HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WANAOISHI KARIBU NA BONDE LA MTO RUFIJI WATAHADHARISHWA

 

Na Gustafu  Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka Wananchi walioweka makazi na kufanya shughuli za kilimo katika bonde la mto Rufiji kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya  maji  yanayoongezeka katika mto huo.

Kunenge ametoa kauli hiyo Machi 14 mwaka huu wakati akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari kuhusu maji yaliyojaa mto Rufiji ambayo yameleta madhara kwa baadhi ya makazi na hata mazao ya wakulima wa Wilayani Rufiji na Kibiti.

Amesema mto Rufiji umejaa maji kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni pamoja na maji  yaliyotoka katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu  Nyerere ambalo kwasasa limeanza kuzalisha megawati 235.

    Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na waandishi wa habari ofisini 

Kunenge amesema kutokana na mvua hizo bwawa la Mwalimu Nyerere lilijaa kwa kina cha mita za ujazo 183.85 na hivyo kufikia maamuzi ya kufungulia baadhi ya mageti ili kupunguza maji hayo ambapo hatahivyo kwasasa yamepungua na kufikia mita za ujazo 183.45.

Amesema kufunguliwa kwa mageti katika bwawa hilo kulisababisha maji kusambaa katika bonde la mto Rufiji na hivyo kuleta mafuriko ambayo yamesababisha kuwepo kwa athari kwa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mto huo.

Amesema kabla ya kufunguliwa kwa mageti hayo Serikali ilitoa taarifa kwa wananchi ambao wamepitiwa na bonde hilo kwa njia mbalimbali ikiwemo kutangaza katika Redio ya Rufiji FM,nyumba za ibada na hata kupitia wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.

Kunenge amesema athari mojawapo iliyopatikana ni kuharibiwa kwa mazao baada ya kufunikwa na maji mengi lakini hatahivyo wengine walifanikiwa kuokoa mazao yao kwakuwa waliwai kuondoa mara baada ya kupewa taarifa juu ya kufunguliwa kwa maji hayo .

    Baadhi ya Wananchi waliopo Wilayani Rufiji katika Mkoa wa Pwani wakihama katika makazi yao kutokana na mafuriko yaliyotokea mto Rufiji na kuathiri mashamba na makazi yao

"Baada ya maji kujaa katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ililazimika baadhi ya mageti kufunguliwa ili kupunguza maji hayo lakini kabla ya kufungua wananchi wote walipewa taarifa na wengine kuondoka na hata kuokoa mazao yao ,"amesema Kunenge.

Amesema kufunguliwa kwa mageti hayo kulisababisha maji kusambaa katika mashamba na bonde la mto Rufiji kujaa  na kuleta changamoto kwa wakulima ambao mazao yao yalizingirwa na maji na kuharibiwa ikiwemo Mahindi, Mpunga, Maboga na mazao mengine.

Kunenge amesema kuwa tayari vyombo vya uokoaji vimefanyakazi na sasa hali inaendelea vizuri na kusema tahadhari lazima ichukuliwe kwakuwa mvua kubwa zinaendelea kunyesha.

"Tunaendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuwa waondoke katika maeneo hayo ili kuepusha vifo kwakuwa mvua nyingi zinaendelea kunyesha na hivyo kufanya mto Rufiji kuendelea kujaa maji,"amesema Kunenge.

Hatahivyo Kunenge amesema kuwa kamati ya maafa inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ili kuweza kujua athari iliyopatikana na hivyo  kuitolea taarifa kwa wananchi.


No comments