HEADER AD

HEADER AD

DED KIBAHA ATINGA SOKO LA MNARANI KUSIKILIZA KERO ZA WAFANYABIASHARA

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKURUGENZI wa Halmashauri ya  Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amefanya ziara ya kikazi katika Soko la Mnarani Loliondo Kata ya Tangini ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara hao.

Dkt.Shemwelekwa amefanya ziara hiyo Novemba 14/2025 ambapo pamoja na kusikiliza kero za wafanyabiashara hao lakini pia amewaomba kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu ili waweze kujipatia kipato halali kwa ajili ya kuimarisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

      Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Loliondo alipofanya ziara Novemba 14 /2025.

Amesema kuwa serikali imehakikisha mazingira ya nchi yako salama chini ya uongozi wa  Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo hakuna sababu ya wafanyabiashara kuwa na hofu ya kufanya shughuli zao katika soko hilo.

Aidha, Shemwelekwa ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa endapo Kuna wageni au watu wanaotiliwa mashaka ili ikiwezekana hatua za haraka zichukuliwe kwa ajili ya kulinda amani ya nchi.

        Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Mnarani Loliondo wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika mkutano wa pamoja uliofanyika Novemba 14/2025 sokoni hapo.

Amebainisha kuwa kuna watu wasiopenda kuona Tanzania ikiendelea kufurahia amani na ndio maana wamekuwa wakichochea vurugu na kwamba amewasisitiza vijana na wananchi kwa ujumla kulinda amani ambayo ni msingi wa maendeleo ya Taifa.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya Wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu Shemwelekwa amesema ni vizuri wakachangamkia fursa hiyo kwakuwa fedha hizo ni zao.

Amesema fedha hizo zipo ,hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuunda vikundi vya kuanzia watu watano na wawe na  Katiba inayowaongoza ili waweze kukopeshwa kwa ajili ya kuendeleza biashara zao .

Pia, amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwapa Afisa Maendeleo na Afisa Biashara watakaowasaidia katika usajili wa vikundi hivyo ambao watakuwa katika Soko hilo na kutoa huduma ya kuunda vikundi vya wafanyabiashara hao. 

Mwenyekiti wa Soko hilo Mohamed Mnembwe akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Soko hilo amemshukuru Mkurugenzi kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao. 

Mwenyekiti wa soko la Mnarani Loliondo Mohamed Mnembwe (kushoto) akiteta jambo la Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Rogers Shemwelekwa katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika Novemba 14/2025.

Mnembwe ameishukuru serikali kwa ujenzi wa soko jipya la kisasa ambalo linaendelea kujengwa wakisema kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara lakini ameomba kukarabati eneo la soko wanalolitumia hivi sasa ambalo Kuna sehemu zinahitajika bati 30.

"Mkurugenzi tunakushukuru sana kwa kuja kutatua changamoto zetu hapa sokoni ,sisi tuko pamoja na tunaendelea kukushukuru," wamesema baadhi ya wafanyabiashara kwa niaba ya wenzao.

Hata hivyo,ziara hiyo imetajwa kuwa chachu ya kuimarisha uhusiano kati ya Halmashauri na wafanyabiashara  pamoja na kuongeza hamasa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa ya Kibaha.

  Sehemu ya soko la Mnarani Loliondo katika eneo la bidhaa mchanganyiko kama linavyoonekana pichani.


No comments