HEADER AD

HEADER AD

TIMU YA WATAALAM YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA YAWAFUNDA WAJUMBE WA BODI ZA USULUHISHI WA MIGOGORO YA NDOA KATA YA KIMANGE NA MANDELA

Na Gustaphu Haule, Chalinze

TIMU ya wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) imefanikiwa kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za usuluhishi wa migogoro ya ndoa wa Kata ya Kimange na Kata ya Mandela kwa kuwapa  mafunzo na  elimu ya namna ya kukabiliana na migogoro ya ndoa inayojitokeza katika  maeneo yao.

Mbali na kutoa mafunzo na elimu kwa wajumbe wa bodi hizo lakini pia wataalamu hao wametumia nafasi hiyo kutatua  migogoro ya ardhi ukiwemo mgogoro wa siku nyingi unaomkabili Mkazi wa Kijiji cha Pongwe Kiona Kata ya Kimange Hadija Fungo.

Mafunzo hayo yametolewa Oktoba 31/2026 katika Kata hizo yakiongozwa na mratibu wa Kampeni hiyo ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere pamoja na mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni.

Wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia akiwemo Wakili Marwa Mohere mwenye kofia nyeupe ya kepu na mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni mwenye T-shirt nyeupe wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa wa Kata ya Kimange na Mandela mara baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika Oktoba 31/2026 katika ofisi ya Kata ya Mandela.

Katika mafunzo hayo , Mohere amewafundisha wajumbe wa  bodi hizo kuhusu usuluhishi wa migogoro ya ndoa sambamba na kuwapa nyaraka maalum zikatazotumika pale wanapofanya usuluhishi ambazo ni fomu namba 1,2 na namba 3.

Miongoni mwa mambo yaliyofundishwa kwa wajumbe hao ni pamoja na aina za ndoa,dhana ya ndoa,ndoa batili ,ndoa batilifu,na pia juu ya ufahamu kati ya bodi za usuluhishi na mabaraza ya ardhi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Wakili Mohere amesema kuwa Tanzania hakuna Sheria inayoruhusu  ndoa ya jinsia moja na kwamba ndoa pekee inayotambuliwa ni kati ya Mwanaume na Mwanamke na ndoa hizo mara nyingi ni za Kidini,Kiserikali na Kimila.

        Mtaalamu wa timu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Wakili Marwa Mohere akiwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa kutoka Kata ya Kimange na Mandela katika mafunzo yaliyofanyika Oktoba 31/2026 katika ofisi za Kata ya Mandela Halmashauri ya Chalinze.

Mohere amewaomba wajumbe wa bodi za usuluhishi wa Kata hizo kuhakikisha wanasimamia maadili ya kuhakikisha ndoa zote zinazofungwa ni zile ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria ya ndoa sura ya 29 toleo la mwaka 2023 lililofanyiwa marekebisho.

Amesema Bodi za usuluhishi za ndoa zimeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 102 cha Sheria za ndoa sura ya 29 na kupewa  majukumu mbalimbali ikiwemo kusuluhisha migogoro ya ndoa,kusikiliza pande zote,kufanya uchunguzi ,kutoa cheti cha kushindwa kusuluhisha na kusaidia mchakato wa talaka.

Mohere ameongeza kuwa bodi za  usuluhishi za Kata zipo kwa mujibu wa Sheria na kwamba wahakikishe wanatumia nafasi yao kuzuia ndoa za utotoni kwakuwa ndoa hizo zinakwamisha ndoto zao,lakini wasiwe wepesi kutoa fomu namba 3,kwa ajili ya talaka.

     Wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa Kata ya Kimange na Mandela wakijengewa na mtaalamu wa timu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Wakili Marwa Mohere Oktoba 31,2026.

"Nawasisitiza msiwe wepesi kutoa fomu namba za 3 katika usuluhishi kwani mkifanya hivyo mtakuwa mnaongeza watoto wa Mitaani kwasababu ya wazazi wao kutalakiana,",amesema Mohere.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni amewashauri wananchi wenye migogoro ya ardhi akiwemo Hadija Fungo kufungua shtaka katika baraza la ardhi la Kata ili kusudi wahusika waitwe na hatua zianze kuchukuliwa.

Maghaibuni amesema kuwa Mama Samia amesogeza huduma za kisheria karibu na wananchi ili waweze kusaidiwa kirahisi kutatua migogoro yao na hivyo kupata haki zao kirahisi na kwamba wale wote waliowasilisha migogoro yao kwa wataalamu wa sheria waamini haki itapatikana.

        Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni akiwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa katika mafunzo yaliyofanyika Oktoba 31/2026 katika ofisi ya Kata ya Mandela.

Mwenyekiti wa bodi ya usuluhishi Kata ya Mandela Kassim Majula ameeleza kufurahishwa na mafunzo yaliyotolewa na wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia na kusema elimu aliyoipata itakwenda kusaidia katika utatuzi wa migogoro katika maeneo yao.

Majula ,amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kwa kiasi kikubwa kupata elimu ambayo itawasaidia katika utatuzi wa migogoro ya ndoa na migogoro ya ardhi kwani wakati mwingine walikuwa hawajui namna ya kuisuluhisha kwakuwa hawakuwa na elimu ya kutosha.

"Mara kadhaa tumekuwa na utata hasa pale tunapotoa maamuzi yetu kwani inafikia mahali hata bodi yenyewe haielewi ianzie wapi na iishie wapi na tulikuwa tunashindwa kutofautisha kati ya bodi ya usuluhishi na baraza la ardhi la Kata na kiukweli elimu hii imetusaidia kuchanganua mambo,",amesema Majula.

Majula amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwamba alichofikiria ni kikubwa kwakuwa awali wananchi walikuwa wanahangaika na wakati mwingine watu walikuwa wanapigana na kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii.

Amesema huduma za kisheria zilikuwa mbali kiasi ambacho wananchi walikuwa wanahangaika lakini kwasasa huduma hizo zipo nchi nzima na zinafika Kata kwa Kata kitendo ambacho kimesaidia kupunguza migogoro na kuleta amani sehemu ambazo hapakuwa na amani.

Mwananchi wa Kijiji cha Pongwe Kiona Kata ya Kimange Halmashauri ya Chalinze Hadija Fungo amesema amefurahi kukutana na wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwakuwa muda mrefu alikuwa anahangaika kutafuta wanasheria.

Fungo amesema alikuwa anatamani kumuona Rais Samia ili amfikishie mgogoro wake lakini kupitia wanasheria waliopo katika kampeni ya msaada wa kisheria ameridhika na ushauri aliohupata na kwamba anaimani mgogoro wake utapata ufumbuzi.

        Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni akimsaidia Hadija Fungo Mkazi wa Kijiji cha Pongwe Kiona Kata ya Kimange kumtatulia mgogoro wake wa ardhi uliodumu tangu mwaka 2017.


No comments