PROF. MHANDO ANG’ATUKA ZIFF,SHIVJI AKABIDHIWA MIKOBA YAKE
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Zanzibar [ZIFF] limemtambulisha rasmi mwongoza filamu Amil Shivji kuwa Mkurugenzi mpya wa tamasha hilo, ambalo ni miongoni mwa matamasha kongwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwa na umri wa miaka zaidi ya 26.
Utambulisho huo umefanyika Oktoba, 8, 2023. Awali akizungumza wakati wa kukabidhi nafasi hiyo, Prof. Martin Mhando , Mkurugenzi wa tamasha anayemaliza muda wake, amesema, ‘’Mtengenezaji filamu huyo mchanga na mwenye utashi ndiyo chachu inayohitajika ili kulihuisha tamasha ambalo limeonesha dalili za kuchakaa katika miaka ya hivi karibuni.
Hivyo namtambulisha kwenu Amil Shivji, mtayarishaji mashuhuri na kazi zinazosifika kama vile ‘Vuta N’kuvute’ [2022] na ‘T-Junction’ [2017].
Ni mwana maono ambaye anaamini katika kutumia nguvu ya filamu kukosoa kanuni zilizopo na kuangazia mapambano ya jamii, hasa zisizo na uwezo.’’ Amesema Prof. Mhando.
Aidha, amemuelezea Shivji kuwa ni msomi aliyefuzu katika Chuo Kikuu cha York na mwenye Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Utayarishaji wa Filamu kutoka Toronto, Canada.
Pia, Amil ndiye mwanzilishi wa Kijiweni Productions, taasisi ya utayarishaji filamu iliyojipambanua katika kusimulia hadithi kwa viwango vya kimataifa.’’ Amesema Prof Mhando.
Ameongeza kuwa, Chande Omar, Mwenyekiti wa ZIFF na msanii mkongwe wa filamu, alionyesha imani yake kwa Shivji, akisema analeta maono mapya yanayoendana kikamilifu na kaulimbiu ya ZIFF ya 2024 ya 'Kuhuisha.
"Haiba yake na dhamira yake itahamasisha kila mtu kuungana na kuiweka ZIFF katika viwango vipya." Amesema Prof Mhando na kumalizia kuwa ameamua kung’atuka katika nafasi hiyo aliyodumu kwa muda wa miaka zaidi ya 15.
‘’Tamasha hadi sasa linatimiza miaka 26, Nimedumu kwa muda wa miaka 15. Mimi nimeoa nina miaka 26 hivyo kwa umri huu sasa ni mkubwa naamua nikae pembeni kupisha damu changa"amesema.
ZIFF tulianzisha kurejesha kasi ya kuangalia filamu, lakini pia tulijikita katika kukuza na kuinua uandaaji wa filamu hivyo kazi hii ni kubwa na inatakiwa kuendelezwa na vijana’’ amesema Prof. Mhando.
Kung’atuka kwangu sio kama nimechoka, bali kuendeleza mawazo mapya,naamini uwezo wa Amil Shivji na ni mtu ambaye naamini anaweza na ataongoza taasisi muhimu hii ya ZIFF.’’ Amesema Prof Mhando.
Kwa upande wake, Amil Shivji amepokea nafasi hiyo kwa mikono miwili huku akiomba ushirikiano kwa wadau na watu wote katika tasnia ya filamu.
‘’Nashukuru kwa nafasi hii tokea nimekuja kama mshiriki wa tamasha na kuingiza filamu yangu kwa mara ya kwanza na kushinda, lakini pia ZIFF ndio iliyonipokea na kunilea.
"Kwa zaidi ya miaka 10, ZIFF imenijenga na kukuza taaluma yangu hii kwani mara ya kwanza hakuna aliyenielewa tokea kuleta filamu yangu ya kwanza iliyokuwa ya dakika 14, mwaka 2013.
"Nimekuzwa na nimeendelea kujikuza, naamini ZIFF sio tu tamasha bali ni chuo na nawashukuru wote akiwemo Prof Mhando na watendaji wengine wote tunamomba aendelee kutushika mkono’’ Amesema Amil Shivji.
Shivji amesema kuwa, ZIFF sio tu tamasha bali ni taasisi inayofanya kazi kwa muda wa mwaka zima kila mwaka, hivyo Vijana wanaotaka kujifunza wanakaribishwa ZIFF watajifunza vingi, iwe kuandaa filamu ama kupiga picha ama kuandika mswada.
"Sote kwa pamoja, tuhakikishe ZIFF inaendelea vizuri, tutahakikisha tutakuwa na mabadiliko mengi ilikuwa na mtazamo wa vijana, na kuwa na mtazamo tofauti zaidi, lengo kuvuta watu wote kuja ZIFF kutoka Mataifa yote kuleta filamu na hata kuja kuangalia filamu.’’ Amesema Amil Shivji.
Amesema tamasha sio kuandaa kwa ajili ya wasanii kushinda tuzo, tamasha ni njia ya kutazama filamu, hivyo watayarishaji na wasanii wa Bara na Zanzibar na Nchi zote za Afrika na Ulaya ni nafasi yenu ya kuleta filamu zaidi.’’ Amesema Shivji.
Shivji amesema dhamira yake kwa sasa ni kuona linaendelea kuwa tamasha bora zaidi duniani.
"Tunahitaji kuliweka tamasha hili sawa na matamasha bora zaidi barani Afrika na duniani. Zanzibar ina mambo yote ya kuifanya ZIFF kuwa tukio kuu barani Afrika, na hilo litakuwa lengo langu katika miaka ijayo
Natoa wito kwa wapenda filamu wote wa Tanzania, mashirika ya serikali, na viongozi wa mashirika kuunga mkono ZIFF na kuhakikisha inabakia na nafasi yake kama kinara wa utamaduni katika Afrika Mashariki." Amesema Shivji.
Shivji amesema kuwa, ushawishi mkubwa ni kuibua midahalo muhimu katika tasnia ya filamu Tanzania, na kusogeza tasnia mbele.
ZIFF, inajivunia tamaduni tajiri za Bara la Afrika, India, Pakistan, Mataifa ya Ghuba, Iran, na visiwa vya Bahari ya Hindi, na huhusisha pia mashindano ya kimataifa ya filamu, muziki, sanaa za maonyesho, warsha, semina, makongamano, na programu za kitamaduni.
Post a Comment