HEADER AD

HEADER AD

BASHE AAGIZA UBORESHWAJI TEKNOLOJIA YA UMWAGILIAJI



Na Annastazia Paul,Simiyu

WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya teknolojia ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima kufanya kilimo chenye tija na manufaa zaidi.

Akizungumza katika kilele cha maonesho ya siku ya chakula duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika uwanja wa halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu, waziri Bashe amesema kuwa ili kuwawezesha wakulima kukabiliana na athari za mazingira zinazoendelea kujitokeza ni lazima zifanywe jitihada ambazo zitawezesha shughuli za kilimo kuwa na tija.

“Tunakadiria kwamba ifikapo mwaka 2050, dunia itakuwa ina watu bilioni tisa, na Afrika itakuwa ina watu zaidi ya bilioni mbili, lakini uzalishaji wa chakula utapungua katika dunia na kihatarishi namba moja itakuwa ni athari za mazingira na biashara kubwa duniani ya kilimo itakuwa ni ya mazao ya chakula.

"kwahiyo niwaombe mkuu wa mkoa na viongozi wa mikoa ni lazima tuanze program ambazo zitafanya shughuli za kilimo ziwe na tija kwa wakulima, mojawapo ni suala la uhakika wa maji nayo ni njia na teknolojia za umwagiliaji", amesema Bashe.


Waziri Bashe amewataka wakulima mkoani Simiyu kujisajili katika daftari la kilimo ili watambulike waweze kunufaika na ruzuku kutoka serikalini, huku akiwataka wakuu wa wilaya na mikoa kutowapatia pembejeo wakulima wote ambao hawajasajiliwa.

“Tumeanza zoezi la kusajili wakulima, nendeni mkasajili ili serikali inapotoa ruzuku ijue inampatia ruzuku nani, anaishi wapi, ana matatizo gani, sasa hivi tunagawa mbegu za pamba, tutagawa madawa, nataka niwaombe wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa msimgawie mkulima yoyote ambaye hajasajiliwa katika daftari la kilimo ili tumjue siku ya mwisho isije ikawa dawa tunazogawa zinaishia kwenye maduka", amesema Bashe.

Waziri Bashe amesema wizara hiyo itafanya marekebisho mawili katika sekta hiyo ili kuwezesha wakulima kuzalisha kibiashara na kukomesha utapeli kwenye kilimo kwani kumekuwa na watu ambao wanafanya utapeli katika sekta ya kilimo na kwamba itatungwa sheria itakayowezesha watu hao kubanwa na kukomeshwa.

“Tunakwenda kufanya marekebisho mawili makubwa ya sheria, kwanza tutafanya marekebisho ya sheria ya mbegu ili sheria zetu za mbegu zitambue mbegu zetu za asili ziweze kuhifadhiwa, ziweze kusafishwa na ziweze kuzalishwa ili wakulima waweze kuwa nazo, ambazo tutakuwa tunazitumia kwa wakulima ili wakulima waweze kuzalisha kibiashara,” amesema Bashe.

Ameongeza“Lakini la pili tunaenda kutunga sheria mpya ya kilimo sasa hivi kumeibuka matapeli kwenye sekta ya kilimo, kwahiyo tunaenda kutunga sheria ya kilimo, kwamba mtu yoyote atakayefanya utapeli kwenye kilimo ni uhujumu uchumi kwa sababu amehujumu maisha na shughuli za mtu" amesema.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ameeleza namna ambavyo  mkoa huo umenufaika na maonesho hayo ya siku ya chakula duniani, ambapo amesema pamoja na mambo mengine wakazi wa mkoa wa Simiyu wamenufaika na elimu ya kilimo, mifugo na lishe.


“Mkoa wetu umenufaika na maonesho haya, kwanza wakulima pamoja na wavuvi wamekwenda kupata mafunzo mbalimbali, lakini pia maonesho haya wananchi wamekwenda kuhamasishwa kilimo cha kisasa ambacho pia inakwenda kuongeza tija na kupunguza tatizo la sumu kuvu kwenye mazao ya chakula.

" Lakini pia wananchi wamekumbushwa namna ya kutumia vyakula vya asili vinavyopatikana kwenye mkoa wetu ili kuimarisha lishe na kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto", amesema Nawanda.




No comments