BILIONI 80 KUJENGA MAGHALA YA KUHIFADHI MAZAO
Na Annastazia Paul, Simiyu
JUMLA ya shilingi Bilioni 80 zinatarajiwa kutumika kujenga maghala 14 nchini kwa ajili ya kuhifadhia mazao ya nafaka ili kudhibiti sumukuvu na kumuwezesha mkulima kupata tija kupitia kilimo.
Maghala hayo yanajengwa kupitia mradi wa kudhibiti sumukuvu Tanzania unatekelezwa kwenye mikoa 10 ikiwemo mkoa wa Simiyu na kuhusisha halmashauri 18 nchini ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Itilima .
Hayo yamesemwa na mratibu wa mradi wa kudhibiti sumukuvu Tanzania Kassim Msuya akiwa kijiji cha Ikindilo kilichopo wilayani Itilima mkoani Simiyu ikiwa ni siku ya maalum ya elimu ya kudhibiti sumukuvu iliyotolewa ndani ya wiki ya chakula duniani ambayo kitaifa inafanyika mkoani Simiyu.
"Mwaka 2016 sumukuvu ilileta madhara kwa Tanzania kwenye mikoa miwili ya Dodoma na Manyara tulipoteza watu 19 Chemba na Kondoa kwasababu ya kula chakula chenye sumukuvu,serikali ikaamua kuja na mradi mahususi kwaajili ya kupambana na sumukuvu unaoitwa mradi wa kudhibiti sumukuvu Tanzania ambao unatekelezwa Tanzania bara na Zanzibar, "amesema Msuya.
Maghala hayo 12 yanajengwa Tanzania bara na mawili Zanzibar ambapo mradi huo una maeneo makuu matatu ambayo ni ujenzi wa miundombinu , soko la mazao , na maabara kuu ya kilimo.
"Moja ya maeneo katika mradi ni ujenzi wa miundombinu,tunajenga kituo cha kibaiolojia Kibaha ambacho ujenzi upo asilimia 98 na ni mahususi kwaajili ya kudhibiti ubora wa viuatilifu ambavyo ni vya kibaiolojia, eneo jingine ni soko la mazao ambalo linajengwa Kongwa ujenzi upo asilimia 40 na kituo hicho kitakuwa na maabara, soko, mtambo wa usindikaji.
"Nafaka yakiwemo mahindi yatakayokuwa yanauzwa nje ya nchi yatakuwa yamepitia utaratibu huu wa maabara,eneo jingine ni maabara kuu ya kilimo inayojengwa Dodoma," amesema Msuya na kuongeza kuwa:
"Maghala haya tofauti kidogo na maghala mengine yamejengwa
kwa kuzingatia udhibiti wa sumukuvu,tuna maabara, tuna ghala, kwaajili ya kuhakikisha kama nafaka inaingia kwenye ghala inachekiwa kwanza ubora wake na kama nafaka inaingia kwenye ghala haijakauka vizuri sehemu ya kukaushia vizuri ili ikauke.
" Hii maabara tutaiwekea vifaa vyote vya kimaabara na vifaa vya kupima kuhakikisha kwamba sumukuvu haipo katika mazao yoyote yatakayoingizwa hapa kwenye ghala ili mfanyabiashara akija kununua mazao hapa ya Ikindilo ana uhakika kwamba ni mazao ambayo hayana tatizo lolote la sumukuvu" ameongeza Msuya .
Msuya amesema ghala hilo likikamilika litakuwa mali ya halmashauri lakini yataendeshwa na wanakijiji wenyewe huku akiongeza kuwa ghala hilo linajengwa na mkandarasi kutoka kampuni ya Nice construction supplies ltd na ujenzi upo asilimia 95 na utakamilika Oktoba 30,2022.
Msuya amesema bado kuna baadhi ya jamiii haina uelewa wa kutosha juu ya sumukuvu na madhara yatokanayo na ulaji wa chakula chenye sumukuvu . "Unakuta mahindi yanatatizo ( sumukuvu) mtu anachambua na kuwapa mifugo mfano kuku , ng'ombe,kuku akitaga mayai yake nayo yanakuwa na sumukuvu,ukimkamua ng'ombe unakunywa maziwa yenye sumukuvu.
"Nafaka ikishakuwa na sumu kuvu lazima uichome moto na uachane nayo ukiangalia mazoea tuliyonayo mtu anachanganya kidogo mahindi yenye sumukuvu na mazima anaendelea kula sasa hilo ni tatizo kuna wafanyabiashara wananuna hayo mahindi kwasababu ya bei ndogo wanaenda kuuzia watu ni kosa kubwa amesema Msuya.
Anaongeza " Tunaendelea kutoa elimu ya uelewa wa sumukuvu,ni tatizo na ina madhara ya muda mfupi na mrefu na nilazima tuiambie jamii ili ijue madhara ya muda mfupi na mrefu kama umeila kwa wingi madhara yake ni kuharisha ,kutapika na hatimaye kifo lakini mbaya zaidi ni hii sumukuvu ambayo tunaila kidogo kidogo mfano asubuhi kuna familia inaweza ikanywa uji ,mchana ugali na usiku ugali kesho na keshokutwa unakuta ni hivi hivi .
Anasema kuwa " watoto wadogo lishe kubwa ni uji kwahiyo unakuta mahindi kama yameathirika na sumukuvu au karanga ina maana unakuwa unamlisha mtoto kitu ambacho kina tatizo ( sumukuvu) endapo kama athari ya sumukuvu imeishaingia kwenye hayo mazao ndani ya miaka 20 hadi 30 ndio tunatengeneza saratani ya ini au koo na kuna tafiti nyingi zinaonesha saratani hizo zina mahusiano na sumukuvu kwahiyo ni tatizo" amesema Msuya .
Kuhusu njia za kuepuka sumukuvu Msuya amesema ni kulima kilimo bora, kutumia mbegu bora, kulima na kuvuna kwa wakati, kukausha nafaka zikiwemo mahindi na karanga kwa kutumia njia zinazoelekezwa na wataalam sambamba na kuhifadhi kitaalamu.
Mwakilishi wa katibu mkuu wizara ya kilimo Dkt Mashaka Mdangi amesema zaidi ya maafisa ugani 3000 na wananchi zaidi ya 61,000 kutoka maeneo tofauti nchini wamepata elimu juu ya kudhibiti sumukuvu huku vijana 420 wakipata elimu kuhusu ujenzi na utengenezaji wa vihenge vya chuma ambavyo vitasaidia kutunza mazao katika mazingira rafiki ambapo kuvu haiwezi kuota.
Katika hatua nyingine Dkt Mdangi amewataka waratibu wa mradi huo kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu ghala hilo ili likamilike kwa wakati.
Post a Comment