HEADER AD

HEADER AD

DCPC YAJIPANGA KUINGIZA MILIONI 121 KUTOKA KWENYE VYANZO VYA MAPATO

Na Andrew Chale, Dar es Salaam

KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) imefanya mkutano wake mkuu wa mwaka 2023 huku wakitarajia  kuingiza zaidi ya Sh  milioni 121 katika bajeti ijayo ya 2023/2024.

Akisoma taarifa ya matumizi na mapato ya Mwaka  2023/2024, mwishoni mwa wiki, Mweka hazina wa DCPC, Patricia Kimelemeta amesema kuwa,fedha hizo zitapatikana kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato ya klabu hiyo.

Amesema kuwa, lengo ni kuhakikisha inakua klabu kinara na kuleta maendeleo kwa wanachama wake, jambo ambalo litaweza kupunguza utegemezi.

"Katika bajeti ya mwakani,tumepanga kuingiza zaidi ya sh milioni 121 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato na kuhakikisha klabu inakua kinara na imara na kupunguza utegemezi, jambo ambalo litachangia kukuza uchumi wa wanachama na kuleta maendeleo ili kusonga mbele. 

"Fedha hizo zinazotolewa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) zitasaidia kulipa pango na matumizi ya ofisi," amesema Kimelemeta.

Amesema kuwa, katika  Mwaka wa fedha 2022/2023, klabu iliweza kuingiza zaidi ya Sh. milioni 45 ikiwa ni pamoja na michango mbalimbali ya wadau na ada za wanachama.

"Matarajio yetu DCPC mwaka ujao wa fedha itaingiza Sh. Milioni 121 ili kuwasaidia wanachama kupata mafunzo na semina mbalimbali za kiuongozi yatakayowaimarisha uwezo wao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku," amesema.

Ameongeza, " Awali, tulikua na wanachama 100, lakini siku zinavyozidi kuongezeka tumefika wanachama 150 na mkakati wetu ni kufika 250 ifikapo mwakani.

Aidha, ameishukuru UTPC kwa kuendelea kuiunga mkono kwa kuipatia zaidi ya Sh. 9,847,600 kwa ajili ya kugharamia kodi ya pango na shughuli nyingine za kiofisi.

Amesisitiza DCPC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa, fedha zinazotolewa zinasaidia waandishi wa habari kuongeza ujuzi na maarifa.

"Ili waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria, jambo ambalo litakuza weledi na uadilifu katika tasnia ya habari nchini.

Pamoja na hayo, Kimelemeta amesema uandishi ni taaluma inayoheshimika na kwamba ipo kwa mujibu wa Sheria, hivyo basi waandishi wanapopata mafunzo yatawasaidia kuwa bora zaidi katika kazi zao.

Amewashukuru Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), TASAF, Shirika la Nyumba la Taifa' (NHC), Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wadau wengine ambao kwa namna moja au nyingine wameiwezesha DCPC kwa hali na mali na kushirikiana nayo katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa'.

Kauli mbiu ya Mwaka huu ni ' Tasnia ya Habari Nguzo Muhimu kwa Ujenzi wa Taifa'.

No comments