HEADER AD

HEADER AD

HATI YA PAPO KWA PAPO CHACHU YA MAFANIKIO


Na Dinna Maningo,Tarime

ARDHI ni muhimu na hitaji kubwa kwa Maisha ya Binadamu bila ardhi huwezi kujenga nyumba wala kulima shamba, bila ardhi hakuna mazao, uthamani wa ardhi unakuwepo pale tu mtu anapokuwa na Hati ya kumiliki ardhi.

Mtu anapokuwa na Hati (Cheti) cha kumiliki ardhi anakuwa na uhakika wa usalama wa ardhi yake anayoimiliki, nyumba au maendeleo yoyote aliyoyafanya katika ardhi yake.

Hatimiliki ya ardhi ni nyaraka maalumu inayotolewa na Wizara ya ardhi ikionesha mwenye haki ya umiliki wa ardhi,eneo na kiasi anachomiliki huku ikiainisha wajibu na haki alizonazo mmiliki huyo.

Hivi karibuni Septemba,16,2022 ofisi ya Ardhi mkoa wa Mara kwa kushirikiana na ofisi ya ardhi Halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia wataalamu wa ardhi wakiongozwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara  Happiness Mtutwa wakapiga kambi kwa siku mbili ofisi ya kijiji cha Nyangoto kilichopo Nyamongo Kata ya Matongo wilaya ya Tarime.




Wataalam wa ardhi walifika kijijini kutoa huduma ya umilikijashi wa ardhi na hutoaji wa Hati papo kwa papo ambapo jumla ya Hati 120 zimetolewa kwa wananchi huku wakiipongeza Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia wataalamu wa ardhi kufika kijijini kutoa huduma ya papo kwa papo.
 
Imeelezwa kuwa utoaji Hati za  papo kwa papo ni matarajio ya mafanikio kwa wananchi wa Kijiji cha Nyangoto ambao walishindwa kupata mikopo na uhakika wa umiliki wa radhi kwakuwa walikuwa na ardhi ambayo waliishi nayo kwa mashaka wengine wakidhani huwenda walijenga kwenye maeneo ya wazi ya serikali lakni baada ya kupimiwa ardhi na kupata Hati hofu iliyotanda kwenye fikra zao imekwisha.

"Ardhi ni mtaji  ukiitunza na yenyewe itakutunza" Ni kauli ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara Happiness Mtutwa wakati akizungumza na Mwandishi wa Habari wa DIMA Online aliyefika ofisi ya Kijiji cha Nyangoto na kukuta zoezi likiendelea la utoaji wa huduma ya Hati za papo kwa papo.


Happiness anasema kuwa yeye na timu nzima ya wataalamu wa ardhi wanazunguka halmashauri zote tisa mkoa wa Mara kutatua migogoro ya ardhi,zoezi la umilikishaji wa viwanja na utoaji wa Hati papo kwa papo.

" Tupo hapa kwa niaba ya ya Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,lengo letu ni kuhakikisha tunawafikia wananchi tunatoa huduma karibu kwa kuwafuata walipo,huko nyuma ilikuwa mpaka uende Dar es Salaam kufuatilia Hati baadae huduma ikasogezwa mkoani,na sasa tunawafuata wanachi mahali walipo hatukai ofisini, mtu analipia kiwanja chake anapewa hati tunasaini anachukua"anasema.

Faida ya kuwa na Hati ya kumiliki ardhi

Kamishna huyo wa ardhi anasema kuwa ardhi ni mtaji ukiitunza na yenyewe inakutunza na ina faida nyingi kwa maendeleo ya mwananchi hivyo ni muhimu wananchi kupima maeneo yao ili wapate hatimiliki ya ardhi.

Happiness anasema kuwa mtu anapokuwa na Hati, ardhi huongezeka thamani na anakuwa na uhakika wa thamani yake kuliko asiye na hati na inasaidia kupunguza migogoro ya ardhi kwakuwa kwenye Hati inaonesha mipaka ya ardhi.

"Usipokuwa na hatimiliki unakuwa na ardhi isiyo kusaidia,ukiwa na Hati unapeleka kama dhamana kupitia Hati na inakufanya uweze kukopeshwa fedha benki,nawasisitiza maeneo mengine ambao hawajapima viwanja wajitokeze  wapimiwe,gharama ya kupimiwa ni 130,000 kwa maeneo ya urathimishaji, gharama za umilikishwaji inategemea na kiwanja cha mtu na matumizi yake.

"Maombi ya kuandaa Hati mwananchi analipia 20,000, Ramani 20,000,Hati yeyewe 50,000,gharama hizi ni za lazima kiasi kingine kinachobaki inategemea na ukubwa wa uwanja wako , wananchi wengi wanacheza kwenye 150,000 260,000"anasema Happiness.

Kamishna huyo wa ardhi anasema Kijiji cha Nyangoto wananchi wengi wana uelewa na uhitaji ambapo zaidi ya viwanja 8,000 vimepimwa na kwamba zoezi la utoaji wa Hati papo kwa papo ni endelevu.

"Tulipata taarifa kuwa wananchi wanahitaji huduma tumefika na tumetoa hati.Wananchi waelewe kuwa hati zipo zinapatikana kwa urahisi japo wapo wananchi wanaamini hati zinapatikana kwa shida ,serikali ya awamu ya sita ni sikivu inafikisha huduma kwa ukaribu"anasema.

Sheria ya ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, na Sheria Na 5 zinatoa mfumo wa kisheria wa kusimamia ardhi na usalama wa umiliki nchini, udhibiti wa maslahi ya ardhi na matumizi bora ya ardhi kwa kuwapimia wananchi ardhi yao na kumilikishwa.

Afisa Ardhi Halmshauri ya wilaya ya Tarime Philipo Malach anasema kuwa Kijijji cha Nyangoto kimepimwa 2019 kwa ufadhili wa Mgodi wa North Mara ambapo ardhi yote ya kijiji cha Nyangoto imepimwa.

"Kijiji kizima kimepimwa na baadhi ya wananchi wameshalipa fedha wamechukua hati zao zoezi limefanyika papo kwa papo wataalamu wote wa ardhi walikuwepo kama Afisa ardhi mteule,mpima ardhi,mchapa kava Afisa ardhi msaidizi,Msajili,Kamishna,Afisa Kodi na Vitendea kazi vilikuwepo pamoja na usafiri wa kusafirisha wataalamu "anasema Malach.

Bhoke Gitano mkazi wa kijiji cha Nyangoto anasema kuwa amefurahi kupata Hati kwakuwa hajatumia gharama ya usafiri kufuatilia hati ofisi ya ardhi mkoa huku akiwasisitiza ambao hawajachukua hati wakamilishe malipo ili wapewe hati zao.

"Nimefurahi sana kupata hati tulikuwa tunaisikia tu huko Dar kupitia vyombo vya habari lakini leo nimeipokea hapahapa kijijini,nililipa fedha mwezi wa nne mwaka jana nimeipata bila hata kuifuatilia kwa kulipa gharama za usafiri kwenda mkoani nimetembea kwa miguu yangu hadi hapa ofisini,nilikuwa nasikia hatihati sasa nimeiona kwa macho" anasema Bhoke.

Sadock Maningo anasema kuwa mtu anapokuwa na hati anakuwa na uhakika wa ardhi yake,na inasaidia kupunguza migogoro ya mipaka kwakuwa Hati hizo zinaonesha mipaka ya umiliki ardhi ya mtu na kwamba Hati hiyo itamsaidia kupata mkopo benki.

"Sasa hivi mtu akinisogelea kuhusu ardhi mi nanyamaza tu maana nina Hati inayonilinda kisheria,hata mgodi ukitaka eneo langu lazima wapite kwangu na nikitaka kuomba mikopo benki nitapata maana nina dhamana ya hati" anasema Sadock.

Shaban Omary yeye hakubahatika kupata Hati kutokana na herufi ya jina lake kukosewa " Mimi nimekosa hati kwasababu jina langu limekosewa kwenye kitambulisho cha NIDA tunaomba hii huduma ya papo kwa papo inapotolewa watu wa NIDA wawe wanakuwepo ili kufanya marekebisho ya majina kwenye vitambulisjo wao ndio walikosea majina yetu wakati wanatuandikisha.

"Nimeambiwa niende ofisi za ardhi Musoma alafu niende kwa mwanasheria mkoa nikaape,ni gharama natakiwa niwe na pesa lakini hii huduma ningeipata hapa kijijini ingekuwa imenipunguzia usumbufu na gharama za usafiri nimekosa hati kwasababu ya jina kukosewa kwenye kitambulisho cha NIDA"anasema Shaban.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Stooni Kijiji cha Nyangoto Simion Maguri anasema kuwa kilichowasukuma kufanya upimaji ni kutokana na Kijiji kuwa na msongamano wa watu wengi na nyumba nyingi zilizojengwa.

Anazitaja faida za kupata Hati kuwa itasaidia serikali kukusanya kodi ya ardhi,kuepuka migogoro ya ardhi kwamba vita ya kugombania ardhi itaisha,itasaidia mahusiano kuwa mazuri Kati ya mtu na mtu hasa kwa majirani kwakuwa kila mtu atafahamu mipaka yake hivyo miingiliano ya mipaka haitakuwepo.

Simon anaushukuru Mgodi wa North Mara kwa kukithamini Kijiji hicho na kutoa fedha kupima ardhi yote ya Kijiji bila wananchi kutozwa fedha za upimaji "Tunaushukuru mgodi kwa kukifadhili Kijiji kimepimwa,pia tunaishukuru serikali kupitia idara ya ardhi kwa kutuletea huduma kijijini karibu na wananchi,unalipia hapohapo Hati inatengenezwa siku hiyo hiyo unapewa,watu walikuwa wanahangaika kwenda wilayani na mkoani kufuatilia hati na mizunguko ya huko ni mingi "anasema Simon.

Mpimaji wa ardhi mkoa wa Mara Pastory Katanga anasema kuwa hatimiliki ni muhimu kwa kila mwananchi ambaye amepimiwa ardhi na kamba ni vyema wananchi ambao hawajapimiwa wajitokeze wajiunge kweye vikundi katika mitaa yao kisha wapimaji wa ardhi watafika kuwapimia ardhi.

"Hamasa ya watu kujitokeza kupimiwa ardhi ni wastani,urasimishaji unaanzia serikali ya kijiji au mtaa,mkutano mkuu wa Kijiji kisha tunatoa elimu ,kwa sababu zoezi hili ni shirikishi kamati za upimaji za mtaa au kijii zinaundwa wajumbe wake wanachanguliwa na wananchi wanachagua Mwenyekiti,mweka hazina na katibu ,baada ya hapo inafunguliwa akaunti ya upimaji ya mtaa kisha wananchi wanachangia kiasi cha fedha kinachotakiwa.

"Zoezi hilo likishafanyika  ndio tunapima na tunapopima tunapima maeneo yote hata kama watakuwepo ambao hawajalipa fedha watapimiwa na wataendelea kulipa fedha.

Pastory anaongeza kuwa uchangiaji wa fedha za upimaji mkoani Mara bado ni changamoto "Mwingine atalipa fedha leo mwingine atalipa baada ya miezi kadhaa hali hii inaibua malalamiko kwa wale waliotangulia kulipa fedha kwakuwa zinakuwa hazijatosha ili kuwapimia hivyo wanajikuta wakichelewa kupimiwa kwa sababu ya wenzao kuchelewa kulipa fedha za upimaji"anasema.

Sera ya ardhi ya Taifa ya mwaka 1995 inamtaka kila mtu kujua mipaka ya mtu na mtu na mipaka ya nchi kwa kupima ardhi anayomiliki ili kuweka kumbukumbu sawa ya umiliki wa maeneo kwa kutambua ukubwa wake.

ARDHI ni sehemu yoyote iliyo juu na chini ya uso wa nchi,vitu vyote vyenye kuota kiasili juu ya nchi,majengo na miundombinu mingineyo iliyokaziwa  kwa kudumu juu ya ardhi.








No comments