GRUMET FUND YAWAFUNDA WASICHANA KUJILINDA
Mgeni Rasmi Bi.Rehema koka akigawa Taulo za kike kwa wasichana 657 waliofika kwenye kongamano hilo |
Na Mwihava, GF -SERENGETI
Kampuni ya Grumet Fund kupitia idara yake ya maendeleo ya jamii imetoa mafunzo kwa wasichana 657 kupitia progam ya girls Empowerment session tuko pamoja yaliyolenga juu ya kujitambua, kujisimamia na kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji kwa mtoto wa kike.
Wasichana Kutoka Baadhi ya Shule Wilayani bunda na Serengeti wakifatilia mafunzo kwa Makini kutoka kwa wawezeshaji wakati wa Kongamano hilo wilayani Serengeti |
Pia taulo za kike 657 zimetolewa kwa wasichana hao ambao ni wanafunzi kutoka shule za sekondari Hunyari, Sazira na Paul Jones za wilayani Bunda na shule za sekondari Robanda na Mugumu za wilayani Serengeti.
Akifungua mafunzo hayo mgeni rasmi Rehema koka ambaye ni mkuu wa idara ya mifugo wilaya ya Serengeti amewasihi wasichana kujisimamia na kutokukimbilia mila potofu lakini pia ameishukuru na kuipongeza kampuni ya Grumet Fund kwa kujitoa kuwapa elimu wasichani mkoani Mara.
Amesisitiza wasichana hao kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao pamoja licha ya kuwepo vikwazo mbalimbali vinavyowazunguka.
‘’Zipo changamoto za mila potofu zinazomuathiri mtoto wa kike,hedhi ambayo huwatesa baadhi ya wasichana na kuwapotezea muda kutokana na visumbufu vichache,lakini pia umbali kwa baadhi ya watoto wa kike pamoja na changmaoto ya kukatishwa tamaa’’alisema Rehema.
Meneja wa maendeleo ya jamii kutoka kampuni ya Grumet Fund Frida mollel amewataka mabinti kujitambua na kujitegemea bila kusubiri watu wengine kuwafanyia maamuzi ya maisha yao haswa katika vitu visivyofaa vinavyoharibu maisha yao ya sasa na baadae.
Meneja wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Kampuni ya Grumet Fund Bi.Frida Mollel akisema Jambo wakati wa Kongamano hilo |
‘’Sisi Grumet Fund tumekuja hapa kuwapa nguvu na kuwambia kwamba mabinti mnahaki ya elimu,lakini mnahaki ya kusema hapana dhidi ya mila potofu zinazowakandamiza ikiwemo ndoa za utotoni,ukeketaji,mimba za utotoni mnahaki ya kujisimamia na kuachana na makundi potofu’’ alisistiza Frida
Mtaalamu wa afya kutoka hospitali teule ya nyerere (NDDH ) Restuna mluta amewakumbusha wasichana waliohudhuria mafunzo hayo kuwa wanapoonza hedhi ni kiashiria kwamba wako tayari kubeba ujauzito na kuitwa mama, amewataka kuzingatia umri salama wa wao kupata mimba.
Aliongeza kuwa kupata ujauzito katika umri mdogo kunaweza kupelekea madhara kwa mama na mtoto atakaezaliwa , aidha amewataka wasichana kujikinga na mimba za utoto kwa kusema hapana ,lakini pia kuzingatia masomo na hatimaye kutimiza ndoto zao.
Afisa kutoka Dawati la jinsia na watoto wilaya ya Serengeti Sijali Nyambuche amewakumbusha kuwa mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza vitendo vya ukeketaji hivyo amewataka wasichana kutokukubali vitendo hivyo kutokana na madhara makubwa yanayojitokeza ya kukeketwa.
Wasichana waliopata mafunzo hayo kupitia kongamano hilo wameishukuru kampuni ya Grumet Fund kuwapa elimu hiyo na kuiomba serikali na wadau wengine kuongeza zaid makongamano ya aina hiyo ili waelimike zaidi.
Post a Comment