HEADER AD

HEADER AD

MKURUGENZI MAUWASA ACHUKUA FOMU UBUNGE BUCHOSA

Samwel Mwanga, Sengerema

MKURUGENZI mtendaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mjini Maswa (MAUWASA), Mhandisi Nandi Mathias James, amejiunga rasmi katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Buchosa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mhandisi Nandi alichukua fomu hiyo leo Jumamosi, Juni 29, 2025 katika ofisi za CCM wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza ambapo alikabidhiwa na Katibu wa CCM wilaya hiyo, Rashid Semendu.

      Mkurugenzi  Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias James,(kulia) akikabidhiwa fomu ya kugombea ubunge jimbo la Buchosa wilaya ya Sengerema na  Katibu CCM wilaya hiyo,Rashid Semendu.

Akizungumza baada ya kukamilisha hatua hiyo, Mhandisi Nandi amesema kuwa uamuzi wake umetokana na nia ya dhati ya kulitumikia taifa na jamii ya Buchosa kwa kutumia taaluma na uzoefu wake katika sekta ya maji, usafi wa mazingira na usimamizi wa huduma za umma.

“Nimeamua kujitosa katika nafasi hii kwa moyo wa uzalendo. Nataka kuchangia kwa vitendo katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Buchosa, hasa katika nyanja za miundombinu, huduma za maji, afya na ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema.

Jimbo la Buchosa kwa sasa linawakilishwa na Mbunge Erick Shigongo (CCM), ambaye alichaguliwa mwaka 2020 na ni miongoni mwa wabunge ambao siku za nyuma alikuwa na umaarufu wake katika tasnia ya habari na burudani kabla ya kuingia siasa.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema,Rashid Semendu, aliwahimiza wanachama wote wanaojitokeza kuchukua fomu kuzingatia maadili ya chama, amani na mshikamano wakati wa mchakato wa ndani ya chama.

         Katibu wa CCM wilaya ya Sengerema, Rashid Semendu(kulia)akimpatia maelezo ya fomu ya kuwania ubunge,Mhandisi Mathias Nandi kabla ya kumkabidhi.

    Mkurugenzi Mtendaji MAUWASA,Mhandisi Nandi Mathias akisaini fomu mara kabla ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge jimbo la Buchosa wilaya ya Sengerema.

No comments