HEADER AD

HEADER AD

RAZARO BIYA ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI CCM KATA YA TANGINI


 Na Gustaphu Haule, Pwani


WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tangini Wilaya ya Kibaha Mjini wamemchagua Lazaro Biya kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata  hiyo kwa kura 93.

Biya amechaguliwa kufuatia uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi hiyo uliofanyika Oktoba 1,2026 katika ofisi za CCM Kata ya Tangini ambapo hatahivyo ataongoza Kata hiyo hadi mwaka 2027 wakati uchaguzi wa ndani ya chama utakapofanyika tena.

     Mwenyekiti wa CCM Kata ya, Tangini Lazaro Biya akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti katika uchaguzi uliofanyika  Oktoba 1,2026.

Katika uchaguzi huo Biya aligombea akiwa na wapinzani wenzake wawili akiwemo aliyekuwa diwani wa Kata hiyo katika kipindi cha mwaka 2020/2025 Mfaume Kabuga(Kalanguti) pamoja naJenifa Mbawala kutoka CWT Kibaha.

Wajumbe wa uchaguzi huo walikuwa 131 lakini Biya aliibuka kidedea kwa kupata kura 93 huku Mfaume Kabuga akipata kura 37 na Jenifa Mbawala akipata kura 01.

Msimamizi wa uchaguzi huo Frank Msimbe ambaye ni diwani wa Kata ya Msangani  amewapongeza wajumbe hao kwa kufanya uchaguzi kwa amani,utulivu na umakini kwakuwa hakuna kura iliyoharibika.
        Msimamizi wa uchaguzi wa CCM Kata ya Tangini Frank Msimbe ambaye ni diwani wa Kata ya Tangini akitangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 01,2026.

Msimbe amesema kuwa kizuri zaidi wagombea wote wameridhika na matokeo hayo kwakuwa uchaguzi ulikuwa huru kwahiyo kwa mamlaka aliyonayo anamtangaza Lazaro Biya kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini.

"Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa namtangaza Lazaro Biya kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini kwa kipindi hiki  kwakuwa yeye ndiye aliyeongoza kwa kupata kura nyingi zaidi ya wagombea wenzake,"amesema Msimbe.

Nae Mfaume Kabuga ambaye kura zake hazikutosha katika uchaguzi huo amesema yeye ameridhishwa na matokeo hayo kwakuwa uongozi nikupokezana na kwamba atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa mwenyekiti aliyeshinda.

Katibu wa CCM Kata ya Tangini Sophia Mtase amesema anawashukuru wajumbe kwa kufanya uchaguzi kwa utulivu kama ambavyo awali walitamani uchaguzi huo huwe huru na haki na kwamba aliyeshinda kashinda.

       Katibu wa CCM Kata ya Tangini  Sophia Mtase akizungumza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 01,2026.

Mtase amesema kura ni namba na mwenyekiti aliyeshinda anatosha na kwakuwa mwenyekiti ni mtu wa kazi ameahidi kumpa ushirikiano wakutosha kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama.

Aidha,Mtase amempongeza  diwani wa Kata ya Tangini aliyemaliza muda wake Mfaume Kabuga kwa kujitokeza kugombea kwakuwa leo ameshindwa lakini siku nyingine atashinda.

Mwenyekiti aliyeshinda katika uchaguzi huo Lazaro Biya amewashukuru wajumbe kwa kumchagua kuwa mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini.

       Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Tangini wakiwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 1,2026.

Biya, amesema yeye ni mwenyekiti wa wote na atafanyakazi kwa maslahi ya chama na atakuwa mwenyekiti wa kila mwanachama wa CCM Kata ya Tangini.

Hata hivyo, Biya ameomba ushirikiano kutoka kwa wanachama hao kwasababu maamuzi yote ya chama yanatokana na wanachama na sio maamuzi yake pekee.

No comments