BARAZA LA WAANDISHI WA HABARI AFRIKA LAMCHAGUA MWENYEKITI CAJ
Rais mpya wa CAJ,Christopher Isiguzo kutoka nchini Nigeria
Na Mwandishi Wetu,Nairobi
BODI ya Uongozi ya Baraza la Waandishi wa Habari Afrika (CAJ) imemchagua Christopher Isiguzo kuwa Rais mpya wa CAJ huku ikitangaza rasmi Jiji la Nairobi, Kenya kuwa Makao makuu ya Bodi.
Isiguzo anatoka nchini Nigeria ambaye pia ni Rais wa Muungano wa Wanahabari wa Nigeria (NUJ) ambapo amesema kuwa Baraza hilo linaendelea kuchukua jukumu la kulinda na kutetea uhuru wa kujieleza na habari kama ilivyoainishwa katika Azimio la Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Kupata Habari Barani Afrika.
Isiguzo amechukua nafasi ya Rais mwanzilishi Alexandre Niyungeko ambaye pia ni Rais wa Muungano wa wanahabari wa Burundi UBJ ambaye amejiuzulu kutokana na majukumu mengine.
Mkutano huo ulikuwa wa kujadili maendeleo ya taasisi hiyo na kutoa mamlaka ya kisheria kuanzishwa kwa Sekretarieti ya CAJ Jijini Nairobi, Nchini Kenya.
CAJ iliyozinduliwaJuni 23 mwaka 2020, imesajiliwa rasmi chini ya sheria za Kenya ambapo katika kikao chake, bodi hiyo pia imetangaza maendeleo mapya yaliyofikiwa kisheria yanayotoa msukumo kukabiliana na changamoto za waandishi wa habari bara la Afrika.
Baraza la CAJ linalenga kuleta mtazamo wa Kiafrika kwa masuala ya kushughulikia changamoto za uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari, na upatikanaji wa habari, unaoathiri wanahabari wanapokuwa wakifanya kazi zao kulingana na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 na mwamko wa Kiafrika kukabiliana na masuala hayo.
William Oloo kutoka chama cha Wanahabari wa Kenya(KCA) anaendelea kushika nafasi yake ya Katibu wa CAJ na mweka hazina, Bi. Monique Kacou kutoka nchini Ivory cost (Cote d'Iviore).
Wajumbe wengine wa Baraza la Uongozi ni: Ibrahima Ndiaye kutoka nchini Senegal,Bi.Idda Francis Mushi kutoka Tanzania,Bi.Indira Correia Balde kutoka Guinea - Bissau,
Syabonga Dlamini wa Swaziland,Abdalle Ahmed Mumin wa Somalia,Bi.Patsy Athanase wa visiwa vya Shelisheli (Seychelles) na Emmanuel Chibwana kutoka nchini Malawi.
Katika hatua nyingine, Mjumbe mwingine mpya anatarajiwa kutangazwa wakati wowote toka sasa kuziba nafasi ya Foster Dongozi kutoka Zimbabwe aliyefariki dunia Desemba mwaka Jana.
"Sote tunafurahia usajili wa CAJ kwa sababu hii itaiwezesha kutekeleza jukumu lake katika kuchangia utatuzi wa changamoto zinazowakabili waandishi wa habari barani Afrika,'' Alisema Alexander Niyungeko, Rais wa CAJ aliyemaliza muda wake.
Alisisitiza wadau mbalimbali kushirikiana na Baraza hilo kuleta maendeleo yanayokusudiwa katika tasnia ya habari kwani yatatoa nafasi ya kusonga mbele na kutoa nafasi ya kuthibitisha mamlaka hiyo kusonga mbele kwa kasi kubwa katika kutekeleza wajibu wa kushughulikia matatizo yanayowakabili wanahabari barani Afrika.
Rais Isiguzo pia alisisitiza dhamira kubwa ya CAJ kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanahabari barani ambapo tayari wameidhinisha vikao vya mashauriano vya kikanda kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari (UNPA) unaoongozwa na UNESCO.
"Matokeo haya yatachangia kuboreshwa kwa juhudi katika kushughulikia suala hili la usalama wa wanahabari barani Afrika" Alisema Rais huyo mpya wa CAJ.
Imeelezwa kuwa hivi karibuni CAJ wataweka wazi mpango wa shughuli mbalimbali watakazofanya zikilenga kushughulikia dhamira za wanahabari barani Afrika ambapo Rais Isiguzo amewaalika washirika mbalimbali wa maendeleo na masuala ya wanahabari kufanya nao kazi nasi kufanikisha malengo hayo.
Post a Comment