WAVUTIWA NA MAONESHO YA CHUO CHA WANYAMAPORI, UTALII
Na Jovina Massano,Musoma.
WANANCHI zaidi ya 7000 wamepata elimu ya Uhifadhi,Utalii pamoja na Utunzaji wa Mazingira katika Maonesho ya Mara International Business Expo yaliyofanyika kwa siku kumi viwanja vya Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Didace Dawson kutoka chuo cha Wanyamapori Pasiansi Wildlife Training Institute alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ambalo lilikuwa limejumuisha Taasisi zote, mawakala na Wadau wa Utalii ambao wako chini ya Wizara.
"Mimi ni mtumishi kutoka Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi nipo hapa kumwakilisha mkuu wangu wa chuo Jeremaya Msigwa,tuna huduma ya elimu ya Wanyamapori na Kuongoza Watalii kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na cha sita wenye ufaulu wa alama D masomo ya Sayansi hasa Biologia,kiingereza na Geografia lakini kwa kuongeza wigo wa ajira tumeanzisha kampuni ya ulinzi ili kusaidia vijana kuwa na ajira iitwayo Pasiansi Wildlife Security Company",alisema Didace Dawson kutoka Chuo cha Wanyamapori Pasiansi-Mwanza.
Nae Zegera Alfred Kunani Mkufunzi Chuo cha Taifa cha Utalii Mwanza amesema wapo kwenye maonyesho ya MIBE kuelimisha umma kuhusu fursa zilizopo kwenye utalii lakini pia Elimu ya jinsi gani watu wanaweza kupata Mafunzo ya Utalii.
"Watu wengi walitamani sana kujua kwa jinsi gani wanaweza kupata fursa ya kusoma maswala ya utalii nimewaeleza vigezo vitakavyo wawezesha kujiunga lakini pia namna chuo cha utalii kinavyotoa mafunzo na kuandaa wataalam bobezi kwenye sekta ya utalii na wanafunzi wengi wameonesha mwamko wa kutaka kusoma maswala ya utalii"alisema Kunani.
Aliongeza kuwa "kupitia Maonesho haya tutaongeza idadi ya wanafunzi wengi, pia yamejikita zaidi kumjengea mwanafunzi kujifua kwa vitendo zaidi chuoni kwa kutembelea hifadhi na maeneo tofauti nchini,Chuo kinatazamana na hospitali ya rufaa ya Sekou Toure Mwanza
Kinatoa mafunzo kwa fani mbili ya Uongozaji watalii, Usafirishaji na utalii kwa ngazi ya Cheti na diploma"Zegera Alfred Kunani Mkufunzi Chuo cha Taifa cha Utalii Mwanza
Kwa upande wake Fides Shao alisema kuwa kupitia maonesho hayo ameelewa vitu vya utalii vilivyopo na mahali elimu inapopatikana kwani alikuwa akielewa kuwa vyuo vya utalii vipo Dar es Salaam na Arusha kumbe hata kanda ya ziwa vipo na aliahidi kufika chuoni kwa ajili ya kumpeleka mwanae kwa kuwa anapenda kusomea Mambo ya Utalii.
Post a Comment