HEADER AD

HEADER AD

MEYA MANISPAA YA KIBAHA AMTUNUKU MKURUGENZI TUZO YA UBUNIFU MFUMO WA UFUNDISHAJI WANAFUNZI KUPITIA TEHAMA


Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amemtunuku tuzo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa kufuatia umahiri wake wa kubuni mfumo wa ufundishaji wanafunzi kupitia teknolojia ya Tehama inayojulikana kwa jina la darasa janja(Live Teaching).

Dkt.Nicas amekabidhi tuzo hiyo Julai 31,2026 kwa afisa utumishi wa Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela mara baada ya kuzindua darasa janja lenye mfumo wa teknolojia ya Tehama katika Shule ya Sekondari Bundikani iliyopo Kata ya Mailimoja Manispaa ya Kibaha.

     Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas ( kushoto) akikata utepe kuzindua mradi wa darasa janja katika Shule ya Sekondari Bundikani hafla iliyofanyika Julai 31,2026.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt.Nicas amempongeza Mkurugenzi huyo kwa kazi nzuri ya kubuni mfumo huo kwani    unakwenda kulisaidia Taifa kuondokana na adha ya upungufu  wa walimu hasa wale wa masomo ya Sayansi.

Amesema mfumo wa ufundishaji kupitia darasa janja ulibuniwa na Mkurugenzi huyo kipindi akiwa Shirika la Elimu Kibaha na ulianza kutumika katika Shule ya Sekondari Kibaha Boys na sasa umeanza katika Shule ya Sekondari Bundikani.

Amesema mfumo huo ndio wa kwanza kutumika Mkoa wa Pwani na Manispaa ya Kibaha ndio ulipoanzia na kwamba unakwenda kuwa sehemu ya kuwasaidia wanafunzi wengi kusoma kwa wakati mmoja hata kama wapo katika shule tofauti.

"Mfumo wa ufundishaji wa darasa janja ( Live Teaching) umeanzishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa lakini baada ya kuanzisha ulikwenda Wizarani na ukapitishwa kwahiyo kwasasa umekuwa mradi wa nchi nzima"amesema Dkt .Nicas 

Amesema kwa Kibaha Shule ya Bundikani ndio ya mfano lakini mfumo huo unafika kwa Shule Saba za awali na baadae watahakikisha wanapeleka katika Shule zote 24 za Sekondari zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

       Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha akivalishwa skafu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bundikani alipokwenda Shuleni hapo  Julai 31,2026 kwa ajili ya kuzindua darasa janja lenye mfumo wa teknolojia ya Tehama ( Live Teaching) .

Aidha,Dkt  Nicas amesema anatamani Serikali itambue mradi huo kwa jina la Dkt.Shemwelekwa Live Teaching huku akiiomba Wizara ya Elimu kutumia mradi huo na kuupeleka katika Shule zote za Sekondari nchini ili kuwasaidia Wanafunzi kusoma kwa urahisi zaidi.

Amesema kutokana na umuhimu na faida ya mfumo huo Manispaa ya Kibaha imeona itoe tuzo hiyo kwa ajili ya kutambua juhudi na kazi nzuri iliyofanywa Mkurugenzi huyo kwakuwa ameweka alama kubwa ambayo inakwenda kuvisaidia vizazi vya Taifa la Tanzania.

Amesema kilio kikubwa ni walimu wa Sayansi ambao hawatoshelezi kufundisha wanafunzi wote kwa wakati mmoja lakini kwa kuanzisha darasa janja litakuwa ni mkombozi na kwamba anapenda kuona kila Shule hiwe na darasa la Live Teaching.

Pamoja na kuzindua darasa janja katika Shule hiyo lakini pia Dkt .Nicas amesema Manispaa ya Kibaha imejipanga kuleta Mapinduzi ya elimu kwa kujenga miundombinu ya Shule yenye ghorofa na moja ya Shule atakayoanzanayo ni Shule ya Bundikani.

Amesema wameamua kufanya hivyo baada ya kuona ardhi haizaliwi ila watu wanaongezeka kila siku na hata idadi ya wanafunzi inazidi kuwa kubwa hivyo wanataka kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma katika mazingira mazuri na yenye kuvutia .

      Wanafunzi wa Skauti kutoka Shule ya Sekondari Bundikani wakimuongoza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas kukagua na kuzindua darasa janja la teknolojia ya Tehama lililojengwa katika Shule hiyo.

Aidha,Dkt.Nicas amemuagiza Mhandisi wa Manispaa ya Kibaha kuanza kuandaa mchoro wa jengo la ghorofa nne la Shule hiyo ilikusudi inapofika mwakani ujenzi uanze huku akisema zoezi la ujenzi wa Shule za ghorofa katika Manispaa utakuwa endelevu.

Amesema Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani ya elimu na Manispaa ya Kibaha ni wanufaika wakubwa wa fedha hizo kwahiyo ni vyema Rais akapewa haki yake.

Amesema katika vipindi vyote hakuna Rais aliyefanya vizuri kama Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani miaka ya nyuma wanafunzi walikuwa wanafaulu lakini kusoma ilikuwa shida kwakuwa miundombinu haikuwepo ya kutosha tofauti na kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele cha ujenzi wa madarasa ya shule.

Amewaomba wanafunzi wa Shule hiyo kwenda kuwa mabalozi wazuri wa kuyasemea yale yaliyofanywa na Mkuu wa Nchi pamoja na Serikali yake lakini lazima watambue Serikali haiwezi kutatua changamoto zote kwa wakati mmoja lakini kadri siku zinavyozidi kwenda mbele  ndivyo hatua zinavyochukuliwa.

Afisa Elimu wa Manispaa ya Kibaha Theresia Charles amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kujenga kwa darasa hilo ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji.

        Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha Theresia Charles.

Charles amesema Shule ya Sekondari Bundikani inazaidi ya wanafunzi 2400 lakini wanafunzi wa kidato cha nne pekee ni zaidi ya 400  na mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wote kwa wakati mmoja inakuwa ngumu lakini kupitia mfumo huo itakuwa rahisi kufundisha wanafunzi wote kuanza A hadi H.

Afisa utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha.

Mlela amesema Manispaa ya Kibaha ni kati ya Halmashauri ambazo zimepokea fedha nyingi kutoka Serikali Kuu inayoongozwa na Rais Samia na fedha hizo zimesimamiwa vizuri na Baraza la Madiwani na kuweza kuleta manufaa kwa Wananchi kwa kuwapa huduma bora.

Amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya kwani ukiangalia upande wa ukusanyaji wa mapato yameongezeka zaidi ya mara tano.

        Afisa utumishi wa Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela akiwa ameshika tuzo ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa aliyetunukiwa Julai 31,2026 kwa ajili ya ubunifu wa darasa janja linalotumia teknolojia ya Tehama.

Amesema Mkurugenzi wakati anateuliwa na Rais kuja Kibaha alikuta ukusanyaji wa mapato ni Sh.bilioni 5 lakini hadi sasa mapato yamefikia zaidi ya Sh . bilioni 26 fedha ambazo zinatumika katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

Amesema kupitia mapato ya ndani Manispaa imeweza kujenga Shule mbalimbali za Msingi zenye mchepuo wa lugha ya Kiingereza ikiwemo Shule ya Msingi  Mtakuja, Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere na Shule ya Msingi Mwambisi lakini kwa upande wa madarasa janja mpango ni kuhakikisha Shule zote za Sekondari zinakwenda kupata madarasa janja.

Amesema katika bajeti ya mwaka 2026/2027 Manispaa ya Kibaha imepanga kujenga Shule ya kwanza ya ghorofa ya mfano  katika Kata ya Pangani lakini wataangalia namna ya kujenga pia Shule ya ghorofa Bundikani.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Kibaha kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.

        Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka ( mwenye ushungi) akisikiliza kwa makini maelezo ya umuhimu wa darasa janja kutoka kwa Mwalimu wa Shule ya Bundikani Prosper Mwanjala.

Nyamka, amesema kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa ilani ambayo inajibu aadi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo amewaomba viongozi hao kuendelea kusimamia miradi hiyo ili kuwasaidia Wananchi kupata huduma bora kama ambavyo Rais anataka.

Diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi, amesema anaushukuru uongozi wa Manispaa kwa kujenga darasa janja katika Shule ya Sekondari Bundikani.

Lutambi amesema kuwa wamelipokea darasa hilo kwa furaha kubwa na wapo tayari kulitunza kwa faida ya Wananchi na wanafunzi wa Kata Mailimoja na Manispaa kwa ujumla.

Lutambi ,amesema kuwa tangu mwaka 2020/2025 Shule ya Sekondari Bundikani haina ziro na ameahidi kwa matokeo ya mwaka huu hakutakuwa na ziro na kwamba anataka wanafunzi wa kidato cha nne kwa asilimia 90 wafaulu kwenda ngazi ya juu.



No comments