MRADI WA 'BOOST' WAPUNGUZA MSONGAMANO WA WANAFUNZI DARASANI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MRADI wa BOOST wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi umeleta faraja kwa Wanafunzi,Walimu na Wananchi katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Ni baada ya kujengwa shule nane zilizokuwa na msongamano wa wanafunzi kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo madawati yamewekwa ndani ya madarasa sambamba na matundu ya vyoo.
Jumla ya Tsh. sh Bilioni 1.5 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo katika wilaya ya Maswa ambapo tayari ujenzi umekamilika wa shule mpya tatu na vyumba vya madarasa 13 na matundu ya vyoo 14 .
Jengo la Utawala katika shule mpya ya Msingi katika Kijiji cha Cha Jija wilaya ya Maswa iliyojengwa kupitia Mradi wa BOOST
Fedha hizo zikitolewa na Serikali pamoja na Benki ya Dunia na utekelezaji wa Mradi huu hapa nchini ni kwa miaka mitano kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2025/2026 na kuzinufaisha halmashauri zote 184 hapa nchini ikiwemo na halmashauri ya wilaya ya Maswa.
Wakizungumza na Waandishi wa habari kwa nyakati na maeneo tofauti tofauti waliotembelea shule nane zinazotekeleza mradi huo ili kujionea uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu kwa madarasa ya awali na msingi; Wanafunzi, Walimu na Wananchi wameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umewaletea faraja kubwa sana.
Wamesema kuwa shule hizo zimekuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi hata kuwafanya walimu washindwe kuwahudumia wanafunzi wao mmoja mmoja kwani kawaida darasa moja linapaswa kuwa na wanafunzi 40 lakini kwa sasa darasa moja limekuwa na wanafunzi zaidi ya 100.
Mojawapo na jengo ambalo ni vyumba vya madarasa katika shule mpya ya Msingi katika Kijiji Cha Shishiyu iliyojengwa kupitia Mradi wa BOOST
“Shule ya Msingi Ipililo B ina jumla ya wanafunzi 1429 na vyumba 9 tu vya madarasa hivyo kuwafanya wanafunzi zaidi ya 100 kusomea katika darasa moja, kwa hali hii huwezi kumsaidia mwanafunzi mmoja mmoja kutokana na wingi huo.
"Hivyo kujengwa kwa madarasa matatu ya kisasa kwenye shule yetu hii kupitia Mradi wa BOOST kwetu ni faraja itatupunguzia mrundikano huu wa wanafunzi kwenye darasa moja,”alisema Mwl Pili Sanane ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ipililo B.
Wameeleza kuwa kufuatia kutolewa kwa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule ya awali hadi kidato cha sita kumefanya ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi katika shule hasa za Msingi, na yote inatokana na mwamko wa wananchi kuwapeleka watoto wao shule huku serikali ikilia msisitizo jambo hilo.
Moja ya vyumba vya madarasa katika shule mpya ya Msingi katika Kijiji Cha Mwakabeya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kupitia Mradi wa BOOST
“Baada ya serikali kutoa elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi kidato cha sita kumekuwa na wimbi kubwa la uandikishaji hasa wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa shule za msingi.
" Hali hiyo imeendelea kwa kasi ndiyo maana leo kwenye shule yetu ya Jija A tuliletewa fedha na tumejenga shule nyingine mpya yenye mikondo miwili miwili hii kwetu sisi ni faraja kubwa sana maana wanafunzi wengine watahamia kwenye hii shule mpya,”amesema Mathayo Bujenja ambaye ni Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Jija A.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nguliguli,Mwl Rameshi Moses amesema kuwa licha ya shule yake kujengewa madarasa mawili pamoja vyoo vimesaidia kupunguza mlundikano wa muda mrefu hasa nyakati za mapumziko wanafunzi wamekuwa wakitumia muda mrefu kujisaidia.
Wanafunzi wa darasa la NNE katika shule ya Msingi Mwakabeya wilaya ya Maswa wakiwa wamekaa chini kwa ukosefu wa madawati na upungufu wa vyumba vya kusomea hali iliyopelekea serikali kuwajengea shule mpya yenye madawati kila darasa kupitia Mradi wa BOOST
“Katika vyoo tulikuwa na mrundikano mkubwa wa wanafunzi hasa wakati wa mapumziko walikuwa wakijipanga foleni ili kuingia chooni kujisaidia, walikuwa wanatumia muda mwingi sana.
" Sisi muda wetu wa mapumziko ni dakika 20 tu lakini kutokana na hali hiyo inabidi tutumie muda zaidi ya huo uliowekwa na serikali ila kwa sasa hali hiyo imepungua baada ya vyoo kukamilika,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ambazo mradi huo unatekelezwa wamesema kuwa kwa sasa wamepata faraja kubwa kutokana na kusoma katika mazingira rafiki ambayo kwa sasa mrundikano katika darasa moja umepungua sambamba na kusoma wakiwa wamekaa kwenye madawati.
Wanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Nguliguli wilaya ya Maswa wakiwa kwenye darasa lenye madawati lililojengwa kupitia Mradi wa BOOST
“Darasani tulikuwa tunasoma tuko wanafunzi wengi katika darasa moja na pia tulikuwa wengine tunakaa chini ya sakafu lakini kwa sasa tuko kwenye darasa jipya tunasoma vizuri na tunakalia madawati hivyo hata kujifunza kwetu kumekuwa ni kuzuri sana,”amesema Msabi Yoha ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwakabeya.
Naye Charles Malinzuri ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Igunya amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo katika shule yao hakuna hata mwananchi mmoja aliyechangishwa kiasi cha fedha tofauti ilivyokuwa siku za nyuma wakikimbizana na wananchi katika michango ya ujenzi wa shule hivyo ameishurukuru sana serikali kwa kutekeleza maradi wa BOOST.
Darasa la Elimu ya Awali katika Kijiji cha Shishiyu wilaya ya Maswa likiwa na moja ya Vifaa vya kuchezea Watoto lililojengwa kupitia Mradi wa BOOST.
“Sisi hapa Igunya kwa kweli tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutuletea mradi huu wa BOOST maana hakuna hata mwananchi mmoja ambaye amechangishwa kiasi chochote cha fedha na tumejengewa madarasa ya kisasa haku na ile hali ya kukimbizana na wananchi kwa ajili ya michango kama ilivyokuwa huko kwa siku za nyuma,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuipatia halmashauri hiyo kiasi cha Sh Bilioni 1.5 katika sekta ya elimu kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya elimu ya Awali na Msingi kupitia mradi wa BOOST.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akizungumza na Waandishi wa habari (hapo pichani)juu ya utekekezaji wa Mradi wa BOOST katika wilaya hiyo
Amesema kuwa wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Uchaguzi ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi wameweza kutekeleza Mradi huo na kuyagusa majimbo yote kulingana na uhitaji kwa kila eneo.
Katika wilaya ya Maswa mradi wa BOOST kwa jimbo la Maswa Magharibi umetekelezwa kwa kujenga Vyumba vya madarasa Viwili na Matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Igunya kwa gharama ya Sh 56,300,000.
Shule mpya ya Msingi yenye mikondo Miwili katika kijiji cha Jija kwa gharama ya Sh 540,300,000, Vyumba viwili vya madarasa na darasa la Awali la mfano kwa gharama ya Sh 69,000,000 katika shule ya msingi Mwabayanda na Shule mpya ya msingi yenye mkondo mmoja mmoja katika kijiji cha Shishiyu kwa gharama ya Sh 348,500,000.
Mwonekano wa baadhi ya Majengo ya shule mpya ya Msingi katika Kijiji Cha Mwakabeya wilaya ya Maswa kupitia Mradi wa BOOST.
Kwa upande wa Jimbo la Maswa Mashariki wameweza kutekeleza mradi wa BOOST kwa kujenga Vyumba Vitatu vya Madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Ipililo B kwa gharama ya Sh81,300,000, Shule mpya ya msingi yenye mkondo mmoja katika kijiji cha Mwakabeya kwa gharama ya Sh348,500,000, Vyumba Vitatu vya madarasa na matundu matatu ya vyoo.
Pia katika shule ya msingi Ngudu zimetumika gharama ya Sh 81,300,000 na Vyumba Viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Nguliguli kwa gharama ya Sh 56,300,000.
Aidha amesema kukamilika kwa mradi huo katika maeneo hayo kwenye halmashauri hiyo kutapunguza mrundikano wa wanafunzi kwenye shule hizo ambazo pia vyumba vya madarasa vimewekewa madawati sambamba na kuboresha mazingira ya kufundishia kwa walimu hasa kwenye madarasa ya Awali.
Vyumba vitatu vya madarasa vikivyojengwa na Mradi wa BOOST katika shule ya Msingi Ipililo B iliyoko wilaya ya Maswa.
Mwl Mathayo Bujenja ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi ya Jija wilaya ya Maswa iliyojengwa na serikali kupitia Mradi wa BOOST akizungumza na Waandishi wa habari (hapo pichani)walipotembelea shule hiyo.
Post a Comment