HEADER AD

HEADER AD

MEYA MANISPAA YA KIBAHA AFUNGA MACHIMBO YA MCHANGA BWAWA LA CHUMVI

 


>> Asema yatafunguliwa hadi utaratibu wa kisheria utakapofuatwa

>> Asema kuna utata ukusanyaji wa mapato

Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amegeuka kuwa mbogo na hatimaye kuyafunga machimbo ya mchanga ya bwawa la chumvi yaliyopo Kata ya Visiga hadi hapo utaratibu wa kisheria utakapokamilika.

Dr.Nicas amefunga machimbo hayo Oktoba 12/2026 wakati alipotembelea eneo hilo na kuona mazingira yameharibiwa kwa kuchimba mchanga wakati Manispaa haijatoa kibali cha uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwa katika machimbo ya mchanga ya bwawa la Chumvi Kata ya Visiga Oktoba 12/2026.

Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo la machimbo hayo amesema kuwa kuna utata juu ya ukusanyaji wa mapato huku akisema Manispaa ya Kibaha inapoteza mapato mengi kwakuwa utaratibu wake haueleweki.

Dr.Nicas amesema inafikirisha kuona machimbo hayo yapo Manispaa ya Kibaha halafu leseni inatoka Kibaha Vijijini lakini kwenye ukusanyaji mapato wanagawa kati ya Halmashauri ya Kibaha Vijijini na Manispaa ya Kibaha jambo ambalo ameona halijakaa sawa.

"Tumekagua machimbo haya lakini nimelazimika kuyafunga kwakuwa Manispaa ya Kibaha haijatoa leseni wala kibali chochote cha uchimbaji, kwahiyo yule ambaye anaona eneo hilo ni lake afike ofisini kwa ajili ya kupata utaratibu mzuri wa uchimbaji,"amesema Nicas

Dr.Nicas amesema kuwa sababu za kufunga machimbo hayo ni kutokana na uharibifu wa mazingira uliotokana na ukataji wa miti hovyo lakini pia Manispaa inapoteza mapato mengi kupitia machimbo hayo.

          Machimbo ya mchanga ya bwawa la Chumvi yaliyopo katika Kata ya Visiga Manispaa ya Kibaha.

Amesema kuwa kwasasa hataki kuona vifaa vyovyote vya uchimbaji wala mtu yeyote kuingia katika eneo hilo huku akisema askari watakuwepo eneo hilo wakilinda hadi hapo utaratibu wa kisheria utakapotolewa.

Dr.Nicas amemuagiza Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha Byson Mpogoza kuhakikisha anawaandikia barua wahusika wa eneo hilo juu ya kusitisha uchimbaji wa madini ya mchanga katika eneo hilo hadi hapo leseni itakapotolewa na Manispaa.

Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha Byson Mpogoza amesema kuwa kinachotekelezwa ni maelekezo ya Meya wa Manispaa ya Kibaha ya kuhakikisha machimbo hayo yanafungwa hadi hapo leseni au kibali kitakapotolewa na Manispaa.

Mpogoza amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 uchimbaji wa madini bila leseni na kibali ni uchafuzi wa mazingira kwakuwa wamekata miti hovyo.

         Baadhi ya vifaa vya kuchimbia mchanga katika machimbo ya bwawa la chumvi Kata ya Visiga vikiwa vimesimama kufanyakazi kwa amri ya Meya wa Manispaa Dr.Mawazo Nicas.

Nae Moses Mushi dereva wa lori la kubeba mchanga amesema kuwa ameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kufungwa kwa machimbo hayo ambapo ameiomba serikali inapotoa vibali ya kuchimba mchanga basi ni vyema wakajiridhisha kwanza kabla ya kutoa vibali hicho.

Amesema yeye kama mbeba mchanga hana kosa kwakuwa anapokuja katika machimbo hayo anazingatia kulipa ushuru wa tripu moja Sh.20,000 kwahiyo kama ni kosa basi lipo kwa Serikali yenyewe.
          Baadhi ya wachimbaji wadogo wa mchanga katika machimbo ya bwawa la Chumvi lililopo Kata ya Visiga Manispaa ya Kibaha wakitafakari jambo baada ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas kuyafunga machimbo hayo Oktoba 12 /2026.


No comments