WAGONJWA WA AKILI MILIONI SITA HAWAPATI HUDUMA YA AFYA
Na WAF, Dar es Salaam
IMEELEZWA kuwa wagonjwa wa akili takribani 711,789 sawa na asilimia 10 tu wamepata huduma ya afya ya akili idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa Milioni saba huku wagonjwa wakiongezeka kwa asilimia 13 Duniani.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza Wizara ya Afya Dkt.James Kiologwe katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya afya ya akili duniani yaliyofanyika Oktoba 3, 2022 katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam, yenye kauli mbiu ya "Afya ya akili ni kipaumbele kwa wote."
Dkt. James amesema takwimu kutoka vituo vya kutolea huduma za afya ya mwaka 2019/2020 hapa nchini zinaonyesha kuwa, takribani wagonjwa 711,789 sawa na asilimia 10 tu ya wagojwa Milioni 7 wamepatiwa huduma za afya ya akili na kukiri kuwa idadi hiyo ya mahudhulio ni ndogo na kwamba sababu inatokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na matatizo mbalimbali ya afya ya akili na unyanyapaa.
Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge amesema kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kumekuwa na ongezeko la takribani asilimia 13 la wagonjwa wa akili.
"Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kumekuwa na ongezeko la takribani asilimia 13 la wagonjwa wa akili, inakadiriwa kuwa na wagonjwa Milioni 7 wenye magonjwa mbalimbali ya akili na matumizi ya dawa za kulevya nchini, huku miongoni mwao zaidi ya watu milioni1.5 wanaishi na ugonjwa wa Sonona (Depression)"amesema Rehema.
Ametaja sababu kubwa ya matatizo ya Afya ya akili ni mabadiliko katika mfumo wa malezi ndani ya familia na jamii, msongo wa mawazo na matumizi ya vilevi kupita kiasi hususani pombe, bangi na dawa nyingine za kulevya.
Rehema ameweka wazi kuwa, kumekuwa na matukio mengi ya ukatili ambapo wanawake wanne kati ya kumi walio katika umri wa miaka 15 – 49 walifanyiwa ukatili wa kimwili, wakati takribani wanawake wawili kati ya kumi walifanyiwa ukatili wa kingono, hii hutokana na ongezeko la magonjwa ya akili.
Ametoa wito kwa wananchi kusaidia wahusika wa matatizo ya afya ya akili kupata matibabu, huku akisisitiza kuepuka unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa badala yake wawasaidie kurudi katika hali ya kawaida.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema, mpaka sasa huduma za afya ya akili zinaendelea kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na vya binafsi Jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa huduma ziantolewa kwa kutumia wataalamu wabobezi katika utoaji wa huduma za afya ya akili, lakini katika vituo ambavyo havina wabobezi wa afya ya akili watoa huduma wengine wamekuwa wakijengewa uwezo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma hiyo.
Post a Comment