HEADER AD

HEADER AD

UCHAGUZI CCM TAWI LA MRITO WAVURUGIKA, SANDUKU LENYE KURA ZILIZOPIGWA LATUPWA


>>Wapiga kura wasema mtu mmoja alikuwa anarudia kupiga kura zaidi ya mara moja.

>>Ulinzi kituo cha kupigia kura haukuwepo

>>Diwani aliyekuwa msimamizi wa Uchaguzi lawamani kwa kustisha uchaguzi saa nane

>>Naye ajitetea asema tatizo ni utaratibu haukufuatwa, Uchaguzi warudiwa leo.


Na Dinna Maningo, Tarime 

ZOEZI la upigaji kura za maoni Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Murito, Kata ya Kemambo- Nyamongo, wilayani Tarime, kwa ajili ya kumpigia kura mtiania wa kugombea nafasi ya uenyekiti wa Kijiji cha Mrito katika uchaguzi wa serikali za mitaa umeingia dosari baada ya kutokuwepo kwa usimamizi mzuri katika zoezi la upigaji kura huku zoezi likichelewa kuanza na kustishwa kabla ya muda.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni, watiania nafasi ya uenyekiti wa kijiji cha Murito ni Yakobo Ryoba Irondo mkazi wa Kitongoji cha Nyambeho anayetetea nafasi yake ya uenyekiti, Manyanki Bhoke Jokihinda mkazi wa Kitongoji cha Nyambeho na Joseph Manga Gibao wa Kitongoji cha Keghati ambapo zoezi la upigaji kura lilifanyika katika shule ya Sekondari Mrito.

Habari zinasema kwamba zoezi la wananchama kupiga kura lilianza Kati ya saa tano na saa sita mchana na kustishwa saa nane mchana badala ya saa kumi jioni jambo ambalo lilipelekea baadhi waliokuwa kwenye foleni kushindwa kupiga kura.

Inasemekana kwamba zoezi la upigaji kura halikufuata taratibu kwani hakukuwa na orodha ya majina kuonesha ni watu gani wanaostahili kupiga kura ambapo inadaiwa kuwa wapiga kura walipaswa kupiga kura kwa kuonesha vitambulisho vya kielektoniki au namba za vitambulisho kwa wale ambao hawajapata vitambulisho vya kielektoniki ama kadi ya mwanachama.

Habari zinasema kwamba kwakuwa hakukuwa na orodha ya majina ya wapiga kura au namba za kadi ya kielektoniki ilipelekea kila mtu kupiga kura hadi wasiowanachama wakiwemo wa kutoka  Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Inasemekana kuwa hakukuwa na usiri wa upigaji kura kwani wapiga kura walipiga kura hadharani nje ya majengo ya shule ya Sekondari Murito. Badala ya mmoja mmoja kuingia ndani ya chumba kupigia kura kwa usiri.

Imebainika kuwa kilichochangia zoezi la upigaji kura kuvurugika ni baada ya Vitongoji vyote 11 kupiga kura katika kituo kimoja shuleni hapo hali iliyosababisha kuwepo msongamano mkubwa wa watu uliopelekea mtu mmoja kupiga kura zaidi ya mara moja.

Kijiji cha Murito kina Vitongoji 11 ambavyo ni Kitongoji cha Mabhere, Keghati, Kumchongome, Kisankwe, , Nyambeho, Milimisi, Nyangebho, Rorya, Murogho, Kemoka na Nyabihero jambo ambalo lilisababisha wingi wa watu wengi kwenye kituo cha kupigia kura.

Habari zinasema kuwa ulinzi na usalama katika kituo hicho hakuwepo ndio sababu ya uchaguzi kuvurugika na mtiania mmoja nafasi ya uenyekiti kuchukua sanduku moja lenye kura zilizopigwa na kulitupa nje kwa madai kuwa upigaji wa kura haukuwa wa haki.

Imeelezwa kuwa Chama cha CCM kilipaswa kuweka vijana wa chama kuimarisha ulinzi kuhakikisha zoezi la uchaguzi linakwenda vizuri.

Habari zinasema kwamba licha ya zoezi la uchaguzi kuvurugika, aliyeonekana kuongoza kwa kura nyingi alikuwa ni mtiania Joseph Manga anayetoa kitongoji cha Nyambeho. 

Hata hivyo Msimamizi wa Uchaguzi Tawi la Murito ambaye ni Diwani wa Kata ya Kemambo Rashid Bogomba amelaumiwa kuwa amechangia zoezi la uchaguzi kwenda vibaya kwa kushindwa kusimamia vema zoezi la upigaji kura ikiwemo watu kupiga kura bila kufuata utaratibu wa kutumia majina ya wanachama halali waliosajiliwa kwenye mfumo wa kiektroniki.

Mwandishi wa DIMA ONLINE amefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wanachama ambao wameomba majina yao yasiandikwe na pia amezungumza na wagombea na viongozi wa Chama kufahamu nini sababu ya kuvurugika  uchaguzi huo, nao walikuwa na haya ya kusema;

Mwanachama mmoja mkazi wa Kitongoji cha Murito amesema " Uchaguzi umevurugika baada ya kukosa usimamizi mzuri wa ulinzi, kuna mgombea mmoja wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea akaona kama anaelekea kushindwa akachukua box lenye kura zilizopigwa akalitupa nje kura zikamwagika  na hivyo zoezi likavurugika na kustishwa ." amesema.

Mwanachama mwingine amesema " Diwani aliyekuwa msimamizi ndio tatizo hakusimamia vizuri uchaguzi, kura zilianza kupigwa saa sita mchana ilipofika saa nane akastisha zoezi kwamba watu wanajirudiarudia kupiga kura wakapeleka mabox ndani kuhesabu kura.

"Hali hiyo ilisababisha ambao walikuwa hawajapiga kura waliokuwa kwenye foleni kunyimwa haki yao ya kupiga kura kwakuwa zoezi lilistishwa mapema saa nane mchana badala ya muda halali wa saa kumi jioni. Kiukweli chama chetu hakikuwa kimejipanga vizuri kwenye zoezi la uchaguzi mambo yalikuwa ni shagalabagala tu hakuna cha utaratibu.

Mwanachama mwingine amesema " Tumepiga kura eneo la wazi hakukuwa na usiri, mtu unapiga kura nje watu wanakuona hakuna hata kakificho kakupigia kura. Kwanini mtu asingekuwa anaingia ndani kupiga kura wakati kuna madarasa na kituo kilikuwa shuleni na badala yake tunapigia kura nje hadharani ! ".

DIMA ONLINE imefanikiwa kuzungumza na watiania leo majira ya saa moja asubuhi kufahamu sababu za uchaguzi kuvurugika ambao wameeleza kuwa ulichangiwa na utaratibu na usimamizi mbaya.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Murito anayetetea nafasi hiyo Yakobo Ryoba Irondo alipoulizwa sababu za uchaguzi kuvurugika amesema " uchaguzi ulivurugika unarudiwa leo nitakupa maelezo jioni tukishamaliza uchaguzi" amesema Yakobo.

Mtiania Joseph Manga Gibao amesema" Watu walijitokeza kwa wingi kupiga kura. Kosa la kwanza zoezi lilianza saa tano likastishwa saa nane mchana watu wengine wakishindwa kupiga kura.

" Kosa lingine mtu alikuwa anapiga kura anarudia zaidi ya mara moja, mizengwe ilikuwa mingi hata hukujua kama ni uchaguzi wa Chama kimoja. Yaani ilionekana kama kuna mtiania mmoja alikuwa anabebwa unaona kabisa hawa watu wako kwa mgombea fulani na hivyo uchaguzi kuwa na dosari.

Anaongeza " Diwani alikosea kustisha zoezi la upigaji kura saa nane, akasema watu wanajirudiarudia kupiga kura. Ni kweli kuna baadhi walijirudia kupiga kura lakini kuna wengine walikuwa hawajapiga kura na walikuwa kwenye foleni.

" Tatizo lingine watu walikuwa wameandikishwa kwa mfumo wa kiektroniki lakini huo mfumo haukutumika kwenye upigaji kura ,tulitegemea kura zipigwe kwa kila kitongoji lakini wote walipigia kwenye kituo kimoja hali iliyosababisha mvurugiko kwakuwa watu walikuwa wengi kukawa na mwingiliano wa watu mara huyu anatafuta mtu wa kumwandikia.

" Mara unaona mtu anapiga kura mstari wa Kitongoji hiki akimaliza anaenda kujipanga mstari mwingine wa Kitongoji kingine anapiga kura. Mtiania mmoja akachukua box moja la kura zilizopigwa akalitupa likaanguka nje, kura zikamwagika watu wakaziokota wengine wakazichana ikabidi zoezi listishwe.

Ameongeza " Viongozi wa Chama wilaya akiwemo Katibu walifika wakatoa utaratibu kuwa uchaguzi urudiwe leo na kura zipigwe kule kule kwenye Vitongoji. Watu wametangaziwa kupitia  vipaza sauti kwahiyo naamini watu watajitokeza kupiga kura. Tunaomba zoezi lifuate taratibu na haki" amesema Joseph.

Mtiania Manyanki Bhoke Jokihinda aliyedaiwa kuchukua sanduku moja la kura zilizopigwa na kulitupa chini nje ya darasa na hivyo zoezi la kuhesabu kura kutoendelea kufanyika alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo amesema ;

" Kama nilitupa box la kura zikamwagika chini si wangeziokota wahesabu ? Kilichotokea uchaguzi haukufuata taratibu haki hazikutendeka, watu hawakuvaa sare za Chama yaani ulifanana na ule uchaguzi wa kawaida wa CCM na vyama vingi ambao wapiga kura hawavai sare, haukuwa wa kujitofautisha.

" Uchaguzi haukuonesha misingi ya kupiga kura, ilitakiwa mtu akifika kupiga kura kuwepo na orodha ya majina aseme jina lake kisha msimamizi aangalie amtiki alafu apige kura lakini hakukuwa na majina kila mtu aliyefika alipiga kura hata kama si mwanachama. Hakukuwa na utaratibu wa kuonesha kadi ya Chama hivyo uthibitisho wa uhalali wa wapiga kura haukuwepo.

Anaongeza kusema " Hata mimi mgombea mwenyewe sikupiga kura maana nilikuwa naangalia zoezi linavyokwenda . Mimi hata ningeshindwa sikatai maana lazima mshindi awepo lakini nilichokipinga ni utaratibu uliotumika kupiga kura wa kiholelaholea yaani mtu mmoja anapiga kura mara sita! Tukaona sio sahihi tukastisha zoezi.

" Diwani alichangia kuvurugika uchaguzi kwa kushindwa kusimamia vema zoezi la upigaji kura na kustisha uchaguzi kabla ya muda, na hakukuwa na idadi ya watu wangapi waliosajiliwa kuweza kupiga kura. 

" Wamesema uchaguzi utarudiwa leo ila mimi sijapewa taarifa wala kujua ni utaratibu gani utatumika je ni ule ule kama wa jana? nipo naangalia kinachoendelea" amesema.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mrito,  Tungucha Rich Machonchori alipoulizwa kueleza sababu ya uchaguzi kuvurugika na kwanini zoezi la kupiga kura likichelewa kuanza na kuwahi kustishwa amesema;

" Uchaguzi ulivurugika mtiania mmoja alitupa box lenye kura. Alafu sikufahamu unaweza kusema wewe ni Mwandishi kumbe si kweli maana hata kwenye mitandao huwa tunaona matapeli wakipiga simu. kwanza nina kazi ya kufanya hivyo njoo ofisini siwezi kuzungumza kwenye simu " amesema kisha akakata simu.

Msimamizi wa uchaguzi azungunza

Mwandishi wa chombo hiki cha Habari alimpigia simu msimamizi wa uchaguzi Tawi la Murito ambaye ni Diwani wa kata ya Kemambo Rashid Bogomba kufahamu sababu za uchaguzi kuvurugika.

Bogomba amesema" Utaratibu wa uchaguzi ndio ulioleta shida, zamani watu walikuwa wanapigia kura kwenye Vitongoji vyao, ilisaidia wanachama kupiga kura kwa urahisi na kwa muda sahihi. Huu uchaguzi wa sasa Vitongoji vyote 11 vimepiga kura kwenye kituo kimoja yaani mtu anatoka umbali wa km 4 kwenda kupiga kura.

" Hali hii imeleta shida wapiga kura wakawa wengi kukawa na miingiliano iliyopelekea watu kupiga kura kwa kujirudia. Nilistisha zoezi la upigaji kura baada ya kuonekana watu wale wale wanarudia kupiga kura na hao wagombea ndio walisema tustishe.

"Tukastisha tukaingia ndani kuhesabu kura wakati tunaendelea kuhesabu kura likiwa limebaki box mmoja mgombea Manyaki alichukua hilo box akalitupa nje . Na yeye ndiye alisema tustishe zoezi la upigaji kura kwakuwa watu wanajirudia yeye huyo huyo akalalamika tena kuwa zoezi limestishwa kabla ya muda uchaguzi urudiwe " amesema Rashid.

" Zoezi la upigaji kura lilichelewa kuanza kwasababu masanduku ya kupigia kura yalikuwa yanatoka wilayani yakachekewa kufika na hivyo zoezi kuchelewa kuanza. Na ilipoonekana watu wanajirudia kupiga kura ilibidi wino uletwe watu wakishapiga kura wachovye kwenye vidole ili wasijirudie.

" Lakini walikuwa wanaenda wanapaka mafuta wino unafutika wanarudi tena kupiga kura na malalamiko hayo waliyatoa wenyewe ndo wanafahamiana mimi siwafahamu wakazi wote wa Tawi la Murito ikabidi zoezi listishwe " amesema Rashid.

Rashid ameongeza kusema " Kuhusu watu kupiga kura bila orodha ya majina na kadi za kielektoniki ni kwasababu watu wengi hawajajiandikisha na hawana kadi za kielektoniki tungesema tufuate huo utaratibu watu wengi wasingeweza kupiga kura.

"Pia tungefuata utaratibu wa kusoma jina moja moja Vitongoji vingine visingweza kupiga kura ingekuwa kama kule kwenye Tawi la Kerende Vitongoji viwili ndio vilivyopiga kura kati ya Vitongoji kumi kwakuwa muda wa upigaji kura uliisha na Vitongoji vingi vikashindwa kupiga kura na wenyewe wanarudia uchaguzi leo.

" Ameongeza " Tulikubaliana kwakuwa watu wanajuana kwenye Vitongoji vyao kila kitongoji kiwe na foleni yake mtu apige kura na ambaye siyo mwanaccm kitongoji husika akifika kwenye foleni wamkatae lakini hawakufanya hivyo.

"Mimi siwajui ni msimamizi natokea kijiji cha mbali cha Kewanja isingekuwa rahisi kuwatambua wanaostahili kupiga kura,wao haohao wakasema zoezi listishwe watu wamemaliza kupiga kura wanachokifanya ni kujirudia ikabidi listishwe saa nane.

Uchaguzi huo unarudiwa leo ambapo zoezi la upigaji kura linafanyika kwenye Vitongoji na wanachama wanaendelea na upigaji zoezi la kura.

Kwa mujibu wa Tangazo la ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa iliyotolewa Agosti, 15, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, kampeni zitaanza Novemba, 20-26,2024 na uchaguzi wa kuwachagua Wenyeviti wa vijiji, mitaa, Vitongoji na wajumbe utafanyika Novemba, 27, 2024.


No comments