HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI KUWEKA SHERIA KALI KUMLINDA MTOTO

Na Andrew Chale, Dar es Salaam

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Dkt. Pindi Chana amesema Serikali inaenda kuweka sheria kali katika kuhakikisha inamlinda Mtoto hapa nchini ambapo jopo la Mawaziri wa Wizara zaidi ya nne watakutana katika kamati maalum.

Dkt Pindi Chana amesema jopo hilo litaundwa na Kamati ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Tamisemi, Maendeleo ya Jamii na wazara yake ya Katiba ili kuangalia chanzo ni nini kinachosababisha ukatili kwa watoto nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati wa kongamano la kujadili ulinzi wa mtoto  kuwa kamati lililoandaliwa kwa ushirikiano na mtandao wa kupinga utumkishwaji wa Watoto na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Juni 5,2024 Jijini Dar es Salaam ambalo pia limewakutanisha wadau mbalimbali wa taasisi za ndani na nje za masuala ya watoto.
Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Pindi Chana akizungumza

Amesema jopo hilo litaangalia chanzo cha ukatili ni nini kisha wataweka mikakati ili kiudhibiti unyanyasaji huo.

"Tumekubaliana tukutane tuweke mikakati ya kuangalia vyanzo vya ukatili kwa watoto, tutashirikiana na familia, shule, taasisi za dini ili tuweze kudhibiti ukatili.

Amesema wakati umefika wa kuweka mikakati kuhakikisha mtoto anapata haki zake ikiwemo ya elimu, matibabu na kulindwa dhidi ya utumikishwaji na shughuli nyingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UN Global Compact Chapa ya Tanzania, Marsha Yambi, amesema watoto milioni 200 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali duniani ambapo kati yao milioni 73 wako chini ya miaka 10.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, amesema kilimo kinaongoza kwa kuajiri watoto wengi hasa katika mashamba ya chai, tumbaku, miwa, mwani, karafuu na shughuli za uvuvi.

"Sekta binafsi inaonekana inachangia kuajiri watoto wadogo kwenye mashamba, tuhakikishe watoto hawawi katika ajira na tupate faida kwa haki na siyo kwa kupitia watoto," amesema Yambi.

Mratibu wa Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa Watoto nchini, Scholastica Pembe, amesema kongamano hilo linalenga kujadili sera na sheria zinazomlinda mtoto na kutolea mfano Sheria ya Ndoa ambayo inaruhusu mtoto aolewe chini ya miaka 18.

Amesema sheria ya kazi inaruhusu mtoto aanze kufanya kazi kuanzia miaka 14 na kuendelea lakini afanyishwe kazi ambazo si hatarishi na apate muda wa kucheza.

"Unaweza kujiuliza mtoto ambaye pia ni mama anapata wapi muda wa kucheza, muda wa kupumzika na asifanye kazi hatarishi ambazo ni pamoja na kuingia jikoni. Kwahiyo bado tunalo jukumu la kuangalia sera na sheria zetu zimekaaje ili kumlinda mtoto," amesema Pembe.





No comments