HEADER AD

HEADER AD

AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 39 KWA KOSA LA KUMTOROSHA MWANAFUNZI,KUBAKA, KUSHAWISHI

Na Samwel Mwanga, Itilima

MAHAKAMA ya wilaya ya Itilima katika mkoa wa Simiyu imemhukumu, Malimi Masinga(24)mkazi wa Kijiji cha Mwamugesha wilayani baada ya kupatikana na makosa matatu likiwemo la kubaka mwanafunzi.

Hukumu hiyo ya kesi ya jinsi Na.34/2024 imetolewa Julai 7 Mwaka huu na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Robert Kaanwa.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu,Kaanwa amesema kuwa mshitakiwa alikuwa alikabiliwa na mashitaka matatu ambayo kosa la kwanza ni kumtorosha binti chini ya miaka 16 bila ridhaa ya Wazazi kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 134 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura  ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika Kosa la pili la kubaka kinyume na kifungu cha 130(1)(2)e na 131(1) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Katika Kosa la tatu la kushawishi kutoa mwanafunzi kinyume na kifungu cha 60A(4) cha sheria ya elimu sura ya 353 kama ilivyo fanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Awali  ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Itilima, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jaston Mhule kuwa Juni 14 Mwaka huu katika gulio la Kijiji cha Ikindilo wilayani humo alimtorosha mwanafunzi wa kidato cha kwanza(jina limehifadhiwa) kwa nia ya kumuoa.

Mwendesha mashitaka,Mhule alizidi kuieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo aliondoka na mwanafunzi huyo  na kwenda naye Kijiji cha Matale na baadae kijiji cha Mbiti wilaya ya  Bariadi.

 Imedaiwa mshitakiwa aliishi nae kama mke na mme  kwa siku 25 hadi Julai 7 Mwaka huu alipo mpigia simu mzazi wa mwanafunzi kwa lengo la kumfahamisha nia ya kumuoa ambaye ni mwanafunzi na kisha alikamatwa Julai 8 Mwaka huu na  tarehe 8/7/2023 na kufikishwa kituo cha polisi Itilima. 

Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi Sita na vielelezo vitatu vilitolewa na upande wa mashtaka ili kuthibitisha makosa hayo.

Upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani tukio hilo lina madhara makubwa kwa mhanga kisaikolojia  pia matukio kama haya huacha kumbukumbu mbaya isiyo futika kirahisi katika maisha ya mhanga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na amemsababishia mhanga kukosa maarifa na ujuzi  ukizingatia serikali inatenga fedha nyingi ili watoto wote wapate maarifa na ujuzi kwa manufaa yao na taifa.

Mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza .

Hakimu Kaanwa alimhukumu mshitakiwa kwa kosa la kwanza kumtorosha binti chini ya miaka 16 kwenda jela miaka Sita,kosala pili kubaka kwenda jela miaka 30 na kosa la tatu kushawishi kutoa mwanafunzi kwenda jela miaka mitatu.

Amesema kuwa kwa jumla ya kifungo mshitakiwa amehukumiwa miaka 39 ila kwa kuwa adhabu zitakwenda kwa pamoja hivyo atatumikia miaka 30 jela.

 

No comments