HEADER AD

HEADER AD

UKOSEFU MAENEO YA MALISHO UNAVYOITESA MIFUGO,WAFUGAJI TARIME - 2




>>>Isemavyo Sera ya mifugo 

>>> Mtafiti aeleza umuhimu wa malisho

>>>  Ilani ya  CCM inaielekeza serikali kutatua changamoto
 
Na Dinna Maningo, Tarime

UKOSEFU wa malisho katika vijiji vilivyopo Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, ni changamoto inayowatesa wafugaji na mifugo kulazimika kutembea mwendo mrefu zaidi ya km 5 kutafuta malisho.

Baadhi ya wafugaji wanalazimika kuamka usiku kuswaga mifugo kupeleka kwenye maeneo ya watu yaliyo na malisho kulisha mifugo, mingine kuchunga kwenye makazi ya watu na mashamba yaliyo na mazao na hivyo kusababisha migogogo kati ya wafugaji na wakulima.

Hali hiyo ya ukosefu wa maeneo ya malisho Nyamongo imewalazimu baadhi ya wafugaji kuswaga mifugo kuvuka mto Mara kwenda kuchunga wilaya jirani ya Serengeti, lakini wanapofikia huko huzuiliwa kwakuwa wanatoka wilaya nyingine.

Inaelezwa kuwa usalama wa maisha ya mifugo na wafugaji unakuwa hatarini wakati wavukapo mto Mara kwenda Serengeti, baadhi ya wafugaji na mifugo huliwa na mamba, wasiojua kuogelea huzama majini na hivyo kupoteza maisha huku maeneo yanayotegemewa kwa malisho yaliyopakana na mto Mara yakijaa maji kipindi cha msimu wa mvua ambapo mto hufurika na maji kuvamia maeneo ya malisho .


                    
        Moja ya  eneo ambalo mifuga hulitumia kwa malisho Kijiji cha Matongo lililopakana na Mto Mara , msimu wa mvua maji hujaa mtoni hadi kwenye eneo hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Murito Yakobo Ryoba anasema  kitendo cha kupeleka mifugo malishoni serengeti kuna wakera wafugaji kwakuwa wanatembea umbali mrefu na huvuka mto kwa kutembea kwa miguu kwakuwa wengine hawajui kuogelea.

"Tulikuwa na eneo tengefu la malisho lakini kutokana na migogoro ya mipaka na vijiji jirani ambavyo ni Gibaso,Nyabirongo na Msege  eneo hilo likavamiwa na watu wakisema ni eneo lao na kusababisha mifugo ikose malisho, migogoro ya mipaka kwenye vijiji inaathiri mifugo inakosa malisho, mifugo inapopelekwa Serengeti inaliwa na mamba wakati ikivuka mto" anasema Yakobo.


Sera ya Taifa ya Mifugo 

Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 inaeleza kuwa sekta ya mifugo hutoa mazao mengi ya mifugo yanayotumika nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa mazao hayo kutoka nje ya nchi.Mchango wa sekta ya mifugo kwenye uchumi wa Taifa, huchangia katika kuzalisha chakula, hivyo kuchangia katika uhakika wa chakula.

Mazao mengine ni kubadilisha malisho na masalio ya mazao kuwa chakula, chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi wa vijijini, kutoa ngozi za mazao mengine, na kutoa mbolea na wanyama kazi kwa ajili ya kilimo endelevu na kuchangia katika majukumu ya kijadi kwenye jamii.

Sera hiyo inaeleza kuwa,vikwazo vinavyokabili maendeleo katika sekta ya mifugo ni tatizo kubwa katika mfumo wa umilikaji wa ardhi,rasilimali za maji na malisho ni kutokuwa na utaratibu wa kutenga na kumilikisha ardhi kulingana na taratibu za sheria au kimila.

Matatizo mengine ni kupanuka kwa shughuli za kilimo katika maeneo yaliyokuwa yanatumika kwa kufuga na kichungia,kupanuliwa kwa mbuga za Wanyamapori na kuhamahama kwa wafugaji kunakozuia kuendelezwa kwa maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2017 wakati wa zoezi la kupiga chapa mifugo Halmashauri ya wilaya ya Tarime inakadiliwa kuwa na zaidi ya Mifugo 606,892, ambapo ng'ombe wa asili ni 148,278,ng'ombe wa maziwa 2,402,mbuzi asili 173,746,mbuzi wa maziwa 207.

Mifugo mingine ni Kondoo 34,558,kuku wa kienyeji 182,780,kuku wa kisasa 8,970, bata 20,431, punda 1,197,mbwa 26,715, paka 7,104 na nguruwe 504.

Afisa Mifugo wa Halmashauri azungumza

Afisa Mifugo Halmshauri ya wilaya ya Tarime Joseph Marwa anasema tatizo linalochangia kuwepo kwa ukosefu/uhaba wa malisho ni ukame hasa msimu wa kiangazi mwezi wa 6-8,japo anasema ukame sio kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine nje ya Tarime yaliyo na changamoto kubwa ya ukame.





"Kijiji cha Surubu wao walitenga eneo la malisho, sehemu nyingine imekuwa vigumu kutenga maeneo ukitenga mtu anaona umekata eneo lake na vijiji vingine havina ardhi za kutenga maeneo ya malisho.Tarime hakuna migogoro ya wakulima na wafugaji kwasababu mtu ni mfugaji huyohuyo ni mkulima"anasema Joseph.

Mtafiti wa Mifugo aeleza umuhimu wa malisho

Patrick Rukiko ni Mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Ziwa kituo cha Mabuki kilichopo wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza anasema Tanzania inakadiliwa kuwa na idadi ya watu wapatao 58,458,191 (UN,2019),asilimia 70  (40,920,733) wanajishughulisha na kilimo na ufugaji.

Anasema Tanzania ni nchi ya tatu kuwa na mifugo wengi barani Afrika = 30.5 milioni (Tanzania Livestock master plan,2018),inachangia kutoa ajira na usalama wa chakula,wanyama hutumika katika shughuli za kijamii.

Patrick anasema uzalishaji wa wanyama umekuwa ni mdogo kutokana na changamoto mbalimbali katika uzalishaji mifugo unaochangiwa na ukosefu/uhaba wa malisho,hupatikana kwa vipindi,ubora mdogo ambapo upatikanaji ni asilimia 26 ya mahitaji yote.


Patrick anasema kuwa malisho ni chakula kikuu cha wanyama wanaocheua wakiwemo, mbuzi, kondoo na wanyama wa porini wenye sifa kama hiyo,malisho huchukua zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji yote ya chakula.

"Malisho huchukua asilimia 70 ya gharama zote za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, ni chanzo cha mapato kwa wauzaji na wazalishaji na hutunza ardhi/kuzuia mmomonyoko.

Mtafiti huyo anasema kama hakuna malisho bora kwa wanyama, uzalishaji utapungua, mifugo na bidhaa zake bei kuongezeka, pato la mwananchi na Taifa kushuka,vifo, ukosefu wa bidhaa bora, kupotea kwa ajira, migogoro ya wafugaji na wakulima.

Hotuba ya Wizara na ongezeko la Mifugo

Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki iliyopo katika Tovuti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi aliyoisoma Bungeni Dodoma Mei, 2022 kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka wa 2022/2023 imeeleza;

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 idadi ya mifugo imeongezeka ambapo ng'ombe wameongezeka kutoka milioni 33.9 hadi milioni 35.3,mbuzi kutoka milioni 24.5 hadi milioni 25.6,kondoo kutoka milioni 8.5 hadi milioni 8.8,kuku milioni 87.7 hadi milioni 92.8 ambapo kuku wa asili wameongezeka kutoka milioni 40.4 hadi milioni 42.7 na kuku wa kisasa wameongezeka kutoka milioni 47.3 Hadi milioni  50.1, nguruwe kutoka milioni 3.2 hadi milioni 3.4 (Ofisi ya Taifa ya Takwimu).


Sekta ya Mifugo katika mwaka 2021 ilikua kwa kiwango cha asilimia 5.0 sawa na mwaka 2020 mchango wake katika pato la taifa ulikuwa asilimia 7.0 sawa na mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Hotuba hiyo katika mwaka 2021/2022 Wizara imepima na kuweka alama zinazonekana katika shamba la Muhukulu -Songea lenye ukubwa wa Hekta 3,200 ambapo vitalu 10 vya malisho vimetengwa.

Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya ardhi ilitenga jumla ya Hekta 128,894.68 katika vijiji vya Mikoa ya Pwani,Dodoma,Iringa,Mbeya,Kigoma,Njombe,Rukwa,Kilimajaro,Singida,Ruvuma, na Lindi na kuwezesha maeneo ya malisho kufikia Hekta 3,189,456.94 kutoka 3,060,562.27 mwaka 2020/2021.

Maeneo 22 ya malisho yenye jumla ya Hekta 143,754.02 yaliyotengwa katika mkoa wa Arusha na Manyara yamesajiliwa.


           Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki

Pia Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2024 kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa imepanga kutenga maeneo ya malisho yenye ukubwa wa Hekta 1,000,000.

Maelekezo ya Ilani ya CCM kwa Serikali

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM ) 2020-2025, Ibara ya 38 inaeleza kuwa sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi,kutokana na umuhimu huo ni dhahiri kuwa ipo haja kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani,ikiwemo ya lishe bora,na usafirishaji nje ya nchi.
 
Ilani inaeleza mafanikio yaliyopatikana katika ilani ya uchaguzi ya 2015-2020 katika sekta ya ufugaji ni pamoja na kuongezwa kwa maeneo ya ufugaji kutoka Hekta milioni 1.4 mwaka 2015 hadi  Hekta milioni 5.0 mwaka 2020, hadi 2020 vijiji 1,852 vimeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini ambapo maeneo ya malisho Hekta 2,788,901.17 yametengwa kwa ajili ya ufugaji katika mikoa 22.

Ibara ya 40 ya Ilani hiyo katika kipindi cha miaka mitano CCM itaielekeza Serikali kuendelea kuleta mabadiliko makubwa na ya kisayansi katika ufugaji kwa kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga,tiba na utafiti wa mifugo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi hasa kwa vijana na kuinua mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.


          Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akiwa na Ilani ya Uchaguzi

Serikali itatakiwa kushughulikia kwa nguvu zaidi migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili kufikia azma hiyo,CCM itaielekeza Serikali kujikita katika kuboresha maeneo ya kimatokeo,ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mashamba darasa na mashamba ya mfano ya malisho katika vijiji, halmashauri za wilaya na miji nchini. 

Kuimarisha utambuzi na usajili wa mifugo nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafugaji na mifugo yao,kurekebisha maeneo ya wafugaji kwa kuyapatia huduma muhimu.

Huduma hizo ni maji,afya na elimu kwa ajili ya kusaidia jamii kutulia sehemu moja na hivyo kuepuka kuhamahama kufuata huduma hizo na kuimarisha huduma za maji,malisho na vyakula  vya mifugo ikiwa ni pamoja na kubaini na kutenga maeneo ya ufugaji kwa kuyatambua,kuyapima,kuyasajili na kuyamilikisha ili kuongeza maeneo yaliyotengwa kutoka Hekta 2,788,901.17 hadi Hekta 6,000,000.





No comments