WANAWAKE 4,000,WATOTO 65,000 HUFARIKI KILA MWAKA
Na Mwandishi wetu,New York, Marekani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Philip Mpango amesema kuwa nchini Tanzania takribani wanawake 4,000 na watoto 65,000 hufariki kila mwaka huku uchelewaji wa kupata huduma za dharura na usafiri wa dharura ukichangia kuwepo kwa vifo hivyo.
Dkt.Mpango ameyasema hayo akiwa nchini Marekani akiwa amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu katika mkutano mkuu wa 77 wa wakuu wa nchi (UNGA) unaoendelea jiji la New York nchini humo.
Hata hivyo katika mkutano huo kampuni ya Vodafone imeahidi kuipatia nchi ya Tanzania msaada wa fedha Dola Milioni 15 (Takribani Tsh.Bilioni 34) ili kuwezesha usafiri wa dharura kwa wajawazito.
Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa kampuni ya Vodafone Joachim Reiter ameahidi katika kikao hicho mbele ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la misaada la Marekani (USAID) Samantha Power.
Joachim amesema kampuni inatarajia kutoa fedha ili kutekeleza mradi huo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu za kukuza uchumi nchini.
Ameongeza kuwa makampuni binafsi yana jukumu muhimu la kushirikiana na serikali kuleta maendeleo na kuchangia ustawi wa jamii.
Waziri wa Afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu aliyeambatana na Makamu wa Rais katika mkutano huo, ameleza furaha yake kwa Tanzania kupatiwa mradi huo.
Amesema mradi huo utaisaidia Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika Mkakati wa Tano wa Afya na Mpango Mkakati wa Tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (one plan 3) ambayo moja ya vipaumbele ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto hivyo msaada huo utakuwa chachu ya kuiwezesha nchi kufikia malengo endelevu ya kidunia.
Serikali ya Marekani kupitia USAID huzipatia pia kampuni binafsi fedha kuwezesha kufikia nchi zenye uhitaji mkubwa.
Picha.Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa USAID Samantha Power (katikati) na Joachim Reiter Mkuu wa masuala ya Kimataifa wa kampuni ya Vodafone.
Post a Comment