HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YAOKOA MILIONI 624 BAADA YA KUSHINDA MASHAURI 50 KATI YA 52

Na Alodia Babara, Bukoba 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera imesaidia kurejesha kiasi cha  Tsh. Milioni 624.6 baada ya kushinda mashauri 50 kati ya 52 yaliyofikishwa mahakama mbalimbali mkoani Kagera.

Naibu Mkuu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera Leonard Swai ametoa taarifa hiyo Mei 21 mwaka huu ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Kipindi cha kuanzia Julai ,2025  hadi sasa tumefanikiwa kufungua mashauri 61 mahakamani ambapo mashauri 52 yameamuliwa  kati ya hayo takukuru imeshinda mashauri 50 sawa na asilimia 97 ,imeshindwa mashauri mawili na mashauri 9 yanaendelea mahakamani. amesema Swai.

Amesema katika mashauri hayo 50 waliyoshinda wamefanikiwa kurejesha kiasi cha zaidi ya shilingi  milioni 624.6.

Hata hivyo amesema kipindi cha Januari  hadi Machi  2026 wamepokea taarifa 132  kati ya hizo 83  zilihusu rushwa na taarifa 49 hazikuhusu rushwa.

Amesema taarifa 83  zilizohusu  rushwa zilichunguzwa  na jumla ya majalada 12 yalifunguliwa kesi mahakamani na  chunguzi zingine zinaendelea.

Ameongeza kuwa TAKUKURU wilaya ya  Kyerwa imesaidia kurejesha fedha kiasi cha Tsh. Milioni 30 fedha zilizotolewa kwajili ya mkopo wa kikundi cha ufugaji nyuki cha wanawake wa Kata ya Katera  ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zinazotolewa kwa mkopo wa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema kikundi hicho kilipokea fedha kupitia akaunti ya kikundi namba 35910010751 iliyopo benki ya NMB February 18 mwaka huu baada ya kuonekana kutimiza masharti yote ya mkopo.

Amesema baada ya uchunguzi wa Takukuru  ilibaini kuwa kikundi hicho kimetumika kama kikundi kivuli  cha kupata mkopo husika wa milioni 30 baada ya kikundi hicho kivuli kuwekewa milioni 30  zilihamishiwa kwenye akaunti namba 01J2033984900 inayomilikiwa na Benjamin Barthazary ambaye alizitumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi.

Ameeleza kuwa, baada ya kubaini kasoro hizo Takukuru Kyerwa  ilielekeza fedha hizo zirejeshwe kwenye halmashauri ya Kyerwa ili zitumike kwenye  makundi yenye sifa na tayari zimesharejeshwa kwenye akaunti ya halmashauri.

Wakati huohuo, wamefanikiwa  kudhibiti ujenzi wa chini  ya kiwango  wa  msingi wa jengo la Zahanati  ya Kijiji cha Runzenze Kata Ntobeye Wilayani Ngara  inayojengwa kwa nguvu za wananchi na jumla ya shilingi milioni 9.5 zimekusanywa na  wananchi  wa kijiji hicho kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.

Anasema ufuatiliaji huo ulibaini  kuwa kiwango cha uwiano  katika  mchanganyiko wa zege ( concrete ratio ) katika jamvi la msingi  huo kuwa ni dhaifu kiasi cha kusababisha jamvi kuanza  kumomonyoka na nondo zilizosukwa kuonekana na kuanza kupata kutu hali inayoashiria ujenzi umefanyika chini ya kiwango.

TAKUKURU kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri, waliishauri serikali ya Kijiji kufanya marekebisho katika hatua hiyo ya ujenzi ili kuzuia madhara ambayo yangejitokeza kutokana na udhaibu wa msingi huo jambo ambalo limekwisha tekelezwa.


No comments