HEADER AD

HEADER AD

RIKIZO YA UZAZI KUZINGATIA MUDA WA UANGALIZI KWA WATOTO NJITI


SERIKALI ya Tanzania, imesema likizo ya uzazi kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti (ambao hawajatimiza siku) inaanza pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalumu kadiri madaktari watakavyothibitisha.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango wakati wa kilele cha siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kitaifa jijini Arusha, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Alikuwa akijibu maombi ya viongozi wakuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi TUCTA.

"Iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi, likizo ya uzazi itaanza pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalumu kadiri madaktari watakavyothibitisha, vilevile mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 mchana kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha". Amefafanua.

Kuhusu kanuni ya kukokotoa mafao ya pensheni kwa wafanyakazi wakati wa kustafu, maarufu kama Kikokotoo, makamu huyo wa rais amesema serikali imepokea hoja ya wafanyakazi kutoridhishwa na kikokotoo na inaifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu.

Ameweka bayana kuwa baada ya kulipokea suala hilo litapelekwa kwa wataalamu wa takwimu bima (Actuarial Science) ili watoe ushauri kulingana na mahitaji ya wafanyakazi na hali ya uhimilivu wa mifuko ya pensheni.

Kwa utaratibu wa sasa mstaafu wa umri wa miaka 55 kwa hiari au miaka 60 kwa mujibu wa sheria analipwa asilimia 33 ya mafao kwa mkupuo mmoja na fedha zinazobakia analipwa pensheni ya kila mwezi kwa kipindi cha miaka 12 na miezi sita, kwa makadirio ya chini.

Chanzo : BBC

No comments