SERIKALI YAIPONGEZA KAMPUNI YA NDENENGO SENGUO KWA UBORA
Na Daniel Limbe, Chato
SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imeipongeza kampuni ya kizalendo ya M/S Ndenengo Senguo Company Limited, inayotekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi na salama kutoka Buzirayombo hadi Mkungo kutokana na ubora wa mradi na kuzingatia muda wa mkataba.
Upanuzi huo ni utekelezaji wa usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya hiyo chini ya Mradi wa miji 28 nchini.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura, ametoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambao ulianza kutekelezwa juni 28,2024 na ukitarajiwa kukamilika juni 27,2025 ambapo mpaka sasa umefikia aslimia 68 ya utekelezaji wake.
Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura akipokea maelekezo kutoka kwa Msimamizi wa mradi wa maji(Kulia) Baldwin Nzelan."Ninakupongeza sana msimamizi wa mradi huu,umeendelea kufanya kazi nzuri licha ya kuendelea kuidai serikali fedha, nikuombe uendelee na kazi hii kwa ufanisi ili ikamilike kabla ya wakati na nina uhakika fedha yako utakipwa yote" amesema Bura.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Chato(CHAWASA) Mhandisi Isaack Mgeni, amesema mradi huo una thamani ya kiasi cha shilingi milioni 974,186,850 na kwamba mkataba wa kukamilika kwake ni mwaka mmoja.
Hata hivyo,amemshukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kukubali kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo utakao wanufaisha wananchi na kuongeza uchumi wa familia,wilaya na taifa kwa ujumla.
"Jamii inapokosa huduma ya maji inasababisha kukosekana kwa utulivu wa familia, na wanaoteseka zaidi ni wanawake na watoto,hivyo mradi huu utakapo kamilika utasaidia wananchi kupata maji majumbani mwao na kuongeza uchumi na maendeleo"amesema Mhandisi Mgeni.
Mhandisi mgeni,amesema kazi kubwa ya uchimbaji mtaro na utandazaji wa bomba zenye urefu wa kimomita 21.5 umefanyika ikiwa ni pamoja na kubadili bomba lenye ukubwa wa milimita 110 na kuweka lenye ujazo wa milimita 160 kwa umbali wa km 9.72.
Msimamizi wa mradi huo, Baldwin Nzelan,ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiamini kampuni yake huku akiahidi kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.
Ametumia fursa hiyo kuiasa jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo katika utekelezaji wa mradi huo ambao ni muhimu kwa wananchi wa Buzirayombo na Mkungo wilayani hapa.
Post a Comment