AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KUBAKA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAHAKAMA ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imemhukumu Mboje Paul (28) mkazi wa kijiji cha Ipuya mkoa wa Singida kwenda jela miaka 30 na kulipa fidia ya Tsh 300,000 baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kubaka.
Hukumu hiyo imetolewa Juni,10, mwaka huu na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Azizi Khamis katika kesi ya jinai Namba 3886/2024 baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka dhidi ya mshitakiwa huyo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mashitaka ya Taifa wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo mwezi Novemba, 2023 majira ya sa 6:00 mchana katika kijiji cha Budekwa wilayani humo.
Mwendesha mashitaka huyo aliielezea mahakama kuwa mshitakiwa alimbaka muhanga ambaye jina lake limeifadhiwa kwa kumlaghai kuwa atampa pesa na baada yakufanya kitendo hicho mshtakiwa alimpa muhanga kiasi cha pesa Sh 1000 kwa ahadi kuwa asije akamwambia dada yake na muhanga ambae alikuwa akiishi nae.
Kosa alilotenda ni kinyume kifungu cha130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya ya Maswa ambapo mshtakiwa alikamatwa na alipohojiwa katika kituo hicho kwa kuandikwa maelezo yake ya onyo alikana kutenda kosa hilo na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa mahakamani.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulileta mashahidi watano na kielelezo kimoja ili kuthibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo hilo na baada ya ushahidi huo kutolewa mshitakiwa naye alipewa nafasi ya kuwasilisha utetezi wake.
Mara baada ya utetezi huo Mahakama hiyo ilimtia hatia mshitakiwa huyo na mwendesha mashitaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshitakiwa ili iwe funzo kwake na kwa jamii .
" Makosa ya kubaka yanaongezeka katika jamii na yanaleta athari kubwa kwa muhanga kisakolojia, kijamii, kiuchumi na kiafya ukizingatia kuwa mshtakiwa ni kijana ambae ana uwezo wa kumchumbia binti au mwanamke yoyote ambae hayupo chini ya umri wa miaka 18.
Pia makosa kama haya ni ukatili wa kijinsia katika jamii na hatimae huweza kusababisha maradhi au kifo kwa muhanga
Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na anafamilia inamtegemea ndipo Mahakama ikamhukumu kutumikia kifungo hicho na kulipa fidia ya kiasi hicho cha fedha kwa muhanga wa tukio hilo.
Post a Comment