HEADER AD

HEADER AD

JAMII YA WAHADZABE WAPATA MRADI UFUGAJI WA NDEGE

Na Samwel Mwanga, Meatu

MRADI wa Ufugaji wa ndege wa nyumbani na wale wa porini kwa ajili ya kuboresha lishe kwa wanajamii wa kabila la Wahadzabe katika wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu unatakiwa kwenda sambamba na utunzaji wa Mazingira.
 
Ufugaji huo pia utachangia upatikanaji wa chakula  na kuongeza kipato kwa jamii ya kabila hilo.
 
Mkuu wa wilaya ya Meatu, Faudhia Ngatumbura akizindua mradi huo  Septemba 9 mwaka huu katika ukumbi wa TASAF ulioko katika halmashauri ya wilaya hiyo, amesema kuwa jamii ya kabila hilo ni miongoni mwa jamii chache za wawindaji wa wanyama pori na wakusanyaji wa matunda ambao bado wanadumisha mtindo wa maisha yao ya asili kwa kutegemea shughuli hizo.

      Mkuu wa wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Faudhia Ngatumbura akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa ndege kwa jamii ya kabila la Wahazabe katika ukumbi wa TASAF Halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema kuwa mradi huo umekuja kwa muda muafaka kwani ufugaji wa ndege unaweza kuwa chanzo cha chakula bora na chenye lishe kama vile mayai na nyama  pamoja na kipato kutokana na kuuza mazao ya ndege.
 
“Hongereni kwa kupata mradi huu ambao unakwenda kutupa suluhisho la kupata kitoweo kwa jamii yetu ya kabila la Wahazabe hivyo niwaombeni tuupokee huu mradi na pia tuutunze ili yale malengo tarajiwa ya kupata kitoweo katika familia yetu yaweze kutimia na tukifanya kwa pamoja tunakwenda kutatua tatizo la uhaba wa kitoweo kwa jamii yetu ya Kihazabe,”.
 
“Huu si mradi wa kwanza kwa jamii ya Wahazabe hii ni kuonyesha kuwa jamii na serikali inathamini uwepo wenu na uhifadhi wenu ndiyo maana mradi kama huu umeletwa kwenu na wadau wa Maendeleo ambao ni Asasi ya AFRIPEDO na kuona hawa wenzetu tukiwawezesha kuna jambo fulani wanaweza kulifanya hivyo niwaombe tukayatunze mazingira yetu tunapotekeleza mradi huu,”amesema.
 
Amesema kuwa jamii ya kabila hilo bado ina changamoto kubwa hivyo inahitaji kupatiwa msaada mkubwa sana hivyo amewaomba wadau wengine kuwasaidia ili wawe na makazi ya kudumu waache tabia ya kuhamahama kwani serikali nayo iko tayari kuwahakikishia wanakuwa na maeneo yao ya kudumu ya kuishi kwa kutunza mazingira.

      Mkuu wa wilaya ya Meatu,Faudhia Ngatumbura(wa tatu kutoka kushoto)akiwa katika picha ya pamoja na jamii wa kabila la Wahazabe.

“Jamii hii ina changamoto kama mlivyosema kwenye risala yenu na ukiangalia historia yenu mlianzia wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga  na mmekuwa mkisogea kila siku na kwenda  meneo ya pembezoni na mimi.

" Niwape moyo tusisogee sasa hivi, sisi wote ni Watanzania tuna utofauti ya ukabila lakini tunakutana mahali kuwa wote ni raia wa Tanzania na hili eneo lenu ni la asili yetu, sasa na ninyi muwe mstari wa mbele kuhakikisha eneo mliopo hamsogei tena hivyo mnawajibu wa kutunza mazingira na kulifanya kuwa eneo lenu la makazi ya kudumu,”amesema.
 
Revocatus Meney ambaye ni Mratibu wa Mradi huo kutoka Asasi ya kiraia ya  Afrinurture For Peoples’ Development (AFRIPEDO)amesema  kuwa serikali imetengeneza mazingira mazuri ya kisheria kwa wanajamii kunufaika na wanyamapori.

        Revocatus Meney ambaye ni Mratibu wa Mradi wa kufuga ndege kutoka Asasi ya kiraia ya  Afrinurture For Peoples’ Development (AFRIPEDO)akitoa mafunzo kwa Wahazabe (hawapo pichani)

" Jitihada hizi za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii kupitia TAWA iliandaa kanuni ya kuanzisha mashamba ya kufuga wanyamapori (Wildlife Conservation (Management of Wildlife Captive Facilities) Regulations of 2020)" amesema.
 
Amesema kutungwa kwa kanuni  hizo kunapanua wigo na kutoa ruhusa kwa kufuga na kunufaika na wanyamapori jambo ambalo wao wameliona ma kuanzisha mradi huo kwa jamii ya kabila hilo kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa kitoweo.
 
       Sehemu ya jamii ya Kabila la Wahazabe katika wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu waliohudhuria mafunzo ya ufugaji wa ndege.

“Ufugaji ndege wa nyumbani na wale wa porini ulibuniwa na kupewa kipaumbele na Asasi yetu AFRIPEDO kama mkakati jadidi wa kuweza kuwapatia nyama ambayo ina protein na kuimarisha usalama wa chakula kwa jamii hii ya Wahazabe.
 
“Kutokana na mwongozo uwekezaji ya mkoa wa Simiyu ile  sura ya 4.1 inahimiza uwekezaji katika tasnia ya Maliasili na Utaliii kwa kuanzisha bustani na ranchi za kufuga wanyamapori hasa kwa wilaya Meatu hili kwa Asasi yetu tumelitekeleza kwa vitendo kupitia mradi huu,”amesema.
 
Pia amesema kuwa  mradi utakuwa shamba darasa kwa wanajamii wengine kujifunza na pia kupunguza vitendo vya ujangili wa wanyamapori kwa kuwezesha jamii ya Kihazabe kupata nyamapori kwa njia halali.

      Sehemu ya jamii ya Kabila la Wahazabe katika wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu waliohudhuria mafunzo ya ufugaji wa ndege.

Amesema kuwa eneo la utekelezaji wa mradi huu ni kijiji cha Makao na Kijiji cha Sungu na baadhi ya ndege wa nyumbani watakaofugwa ni pamoja na Kuku wa kienyeji, Bata wa kufugwa, Bata mzinga, Bata Maladi, Bata Pekini na Njiwa na kwa ndege  ndege wa porini  wataofugwa ni aina ya Kanga, Mbuni,Tandawala wakubwa, Bata bukini, Taji (Korongo – Taji)  na Bata Domokifundo.
 
Jape Jape mkazi wa Kijiji cha Sungu amesema kuwa kuwepo kwa mradi huo unakwenda kuondoa suluhisho la uwindaji haramu wa wanyama kwani walikuwa wakiingia porini na kuwinda wanyama kwa ajili ya kitoweo sasa watapata kitoweo kwa kufuga hivyo silaha walizokuwa wakizutumia kwa ajili ya uwindaji wa wanyama wataziweka chini.
 
“Huu mradi sasa utatufanya tupate kitoweo chetu kwa njia halali kuliko ile ya zamani ambapo tulikuwa tukiingia porini na kuanza kuwinda wanyama kwa kutumia silaha zetu za jadi kupitia mradi huu sasa tutafuga wenyewe na zile siraha tulizotumia kuwindia wanyama wa porini tutahakikisha tunaziweka chini,”amesema.
 
Naye Martha Shimba mkazi wa kijiji cha Sungu anasema kuwa hata wakinamama walikuwa wakitumia muda mrefu sana kwenda nao porini kutafuta kitoweo na sasa wameupokea kwa vizuri mradi huo wa ufugaji kwani kwa sasa afya za watoto wao zitaboreka kwa kupata virutubisho mbalimbali vitakavyotokana na mazao ya ndege kama vile mayai.
 
Shirika la Umoja wa Mataifa ( UNDP ) kupitia Mfuko wa Dunia wa Usimamizi wa Mazingira ( GEF) wameipatia asasi ya  AFRIPEDO  ruzuku kiasi cha dola za kimarekani 84,000 ambazo zitagawanywa kwa awamu tatu za utekezaji wa mradi huu.
 



No comments