HEADER AD

HEADER AD

KILIMO CHA PATA POTEA KINAVYOWATESA WAKULIMA WANAOPAKANA NA MTO MARA

Na Dinna Maningo, Tarime

KUNA Methali ya Kiswahili inasema ' Jembe halimtupi mkulima', ikiwa na maana kwamba mtu yeyote anayekubali kushika jembe na kwenda kulima lazima atavuna mazao.

Methali hii huleta matumaini na hamasa kwa wakulima kuendelea kushawishika kujishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali wakiwa na uhakika wa kuvuna mazao, ili yawasaidie kwa chakula na kuuza kwa ajili ya kujipatia fedha kuendesha maisha yao.

Mkulima anapolima mazao anategemea avune na apate faida na pale asipovuna basi methali hiyo haina maana tena kwakuwa haijatimiza makusudio ya mkulima aliyoyawekeza katika kilimo.

Kwa miaka kadhaa Wakulima Nyamongo, wilayani Tarime, mkoa wa Mara wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na Mto Mara, wamekuwa wakipata hasara katika msimu wa mvua nyingi kwakuwa mto Mara hufurika na kuacha mkondo wake na maji kutapakaa kwenye mashamba ya wakulima.

Maji kutoka mto Mara yakiwa yamevamia mashamba na kusomba mazao

DIMA Online
imefika katika baadhi ya mashamba kijiji cha Matongo kushuhudia jinsi Mto Mara ulivyoathiri mazao hususani zao la mahindi na kuzumgumza na wakulima.


Yakobo Sitta ni mkulima mkazi wa Kitongoji cha Kwinyunyi katika kijiji cha Matongo anasema mto Mara umempa hasara baada ya mazao yaliyokuwa yamekomaa kusombwa na maji.

" Mimi ni msukuma kwetu ni Bariadi nilikuja Nyamongo mwaka 2014 kutafuta maisha, nikafanya kibarua kwa mtu cha kuendesha trekta kuwalimia watu mashamba. Niliamu kujitegemea nikalima mahindi ekari 28 , nimevuna ekari nne, nikapata gunia 40 nilizofanikiwa kupeleka nyumbani.

Anaongeza kusema " Nilivuna ekali zingine 18 za mahindi na kurundika shambani ili nitafute gari la kuyapakia yasafirishwe kwenda nyumbani, lakini yote yamesomba na mto Mara, na yaliyobaki shambani ambayo hayajavunwa maji yamejaa na mvua inaendelea kunyesha maji yanaongezeka" anasema Sitta.

             Mahindi yakivunwa ndani ya shamba lenye maji yaliyotoka mto Mara

"Tunaomba Serikali itusaidie wakulima tupate kifuta machozi, mitaji yetu imefia majini, nilinunua mbegu za mahindi mifuko 110, ambapo mfuko mmoja wa kilo mbili ni sh. 14,000, palizi ekali moja sh. 50,000.

" Ukirudia palizi ni sh. 40,000 kwa ekari, kulima kwa trekta ekari moja sh.70,000 bado matumizi mengineyo. Jumla nimetumia sh.milioni 18 alafu mazao yamesombwa na maji, sina mtaji" anasema Sitta.

John Ntora anasema " Mimi ni mkulima wa mazao mbalimbali tumekumbwa na changamoto ya mafuriko ambayo yameletwa na mto Mara.

John Ntora

"Nimelima ekari 13 za mahindi kila ekari kulima kwa trekta ni sh 60,000 na gharama zingine za shamba chakusikitisha mazao yamesombwa na maji" anasema Ntora.

Apson Marwa anasema alilima ekari tatu za mahindi na amefanikiwa kuvuna gunia tatu pekee, mazao mengine yamesombwa na maji.

Apson Marwa

Naomi Marwa Gibare (72) anasema licha ya umri wake bado anajishughulisha na kilimo cha mahindi na viazi vitamu, anasikitika maji kuharibu mazao.

             Naomi Marwa Gibare

"Mgodi wa Barrick ulihamisha watu kutoka kwenye makazi yao ya asili ukawalipa fidia, kwakuwa maeneo ni machache wakasogea na kujenga jirani na mto Mara,

"Tumepakana na mto, nimelima mahindi na viazi maji yameharibu, Rais Samia tusaidie sisi wazee tutakufa kwa njaa " anasema Naomi.

Gidion John ni mkazi wa Kitongoji cha Kegonga B ni mwalimu wa shule ya awali binafsi (Chekechea) anasema watoto anaowafundisha wazazi wao ni wakulima na kila mtoto malipo ni sh.10,000 kwa mwezi.

Gidion John

Anasema kwamba uchumi wake utayumba maana wazazi watakosa pesa za kumlipa kwakuwa mazao yameharibika.

Limbu Koni anasema " Mimi ni mzaliwa wa Bariadi nilikuja huku kutafuta maisha nikawa nafanya vibarua vya kupalilia mashamba.

Limbu Koni

" Mwisho wa siku nami nikapata shamba langu lililopo mita 70 kutoka mto Mara nikalima ekari 6 kati ya hizo tatu zimesombwa na maji zilizobaki nimeshindwa kuvuna kwasababu maji yamejaa" anasema Koni.

DIMA Online imeshuhudia karavati katika barabara inayokwenda mashambani eneo la Timbo likiwa halionekani baada ya kufunikwa na maji yaliyotoka mto Mara na kusababisha watu kuvuka kwa kuogelea na kutembea majini.

Elias Marwa Makara mkazi wa Kitongoji cha Kwinyunyi anasema " Unaniona na hili panga mkononi, nilikuwa naenda kufeka mahindi yaliyokauka ili yavunwe lakini nimeshindwa kuvuka maji yamejaa karavati halionekani nimeogopa kuvuka " anasema Marwa.

Elias Marwa Makara

Suzana Range anasema " Mafuriko haya yamesababisha wenye punda wamegoma kutoa punda kubeba mahindi wakihofia kupelekwa na maji.


"Inabidi tusombe kwa vichwa kuja nchi kavu na ni mbali tangu saa 12 asubuhi sasa ni saa saba bado tunahangaika kuvusha chakula" anasema Suzana.


Bahati Marwa anaiomba serikali iwasaidie kuokoa chakula kilichokauka kutoka mashambani kwa kutumia mitumbwi.


"Wakulima tunateseka sana mvua iliwa nyingi hatuna uhakika wa chakula ,tunaiomba serikali ione namna ya kutusaidia kutoa mazao yetu shambani ambayo yamevamiwa na mto Mara" anasema Bahati.

Marwa Amos anasisitiza serikali iwasaidie namna ya kutoa mazao yao shambani kwakuwa hawana namna ya kuokoa mazao na hivyo kuendelea kuozea shambani.


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A Matinde Matiko anasema mto usingefurika maji wakulima wangevuna mazao mengi kwani mengine yalikuwa katika harakati za kuvunwa.

"Tukikumbwa na njaa sisi akina mama na watoto ndio tunateseka, tunategemea kilimo kwa chakula na mahitaji mengine.

"Huwa tunaona mikoa mingine kukitokea mafuriko viongozi wakubwa wanaenda kuwatia moyo lakini huku kwetu hatuoni viongozi wakifika kutuona" anasema Matinde.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwinyunyi Daniel Isaroche anasema Kitongoji chake kimepakana na mto Mara na mazao mengi yameathiriwa na maji.

Anaiomba Serikali inayoongozwa na Rais Samia kuwasaidia pembejeo za kilimo kama njia ya kuwapunguzia maumivu.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwinyunyi Daniel Isaroche

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabichune Mgaya Kisire anasema zaidi ya ekali 200 zimesombwa na maji na kwamba kijiji chake kina uhaba wa ardhi kwakuwa maeneo mengine yanatumika kwa shughuli za wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

"Mto umekuwa ukileta shida kuna mwananchi wangu ana mashamba kijiji cha Matongo alivuna viroba 70 vya mahindi akarudi nyumbani ili afate punda wakapakie mahindi alipofika shambani akakuta viroba vyote vimepelekwa na maji" anasema Kisire.

Katibu Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo ambaye ni mkulima katika kijiji cha Matongo, anasema kuwa zaidi ya ekari 2,000 za zao la mahindi katika kijiji hicho zimesombwa na maji.

Katibu Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo

" Kijiji cha Matongo kina wakazi zaidi ya 7,000. Naishukuru DIMA online kufika na kushuhudia mafuriko tunaomba mtupazie sauti zifike kwa viongozi waje watusaidie" anasema Sadock.

Nimategemeo yetu chombo hiki cha habari kitafikisha kero zetu ili serikali itusaidie kutatua hii kero ya kila mara maji kufurika kwenye mazao " anasema Maningo.

Afisa Kilimo Kata ya Matongo Godwin Swai, anasema ekari 348 za mahindi katika kijiji cha Matongo na Ekari 82 za mahindi katika kijiji cha Nyabichune zimesombwa na maji ya Mto Mara.


"Msimu wa mwaka jana ambao mavuno ni sasa watu wamelima sana tangu nihamie Nyamongo, msimu uliopita hawakuvuna sana hali ya hewa haikuwa nzuri kwa baadhi ya maeneo.

Anaiomba Serikali kuona namna ya kuwasaidia wakulima ambao mazao yao yameharibika na mengine kusombwa na maji na kwamba kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha huwenda mazao yaliyosalia shambani nayo yakazidi kuaathirika.

Afisa Kilimo Halmashauri ya wilaya ya Tarime Sylvanus Gwiboha anasema ofisi ya kilimo kwa kushirikiana na taasisi zinazoshughulika na bonde la mto Mara ilikwisha toa elimu kuhusiana na sheria ya vyanzo vya maji lakini pia athari za kulima maeneo ya njia ya maji.

          Maji yakiwa yametapakaa kwenye mashamba

Anasema historia ya mto Mara inafahamika kwa kuwa na tabia ya kufurika na kutupa maji yake kando ya maeneo ya mto hasa kipindi cha msimu wa mvua nyingi.

" Baadhi ya maeneo katika kata ya Kemambo kuna upandaji wa bikoni za mipaka ya mto Mara kwa kushirikiana na jamii zinaendelea, ili wananchi waweze kuhifadhi chanzo hicho ambacho kinategemewa si kwa taifa letu pekee bali hata nchi jirani ya Kenya kwa shughuli mbalimbali.

" Ili kuendelea kulinda chanzo hicho imewekwa siku maalum ya kukutana wadau na kutathimini maendeleo ya utunzaji mto, siku inaitwa 'Mara Day' inayoazimishwa kila tarehe 15, Septemba ya kila mwaka kwa kushirikiana na nchi jirani ya Kenya.

Gwiboha anaeleza sababu za wananchi kuendelea kulima mazao karibu na mto Mara licha ya mto kuathiri mashamba mara kwa mara.

       Mazao yakiwa yameharibiwa na maji

"Wakulima bado wanaendelea kufanya shughuli zao kando ya mto Mara kwa sababu ni rutuba ya eneo husika 'alluvial soils' zina virutubishi vya kutosheleza kulima mpaka kuvuna pasipo kutumia mbolea.

" Sababu nyingine ni wakulima wa zao la mahindi ya muda mfupi na kuyauza yakiwa mabichi kama biashara wakitumia chanzo hicho cha maji kumwagilia, sambamba na kilimo cha mboga. Inapotokea msimu umebadilika wanapata hasara." anasema Gwiboha.

Afisa huyo wa Kilimo anawaomba Wakulima wanaolima kando ya mto Mara waache na kuheshimu sheria na kanuni zilizopo za uhifadhi wa vyanzo vya maji ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo kutokana na matumizi ya kemikali za kudhibiti wadudu.

         Mkulima akivuka maji yaliyotoka mti Mara na kutapakaa kwenye masham

"Watafite maeneo mengine rafiki kwa kilimo, maeneo hayo yanawapa hasara, watakapoacha watakuwa wamelinda viumbe vinavyoishi ndani ya mita 60 toka mtoni vyenye manufaa katika maisha ya viumbe hai vyenyewe na vingine vinavyotegemeana katika mfumo wa Ikolojia (Ecosystem).

Mbali na Mto Mara kuathiri mazao Nyamongo umesomba mazao katika kata zinazopakana na mto huo wilayani Tarime na mazao ya wakulima wa wilaya ya Serengeti ambao mashamba yao yamepakana na mto Mara.

Paul Mahandare akivuna mahindi kwenye shamba lake lililoharibiwa na mafuriko ya mto Mara

Punda wakiwa wamebeba mahindi wakitokea shambani wakipitakwenye karavati lililofunikwa na maji ya mto Mara.
           
   Mfugaji akitoa kero yake ya mafuriko mto Mara
       Mkulima akitoa kero yake ya mafuriko mto Mara



         Mashamba yaliyoharibiwa na maji kutoka mto Mara

         Mahindi yaliyovunwa yakiwa yameharibika baada ya mto Mara kufurika maji na kusambaa mashambani
















































No comments