HEADER AD

HEADER AD

JUMUIYA YA WAZAZI MARA YAWASISITIZA WAZAZI KULEA WATOTO KATIKA MAADILI MEMA


Na Dinna Maningo, Butiama


JUMUIYA ya Umoja wa Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara, imewasisitiza wazazi kuwa karibu na watoto wao wawapo nyumbani na shuleni pamoja na kushirikiana na walimu katika kulinda maadili ya watoto na vijana.

Hayo yameelezwa juzi wakati Jumuiya ya wazazi ya mkoa huo ikiwa katika maadhimisho kuelekea siku ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Februari, 5, mwaka 1977, yaliyoadhimishwa wilayani Butiama.

      Walioketi mbele, kushoto ni Kangi Lugola na Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Mara, Julias Masubo

Jumuiya ya wazazi ilitoa elimu ya malezi kwa wazazi wa jumuiya hiyo na kwa wanafunzi na walimu katika shule ya sekindari Bumaswa Kata ya Bwiregi kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya jumuiya.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Mara, Julius Kambarage Masubo amesema kwamba malezi ya mtoto huanzia nyumbani hivyo wazazi wanatakiwa kulea watoto katika maadili mema.

        Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Mara, Julius Kambarage Masubo

"Sisi kama jumuiya ya wazazi tunashughulika na malezi, elimu na mazingira. Malezi yanaanzia nyumbani kwa wazazi wanakoishi watoto, baada ya hapo wanakabidhi walimu nao wanaendelea kukuza malezi yao wawapo shuleni, wakishamaliza shule jamii inakuwa na jukumu la malezi, sote tushirikiane katika malezi" amesema Masubo.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya wazazi katika mkoa huo, Nyihita Willfred Nyihita amesema jumuiya ya wazazi ina wajibu wa kuhakikisha inaongoza watoto na kuwalea katika misingi inayotakiwa.

        Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya wazazi katika mkoa huo, Nyihita Willfred Nyihita.

"Jumuiya ya Wazazi tumekuja Butiama kutoa elimu ya malezi kwakuwa ni jukumu la jumuiya kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na maadili mema" amesema.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM mkoa wa Mara, na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi na Mbunge wa jimbo la Mwibara, Kangi Lugola aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kuelekea siku ya kuzaliwa CCM, amesema simu na runinga zimechangia kuporomosha maadili ya watoto.

               Mjumbe wa mkutano mkuu mkoa wa Mara,  Kangi Lugola

"Nitoe wito kwa wazazi wenzangu sisi ndio tuna dhamana kwenye jumuiya hii tujitahidi kudhibiti watoto kwenye matumizi ya simu na vipindi visivyo faa kwa watoto vinavyorushwa kupitia runinga.

"Tuwaepushe na michezo ya kubeti, kuchezea kompyuta kwani vitu hivi vinachangia sana kubadili tabia za watoto, mtoto anakaa hadi saa saba usiku kuangalia mpira muda ambao angelala, na wengine wanabeti badala ya kujisomea " amesema Lugola.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Butiama, Baraka Imanyi maarufu 'Obama' amesema kuwa maadili ni suala mtambuka na jumuishi, hivyo wazazi, walimu na jamii wanapaswa kushirikiana katika malezi.

      Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Butiama, Baraka Imanyi maarufu 'Obama

Mwanafunzi wa shule ya sekondari Bumaswa Christina Matiku amewaomba wanafunzi wenzake kutojihusish na vitendo viovu na badala yake wajikite katika masomo kwakuwa elimu ndio ufunguo wa maisha
.

"Nawaomba vijana wenzangu tusome kwa bidii tusikubali kujiingiza katika vishawishi ambavyo vitahatarisha maisha yetu, tuwe na maadili na tuheshimu wazazi na walimu" amesema Christina.

         Mwanafunzi wa shule ya sekondari Bumaswa Christina Matiku


Tazama Video 




No comments