afya Nyangoto na Askari Polisi mmoja hawakuwa na vipimo vyovyote wakasema marehemu kafa kwa kunywa sumu.

"Wakamshika wakamgeuzageuza kisha wakasema marehemu kanywa sumu, kama alikunywa sumu basi Mwenyekiti ndiyo alimnywesha sumu ili kufuta ushahidi kuhusika na kifo chake kwasababu alikuja kumchukua akiwa mzima akaondoka nae alipomrudisha ndipo akafariki" amesema Wambura.

Amesema mwili wa Marehemu umehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Tarime kusubiri kufayiwa uchunguzi huku akiiomba Serikali kuingilia kati suala la mwane kufariki baada ya kuchukuliwa na Mwenyekiti wa Kijiji.

Mjomba wa Marehemu Joram Silimia ameshangazwa kwa kitendo hicho cha kikatili kilichofanywa na kiongozi wa Serikali huku akiiomba Serikali kumchukulia hatua kali Mwenyekiti huyo wa Kijiji ili kuwa fundisho kwa viongozi wengine wanaojichukulia sheria mkononi.

Mjomba wa Marehemu Joram Silimia

Mashuhuda wafunguka

Shuhuda wa tukio hilo Mandera Linus anayeendelea kupata matibabu kituo cha afya Nyangoto amesema" Nilimuomba fedha Jastini Boss wetu nikamwambia naumwa naomba elfu tano nikanunue dawa akakataa akatuambia tokeni hapa.

" Yule mwenzangu marehemu akajisikia vibaya akaniambia hivi mtu akimchukulia simenti zake aende ajilipe ela zake, juzi marehemu alinifuata nyumbani akaniomba nimpe baiskeri akaniambia twende kwa Jastini kwasababu hataki kutupa ela yetu.

"Akapakia mifuko miwili ya simenti tukaondoka tulipofika karibu na kwa Ogunya akatuambia mbona mnachukua simenti tukamwambia sisi tunajilipa hii miwili kwasababu ndiyo ilikuwepo,akatueleza tusifanye hivyo twende tukatoe taarifa kwenye uongozi.

Shuhuda huyo ameongeza kusema" Tukarudisha saruji, kumbe wakati huo kulikuwa na mama mmoja akampigia simu Jastini, Jastini akatuma watu akawaambia mwambieni Mandera ananitafuta, jana mida ya saa nne usiku (Ijumaa) Rasi akanifuata nyumbani akaniambia unaitwa na kiongozi, nikamuuliza kiongozi gani akasema Jastini.

" Nikamwambia Jastini ni bosi wangu nikaenda nikamkuta amesimama kwa Ndeki, Jastini akampigia simu Marwa Bunini Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja akamwambia njoo na ile rungu yako.

" Mwenyekiti alikuja akiwa amelewa alikuwa kwa Bebi anakunywa bia akanipiga vibao na mbao za kenchi nikaanguka chini nikamwambia situende kwanza kwa Mwenyekiti wa Kitongoji nitoe maelezo, akamwambia Rasi nenda nyumbani uniletee spana.

"Rasi akaja na rungu Mwenyekiti akanipiga akachukua ubao uliokuwa na msumari akanipiga akanitoboa mguu kisha akaniambia tuende nyumbani kwao Jose ambaye ni Marehemu.

Mandera amesema walipofika kwao na marehemu Jose, Mwenyekiti wa Kijiji alimuamuru amwite" Tulipofika akaniambia mimi najificha (Mwenyekiti) wewe nenda umwite nikasema haya nikamwita yeye akiwa amejificha kwenye kona akaitika, Bunini akajitokeza akampiga na tofari akaanguka chini akasema ngoja amlegeze kwanza.

"Mimi nikafanya ujanja nikakimbia nikaenda kujificha kwenye kichaka, ilipofika mida ya saa 10 usiku kuna watu walipita njiani  nikaomba msaada wanipeleke nyumbani mmoja akanipeleka" amesema Mandera.

Elias Masiaga aliyekuwa amelala nyumbani chumba kimoja na marehemu amesimulia ilivyokuwa " Ilipofika saa tano usiku tukasikia Jose anaitwa akanyamaza akaitwa tena nikamwambia Jose unaitwa na Mandera maana hiyo sauti naijia ni ya Mandera aliyekuwa anafanya kazi na Jose 

"Jose akaitika akaamka akatoka nje akaniambia njoo ufunge mlango nilipochungulia nje nikamwona Mwenyekiti wa Kijiji amemshika Jose mkono, mkono mwingine ameshika rungu alafu Mandera alikuwa amekaa chini Mwenyekiti akampiga rungu tatu Mandera yeye akakimbia.

"Mwenyekiti akasema mkamateni kuna watu walikuwa na Mwenyekiti mmoja anaitwa Side,Elia msomba maji, Jastini bosi wa Marehemu,mzee Sungura na Rasi wakamkimbiza Mandera lakini aliwachenga hawakumpata.

"Waliondoka na Jose nami nikawafuatilia kwa nyuma umbali kidogo wakafika kwenye mji wa Jastini nyumba mpya anayojenga, Mwenyekiti akamwambia Jose kaa chini akawa anampiga anamuuliza kwanini wewe ni mwizi ?Jose akasema mimi sio mwizi akaendelea kumpiga virungu.

"Jose akakinga magoti kwa mikono akimpiga rungu anakinga magoti na mikono, Mwenyekiti alipoona amejikinga magoti akampiga rungu kichwani akawa anampiga kila mahali kisha akamfukuza ondoka rudi ukalale.

" Jose akaondoka lakini akazidiwa akashindwa kutembea akaniomba nimshikirie tukajikongoja tukiwa njiani akashindwa kutembea akakaa chini nikamsihi jikaze akajitahidi tukafika nyumbani akiwa na hali mbaya tukalala, ilipofika saa 12 asubuhi nikamwamsha aamke ndipo nikakuta ameshakufa." Amesema Elias.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sukube Kitemba Marembera Mwita amesema siku ya Jumamosi Mei, 5,2023 saa 12.30 asubuhi alifika nyumbani kwa marehemu na kukuta Jose akiwa amefariki.

" Nilipigiwa simu siku ya Jumamosi asubuhi alinipigia Domi  Philipo baba yake mdogo na marehemu akaniambia njoo nyumbani nikaenda nikakuta watu wengi nikauliza kuna nini nikaingia ndani nikakuta kweli amekufa.

"Nikampigia simu OCS ili waje waangalie wahoji kujua tatizo ni nini, Polisi wakaja wakahoji watu wakawachukua maelezo na mwingine aliyepigwa yupo hospitali na kuna vijana walikuwa wamelala na marehemu unaweza kuwauliza kilichotokea, tunasubiri majibu ya Polisi na Daktari" amesema Kitemba.

DIMA Online ikawasiliana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Bunini J. Bunini juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwake za kuwapiga wananchi wake vipigo vilivyopelekea mmoja kupoteza maisha huku mwingine akiendelea kupata matibabu Kituo cha Afya Nyangoto.

   Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Bunini J. Bunini

Mwenyekiti huyo amesema kuwa yeye hajahusika kumpiga na kwamba Marehemu alipigwa na watu baada ya kuiba saruji ambayo hakutaja idadi yake na kusema kuwa marehemu hajafa kwa kupigwa bali inasadikiwa amekufa kwa kunywa sumu.

"Ili tukio halijakaa vizuri kwa uhalisia hao vijana walikuwa wameenda kuiba Simenti kwenye mji wa mtu wakakutwa wakapigwa, sio kwamba walipigwa na wananchi wakaua walipigwa kawaida wakaomba msamaha wakawaachia.

" Sasa huyo mwenzake alienda kunywa sumu tusubiri tu ripoti ya Daktari itoke walienda kuiba kwa Jastini, mimi nakushauri hii habari ikiwezekana achana nayo tu. Taarifa ya uchunguzi ya awali iliyotoka ilisema huyo kijana amekunywa sumu hana sehemu aliyopigwa .

"Sasa familia ilikataa ikapeleka mwili wa Marehemu Hospitali ya wilaya ya Tarime kwa uchunguzi zaidi tusubiri hayo majibu yatoke tunaweza jumlisha na yale matokeo ya awali, mimi sijatuma mtu kuwapiga wala sijampiga mimi" amesema Bunini.

Kwa mujibu wa familia ya Marehemu wamesema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa Daktari katika hospitali ya wilaya ya Tarime Mei, 7,2023 na kuwaeleza kuwa marehemu alipigwa na kitu chenye ncha butu kichwani upande wa kulia na kumsababishia mauti.

Hata hivyo DIMA Online haikuweza kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo kwakuwa ulishamweleza Mwandishi wa habari kuwa wao si wasemaji bali msemaji ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji Tarime Gimbana Ntavyo ambaye nae alishamzuia mwandishi wa habari kufika ofisini kwake kumuhoji wala kuzungumza nae.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Tarime Rorya ACP Geofrey Sarakikya amesema hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

Mwili wa Marehemu  utasafirishwa leo kwenda Nyamongo kwa mazishi na utazikwa Mei, 9, 2023.

No comments