SHAIRI : KIFO, KWA HUO MVUTO WAKE !
HIYO nguvu naogopa, kwa huo mvuto wake
Tena haina kukopa, kwa yale makeke yake,
Gharama wengi walipa, ili tu wafike,
Kifo!
Ugua kivyako vyako, kaa huko uteseke,
Watakuja ndugu zako, wachache wawajibike,
Wabebe gharama zako, ili usiathirike
Kifo!
Wapate habari zako, kwamba pesa zichangike,
Ili wewe tiba yako, kwa uzuri ifanyike,
Hapo huwaoni kwako, ufe tukuzike,
Kifo!
Wajue habari zako, pumzi iadimike,
Umepigwa gonjwa lako, umetawanya mateke,
Watafute huko kwako, msibani wafike
Kifo!
Kanga mpya wazijua, msibani zivalike,
Vitenge unavijua, wenyewe wajifunike,
Pafyumu za kufukua, na zipulizike Kifo!
Rambirambi hapo kwako, ni nyingi zimiminike,
Mapochopocho yaliko, yaletwe tena yalike,
Sifa kwa msiba wako, bendi itumike
Kifo!
Wale msiokutana, pamoja mjumuike,
Hata mliokosana, kicheko kije mcheke,
Huyu ana nguvu sana, ujumbe ufike Kifo!
Sijui haya mapenzi, kwa kifo yafahamike?
Kwamba tuzidi yaenzi, kuyafanya tusichoke?
Kifo tuimbe utenzi, je tusitoroke
Kifo!
Vile tunatamania, kwamba kifo kitukuke,,
Kwamba watu wenye nia, kuhani huko tufike,
Pia tungefurahia, mgonjwa saidike
Kifo!
Itupendeze wapendwa, kifo kisisubirike,
Mtu kiafya kashindwa, kujua hali tufike,
Ndivyo hivyo tunafundwa, tuwajibikeni
Kifo!
Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment