HEADER AD

HEADER AD

WAKUU WA MIKOA, MAKATIBU TAWALA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI, NIDHAMU

Na Gustafu Haule, Pawani

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, amefungua mafunzo maalum ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Tanzania Bara na kuwataka wafanyekazi kwa kuzingatia maadili na nidhamu huku kila mmoja akiheshimu mipaka ya mwenzake katika  utendaji kazi zao za kila siku.

Aidha Dkt. Mpango, amesisitiza viongozi hao kushirikisha sekta binafsi katika mipango ya maendeleo na badala yake waache tabia ya kuzikumbuka taasisi za sekta binafsi pale wanapohitaji kuwezeshwa kwenye shughuli mbalimbali za kimkoa.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango( Wa pili kulia

Dkt.Mpango ametoa kauli hiyo Agosti 22, 2022  wakati akifungua mafunzo  ya viongozi hao yaliyoanza kufanyika leo katika Chuo cha  Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Kwa Mfipa chini ya ufadhili mkubwa wa benki ya NMB.

Amesema kuwa wapo baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu  Tawala ambao mara nyingi wanafanya kazi bila kufuata utaratibu na hivyo kuingiliana katika majukumu hali ambayo wakati mwingine inakwamisha shughuli za maendeleo kufanyika kwa wakati.

"Sababu ya kutoa mafunzo haya kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala ni baada ya kuona kuna mapungufu katika maeneo yao ikiwemo kutozingatia mipaka ya kiutendaji ambapo shida ipo katika suala la fedha kwani wakati mwingine Mkuu wa Mkoa nae anataka kuwa afisa masuhuri jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu,"amesema Dkt.Mpango

Amesema,mapungufu mengine ni pamoja na unyanyasaji katika utendaji kwani wapo viongozi wengine wamekuwa wakilazimisha masuala ya ngono kwa watendaji wa chini yao, kukosa mahusiano mazuri baina ya Chama,Wakurugenzi na taasisi nyingine.

Mpango, ameongeza kuwa dhima ya mafunzo hayo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 ambayo inaeleza umuhimu wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa hali shirikishi na kwamba kuanzia sasa kila Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala lazima wakatumie vyema mafunzo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

Kuhusu sekta binafsi ,Dkt.Mpango amesema kuwa mikoa mingi inafanya mambo yake bila kushirikisha sekta binafsi lakini wanapokuwa na shughuli zao kama unapofika wakati wa Mwenge wa Uhuru ndio wanakwenda kuwafuata kuomba mchango hali ambayo haina tija.

Amesema kuwa,inatakiwa sekta binafsi ipewe kipaumbele kila wakati katika shughuli zote za maendeleo hali ambayo itakuwa inajenga mahusiano mema baina yao na Serikali huku akipongeza Benki ya NMB kwa udhamini wa mafunzo hayo.

Amesema ,Benki ya NMB imefanyakazi kubwa ya kuhakikisha Wakuu wote wa Mikoa na Makatibu Tawala wanapata mafunzo hayo kwani ni wazi kuwa wameonyesha njia kwa upande wake sekta binafsi katika kushirikiana na Serikali.

"Nimesikia NMB ndio wafadhili wakubwa katika mafunzo haya,nami nichukue fursa hii kuwapongeza kwa jambo jema walilofanya na nawaomba tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha tunatoa huduma nzuri kwa jamii,"amesema Dkt.Mpango.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Angellah Kairuki,amesema  kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa yote Tanzania Bara  ili wawe na uwezo wa kusimamia wananchi.

Kairuki ,amesema malengo mengine ni pamoja na kuwawezesha kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kuboresha utendaji kazi wao na kwamba mpaka sasa wametoa mafunzo hayo kwa Wakuu wa Wilaya ,Maafisa Tarafa na watendaji Kata kote nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete, amesema kundi hilo ni kiungo muhimu katika utendaji wao na wanawakilisha utekelezaji wa Sera.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema kuwa baada ya mafunzo hayo anatarajia kuanza utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa sambamba na kuimarisha uongozi na kutunza siri za Serikali.

    Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Tanzania Bara wakifuatilia mafunzo maalum ya uongozi yalikuwa yakitolewa Agosti 22 katika Chuo Cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Kwa Mfipa.

Kwa upande wake mkuu wa idara  ya huduma za Serikali kutoka makao makuu ya  Benki ya NMB Vicky Bishubo,amesema kuwa NMB imekuwa mdhamini mkubwa pekee kutokana na mahusiano mazuri na Serikali kupitia ofisi ya Rais Tamisemi.

Bishubo,amesema kuwa baada ya kupata maombi juu ya ufadhili wa mafunzo hayo waliona ni kitu kizuri kinachojenga uongozi imara katika kuhudumia jamii na ndipo wakakubali kusaidia katika ufadhili.

   Mkuu wa Idara ya huduma za Serikali kutoka benki ya NMB makao makuu Vicky Bishubo akiwa na wasaidizi wake .

Amesema NMB inaona fahari kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali ikiwemo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akisema ushirikiano huo utakuwa endelevu.

Hata hivyo,Bishubo,amewaomba wananchi kuendelea kutumia benki ya NMB katika kufanikisha shughuli zao za maendeleo kwani huduma zake ni rahisi huku akisema faida wanayoipata lazima warudishe kwa jamii katika kuchangia katika masuala ya afya,elimu na mengine.


No comments