RC MARA AWAOMBA WANANCHI KUJITOKEZA KUELEZA KERO ZAO WAKATI WA ZIARA YA WAZIRI MKUU
Na Jovina Massano, Musoma
MKUU wa Mkoa wa Mara Said Mtanda amewaomba wananchi katika wilaya za mkoa wa Mara kujitokeza na kueleza kero zao wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Akizungumza na Wandishi wa Habari Februari, 24, 2024 ofisi ya mkuu wa mkoa, amesema kuwa Waziri Majaliwa atakuwa Mara Februari, 25-29, 2024 ambapo atafanya ziara katika wilaya za mkoa huo.
RC Mtanda amesema kuwa Waziri mkuu anatarajia kukagua, kuweka mawe ya msingi, kuzindua miradi mbalimbali ya Maendeleo, kuhutubia wananchi na kusikiliza kero zao sambamba na kuzungumza na watumishi pamoja na viongozi mkoani Mara.
" Nawaombeni wananchi wa mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kumpokea Waziri Mkuu na mtoe kero zenu. Ziara hii ni moja ya majukumu yake ya kiserikali ambapo atapata wasaa wa kuzungumza na viongozi na watumishi wa serikali na kuhutubia wananchi.
" Ziara itakuwa ya ukaguzi sambamba na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ambayo itahusisha sekta ya Afya, elimu, utawala na miundombinu" amesema RC Mtanda.
Mtanda amesema kuwa mapokezi hayo yanafanyika leo Februari, 25,2024 majira ya mchana eneo la Ndabaka wilayani Bunda na kuelekea makao makuu ya mkoa katika ukumbi wa uwekezaji kupokea taarifa ya Maendeleo ya mkoa.
Amesema Februari 26, 2024 Waziri mkuu atakuwa wilayani Bunda, atakagua shule ya msingi Sabasita na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mata.
Amesema atazindua mradi wa maji wa Sazira, atasalimiana na wananchi wa eneo hilo baadae atazungumza na watumishi wakiwemo viongozi na kuelekea uwanja wa shule ya msingi Miembeni kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wilayani hamo.
RC Mtanda amesema ziara itaendelea Februari 27, 2024 katiaka Wilaya ya Butiama, wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya wilaya ya Tarime ambapo kutakuwa na zoezi la kukagua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Butiama.
Atazungumza na watumishi wakiwemo viongozi pia atawasalimia wananchi na kuelekea Mwitongo kuzuru kaburi la hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusalimiana na wanafamilia waliopo hapo.
Ziara itaelekea wilayani Serengeti ambapo Waziri mkuu ataweka jiwe la msingi katika ujenzi wa zahanati ya Getarungu, ataelekea Tarime vijijini ambapo ataweka jiwe la msingi katika jengo la halmashauri hiyo na kusalimiana na wananchi eneo la Nyamwaga.
Mkuu huyo wa mkoa amesema Februari, 28, 2024 ziara itaendelea wilayani Rorya ambapo atakagua miradi wa maji kijiji cha Komuge, atatembelea na kukagua na ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkutano wa hadhara eneo la Utegi.
Amesema baada ya mkutano Utegi msafara utaelekea wilayani Tarime eneo la Sirari na kufanya mkutano wa hadhara kisha ataweka jiwe la msingi katika soko la kimkakati Tarime mjini na kufanya mkutano wa hadhara uwanja wa Serengeti.
Amesema atahitimisha ziara yake Februari 29, 2024 wilayani Musoma kwa kukagua ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma Manispaa na kuelekea halmashauri ya Musoma vijijini kuweka jiwe la msingi jengo la halmashauri hiyo.
Pia atapata wasaa wa kuzungumza na watumishi wakiwemo viongozi na ataelekea Kijiji cha Bwai katika mkutano wa hadhara kuongea na wananchi baada ya mkutano huo atahitimisha ziara yake katika mkutano wa hadhara uwanja wa shule ya sekondari Mara Manispaa ya Musoma.
Post a Comment