GACHAGUA AMUOMBA RAIS RUTO MSAMAHA
NAIBU RAIS Rigathi Gachagua Jumapili amemsihi Rais William Ruto kimsamehe huku akiapa kujitetea vikali kutokana na mashtaka dhidi yake yaliyoko kwenye hoja ya kumtimua ofisini.
Gachagua ameomba msamaha, jumapili Oktoba ,6, 2024 ambapo kesho atafika katika Bunge la Kenya kujadiliwa.
“Tumekumbwa na changamoto tangu tulipoingia ofisini miaka miwili iliyopita. Na katika harakati zetu kufanya kazi, huenda kwa njia moja ama nyingine, tulimkosea mtu.
" Naomba kumwambia ndugu yangu Rais William Ruto kwamba ikiwa katika kufanya kazi nilikukosea, naomba unisamehe,” Gachagua amesema mbele ya waumini katika ukumbi wa maombi ya kitaifa katika makazi rasmi ya Naibu Rais, mtaani Karen, Nairobi.
“Ikiwa mke wangu (Dorcas Rigathi) katika mpango wake wa kusaidia watoto wa kiume, na mipango mingine nchini, amekukosea, msamehe.”
Gachagua pia ameomba msamaha kutoka kwa wabunge 291 na kati yao wametia saini hoja ya kumbandua.
“Kwa wabunge wetu, ikiwa wakati wa shughuli zetu za kikazi, semi au vitendo vyetu vimewakera naomba mnisamehe,” amesema huku wabunge waliokuwepo wakisikiza kwa makini.
Naibu Rais ameomba msamaha kutoka kwa viongozi wa upinzani.
Gachagua amesema: “Ikiwa ndugu zetu ambao hawakuunga mkono rais na mimi jinsi eneo langu na Rift Valley ilimuunga na mkaona tulikosea kwa kuwatunuku watu wetu hilo, labda kwa kauli zilizowakera, tafadhali mnisamehe.”
Idadi kubwa ya wabunge wa chama ODM chake Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga wameunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutusi.
Hata hivyo, wabunge wa chama cha Wiper chake Kalonzo Musyoka wamepinga hoja wakidai “haina manufaa yoyote kwa Wakenya wakati huu.”
Gachagua pia aliwageukia Wakenya kwa ujumla na kuomba msamaha kutoka kwao.
“Ikiwa kuna chochote ambacho tulifanya au kusema na kuwakera au kuwachukiza, tafadhali mnisamehe,” ameomba kwa unyenyekevu.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wanaounga mkono hoja hiyo wamesema kuwa Naibu Rais amejitokeza kuomba msamaha akiwa kaishachelewa.
Mbunge mmoja kutoka eneo la MLIMA Kenya ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema “Ni hatua ya busara kwa Naibu Rais kuomba msamaha kwani hiyo inaonyesha kuwa kama mwanadamu anafahamu kuwa huenda alikosea.
" Lakini angeomba msamaha huo kabla ya hoja kuwasilishwa mbele yetu na nakala zake kuzisambaza wa Wakenya.
Ameongeza kuwa kulingana na Mbunge huyo ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) endapo Rais Ruto ataingilia kati na kushawishi kuangushwa kwa hoja hiyo, atakuwa amewateka hatarini wabunge 291 walioitia sahihi.
“Gachagua ambaye ninamjua bila shaka atawalenga kutuadhibu kwa zozote zile, haswa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Alianza kuchochea raia dhidi yetu hata kabla ya kuandaliwa kwa hoja hiyo. Akiponea hii, ataendelea kutumaliza kisiasa,” ameeleza.
Aidha, inasemekana kuwa endapo Rais Ruto atamsamehe Gachagua, itakuwa vigumu kwake, kwa mfano, kufanya kazi na vitengo vya kiusalama kama vile Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) ikizingatiwa kuwa mnamo Juni, 25, mwaka huu alishinikiza kujiuzulu kwa Mkurugenzi wake Mkuu Noordin Haji.
Hata hivyo, viongozi wa kidini, wakiongozwa na Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit, wamewataka Rais Ruto na Gachagua waridhiane.
Kesho (Jumatatu) wabunge watapata fursa ya kuijadili hoja hiyo kwa kina kuanza saa tatu asubuhi hadi majira ya usku. Mutuse atafafanua mashtaka yote 11, ambapo aliwasilisha mashahidi na ithabati nyinginezo kuonyesha kuwa yana mashiko.
Kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa moja usiku, itakuwa ni zamu ya Gachagua kujitetea kutokana na mashtaka hayo 11.
Baada ya hapo wataipigia kura kuipitisha au kuiangusha.
Endapo itapitishwa, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula atahitajika kuiwasilisha katika Seneti baada ya siku mbili.
Chanzo : Taifa Leo
Post a Comment