HEADER AD

HEADER AD

MIRADI YA BILIONI 40 BUKOBA YAKABIDHIWA KWA WAKANDARASI

Na Alodia Dominick, Bukoba

MIRADI mikubwa iliyokuwa ni kilio cha wananchi wa Bukoba mkoani Kagera ambayo ni soko kuu, stend kuu ya mabasi, ujenzi wa kingo za mto Kanoni na upanuzi wa barabara imepata muarobaini na itaanza kujengwa.

Miradi hiyo itakayogharimu Tsh. Bilioni 40 imekabidhidhiwa kwa wakandarasi tayari kwa kuanza utekelezaji wake.

Jitihada  za mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini wakili  Stephen Byabato zimewezesha miradi hiyo ya maendeleo   iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kisiasa kuanza kutekelezwa.

Wakili  Byabato ameishukuru serikali kwa kuridhia kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Manispaa ya Bukoba .

        Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini (CCM) Wakili Stephen Byabato akizumgumza na wananchi wa jimbo lake.

Amesema viongozi wengi waliopita wamekuwa wakishindwa kutekeleza mahitaji hayo muhimu ya wananchi.

Ameeleza kuwa, katika ahadi za Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020 walihaidi kujenga soko la kisasa na stendi kuu.

"Wakati napambana kuhangaikia utekelezaji wa miradi hiyo baadhi ya watu walikuja kunizuia na kunieleza kuwa nikifuatilia hiyo miradi nitakosa ubunge, nikawajibu soko litajengwa na mimi sio wa kwanza kuwa mbunge hapa wala sitakuwa wa mwisho lazima miradi itekelezwe"anasema Byabato.

Amesema sasa yeye hafanyi tena siasa za maneno bali za vitendo na wanaodai kuwa hakushiriki katika miradi hiyo ya maendeleo  anawaombea kwa mwenyezi Mungu.

"Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji 15 ya awamu ya pili zinazotekeleza miradi ya TACTICS, lengo likiwa ni kupendezesha miji na kuongeza mapato ya ndani" amesema Byabato

Aidha, Wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza Miradi ya TACTICS Manispaa ya Bukoba yenye thamani ya shilingi bilioni 40 wamekabidhiwa maeneo ya kutekeleza miradi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

      Wakandarasi na Serikali wakiweka makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya Soko kuu, Stend ya mabasi, kingo za mto Kanoni na upanuzi wa barabara.

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema  wakandarasi wamekabidhiwa maeneo ya ujenzi wa Soko Jipya la Manispaa ya Bukoba, Stendi ya Mabasi Kyakailabwa, ujenzi wa kingo za Mto Kanoni zenye urefu wa kilometa 7.3 pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kilometa 10.75 ukiambatana na usimikaji wa taa za barabarani 423.

Amesema miradi hiyo imegawanywa katika makundi mawili ambapo Mkandarasi mzawa M/s Dimetoclasa Realhope Limited atajenga soko na Stendi ya Mabasi Kyakailabwa kwa gharama ya shilingi bilioni 18.9.

Ameongeza kuwa Mkandarasi wa kigeni M/s Shandon Luqiao Group Company Limited atajenga barabara kilometa 10.75, kingo za Mto Kanoni kilometa 7.3 na kuweka taa za barabarani 423 kwa gharama ya shilingi bilioni 21.3.

"Matarajio yangu ni kuona miradi hii inakamilishwa kwa wakati kulingana na mkataba ambapo mmepewa kipindi cha miezi 15 kuanzia Julai 15, 2025 hadi Oktoba 14, 2026" amesema Mwassa

Amesema Miradi hiyo inatarajia kuwa kichocheo cha ongezeko la uchumi wa Manispaa ya Bukoba na mkoa wa Kagera kwa ujumla kwa kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana lakini pia kuwa kivutio kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanailinda miradi hiyo na kuwapa ushirikiano wakandarasi kufanya kazi yao bila vikwazo vyovyote.

        Wananchi wa Bukoba mjini wakiwa kwenye mkutano.

No comments