BARIADI WATAKIWA KUTEMBELEA HIFADHI ZA TAIFA
Na Annastazia Paul Bariadi, Simiyu.
MKUU wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange ametoa wito kwa wakazi na maeneo mengine kujijengea utaratibu wa kutembelea maeneo ya Hifadhi za Taifa kufanya utalii wa ndani ili kuunga mkono jitihada za serikali zinazofanywa katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa lango la Andajega lililofunguliwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kuingia katika hifadhi ya taifa ya Serengeti, amesema kufunguliwa kwa lango hilo kutawarahisishia watalii kuingia katika hifadhi hiyo pamoja na pori la akiba la Kijereshi.
“Lango hili lilikuwa limefungwa kwa muda mrefu sana, lakini tunaishukuru sana TANAPA, mkuu wa wilaya ya Serengeti kwa kuridhia kwamba sasa tunakwenda kushikana mkono kuhakikisha tunafungua utalii kupitia lango hili la Serengeti.” amesema Kapange.
Kapange amesema kwa sasa lango hilo (Andajega) limefunguliwa rasmi kwa ajili ya kuwawezesha watalii kuingia hifadhini kufanya utalii na pia litawasaidia kuifikia hifadhi hiyo kwa urahisi zaidi.
“Kutoka hapa kuingia Kilawila ni kilomita 12 tu, eneo ambalo lina wanyama wengi sana, kwahiyo watu wanaweza kufika hapa wakaona wanyama wanaotaka, pia pamoja na pori la akiba la Kijereshi kwahiyo unarahisisha mfano unataka kutembelea kilomita 50 unakuwa umetembelea Serengeti kiasi cha kutosha, unakuwa umetembea na pori la akiba la Kijereshi kiasi cha kutosha ambako kote kuna wanyama.’’ amesema Kapange.
Fredrick Severine ni askari mhifadhi daraja la tatu katika hifadhi hiyo ambaye anaeleza kuwa kufunguliwa kwa lango hilo kutasaidia kupunguza ujangili na kukuza utalii katika maeneo hayo.
“Kutokana na hiki kituo kufungwa muda mrefu, kimeleta changamoto zikiwemo tabia za wanyama kubadilika, wanyama wamekuwa wakiona magari wanakimbia hawajazoea watu pamoja na watalii ni kwasababu wanasumbuliwa na ujangili, ujangili pia umekuja juu kwasababu maeneo haya hayapitiki sana zaidi ya sisi kufanya doria katika maeneo.
"Lakini pia mji umeshindwa kukua kutokana na kwamba watu wamekuwa wakilima mahindi yanaharibiwa na tembo pamoja na simba wamekuwa wakivamia na kula mifugo, hivyo kufunguliwa kwa lango hili kutasaidia changamoto hizi utalii watu wataweza kufanya biashara zingine kama kuchonga vinyago na kutangaza utamaduni wa makabila yao ..kufunguliwa kwa geti hili pia kutasaidia sana kukuza utalii wa kitamaduni.” amesema Severine.
Mwongozaji watalii kutoka kampuni ya Sayona Safari’s anayeongoza watalii katika hifadhi ya taifa ya Serengeti Jessie Sospeter Mpanda amezitaja changamoto wanazokabiliana nazo hasa kipindi cha masika kuwa ni pamoja na barabara kutopitika kirahisi wakati wa mvua nakwamba serikali imeendelea kufanya jitihada kuzitatua.
“Mara nyingi wanyama tunawapata katika maeneo ya uficho uficho, kipindi cha mvua wakati mwingine njia hazipitiki hata barabara kubwa zinakuwa hazipitiki, lakini sasa wamefanya jitihada nzuri hata ukipita barabara kubwa wameweka madaraja na makaravati.
" Upande huu wa kanda ya magharibi ya Serengeti tulikuwa na shida sana kwenye lile daraja la Gulumeti likifurika kipindi cha mvua magari kupita ilikuwa ni shida lakini sasa TANAPA wametutengenezea daraja la kupita juu.” amesema Mpanda.
Post a Comment