WANAWAKE 55 TARIME WAJITOKEZA KUWANIA UDIWANI VITI MAALUM , 24 WAUSAKA UDIWANI KATA
>>Katibu UWT Nyasatu Manumbu asema ujasiri wa Rais Samia katika uongozi umewahamasisha wanawake
Na Dinna Maningo , Tarime
IMEELEZWA kuwa Ujasiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi( CCM) Taifa, katika uongozi umewaibua wanawake wa umoja wa wanawake wa Tanzania (UWT) wilayani Tarime, mkoani Mara kujitokeza kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania udiwani ngazi ya Kata na Viti maalum.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisi ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania ( UWT) wilaya ya Tarime, Katibu wa UWT wilaya hiyo, Nyasatu Manumbu amesema kuwa ujasiri wa Rais Samia katika uongozi na utekelezaji wa miradi umekuwa kivutio kwa wanawake.
Amesema jumla ya wanachama wa umoja wa wanawake wilayani Tarime, wapatao 55 katika Jimbo la Tarime mjini na vijijini wamechukua na kurejesha fomu wakitiania udiwani viti maalum.
" Naupongeza uongozi wa Rais Samia kwa mambo makubwa aliyoyafanya, ametekeleza miradi mingi . Amekuwa mwanamke jasiri katika uongozi wake ,hakuwa muoga licha ya kukuta miradi mikubwa na ya gharama ameweza kuikamilisha.
" Uhalisia huo umepelekea wanawake kuhamasika kujitokeza kuchukua fomu kuomba nafasi ya udiwani wa kata na viti maalum " amesema Nyasatu.
Katibu huyo wa UWT amesema kwamba katika nafasi ya udiwani wa Kata, jumla ya wanawake 24 wamejitokeza kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea udiwani ngazi ya Kata katika majimbo hayo mawili.
Amesema kati ya wanawake waliochukua fomu za udiwani ngazi ya Kata katika jimbo la Tarime vijijini ni wanawake 17 na Jimbo la Tarime mjini ni wanawake 7 na wote walichukua na kurejesha fomu.
" Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu limekamilika , tunasubiri tuanze vikao vya mchujo . Hatujapata changamoto yoyote ,wanachama wamejitokeza kwa wingi wamechukua fomu na wote wamerejesha" amesema Nyasatu.
Amewapongeza wanawake wa Tarime kwa kujitokeza kutiania huku akisema kwamba uongozi hupangwa na Mungu na kwamba kazi ya wanachama wao ni kuthibitisha.
Post a Comment