HEADER AD

HEADER AD

MKE WA MENEJA TARURA AUAWA KWA KUKATWAKATWA MAPANGA SERENGETI


>>Watenda tukio waliingia ndani ya nyumba yake wakamkatakata sehemu mbalimbali za mwili, kiganja cha mkono chakutwa chini

>> Vilio vyatawala

Na DIMA Online, Serengeti 

VILIO , simanzi vimetawala baada ya mwanamke Rhoda Jonathani mwenye umri wa miaka 44, mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoa wa Mara , kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Marehemu alikuwa ni mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) mkoa wa Kagera , Mhandisi Wilson Charles ambaye wamefanikiwa kupata watoto watatu ,kati yao wa kike wawili na mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba ambaye ni mlemavu wa viungo.

              Nyumbani kwa marehemu Rhoda Jonathani

Tukio hilo limeelezwa kutokea siku ya alhamisi, tarehe ,23, Oktoba, 2025 majira ya kati ya saa moja na saa mbili usiku nyumbani kwa marehemu.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia mwili wa marehemu, wamesema marehemu alikutwa amekatwa kiganja cha mkono wa kulia kilichokutwa chini ya sakafu huku mwili ukiwa chini pembeni ya kitanda ukiwa na majeraha makubwa kifuani, mkononi, mdomoni na kwenye matiti.

         Roda Jonathan aliyeuwawa kwa kukatwakatwa mapanga wilayani Serengeti.

Mashuhuda wasimulia

Jana Oktoba, 25, 2025 DIMA Online imefika hadi nyumbani kwa marehemu Kitongoji cha Burunga na kuzungumza na mashuhuda ambapo iliwakuta wananchi, ndugu wakiwa katika majonzi wakiwemo waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato alikokuwa akisali marehemu.

Mophati Mwita anayeishi nyumbani kwa marehemu amesema" Ilikuwa siku ya alhamis nilikuwa jikoni napika mida ya saa moja usiku nilimuomba Musa Marwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Serengeti aliyepanga hapa nyumbani akawashe taa ya nje.
       Mophati Mwita anayeishi nyumbani kwa marehemu

" Alipofika pale uwani alimuona mtu ameingia ndani mwanaume akajiuliza mbona geti limefungwa amepitia wapi ?kumbe aliruka ukutani. Yule mtu akamwambia mbona nagonga geti hufungui ?

" Yule mtu akauliza mama yupo ?wakati anauliza shangazi alikuwa ndani anaongea na simu , wakati yule mtu anaongea na mwanafunzi ghafla akafika mwanaume mwingine, aliposikia sauti ya shangazi akiongea na simu akaingia moja kwa moja hadi chumbani alikokuwa shangazi.

" Yule mwanafunzi akatoka mbio kwenda hadi shuleni kumtaarifu mwalimu mkuu kuwa kuna mtu kavamia nyumbani, shangazi alipiga kelele sikuwa na la kufanya kwasababu mimi ni mdogo na nyumbani tulikuwa mimi, shangazi na mwanae ambaye ni mlemavu pamoja na huyo mwanafunzi" amesema Mophati.

Mophati ameongeza kusema kwamba, baada ya mtu huyo kufanya kitendo cha kikatili aliondoka akiwa na mwenzake na kwamba walifanikiwa kuona sura zao ambazo hawakuzitambua wala kujua majina yao.

" Baada ya tukio lile mkuu wa shule ya sekondari Serengeti  aliwasiliana na viongozi wa serikali , Mwenyekiti wa Kitongoji alifika na Polisi walifika wakamchukua shangazi na kuondoka nae.

" Nakumbuka siku moja kabla shangazi hajauawa kuna watu walikuja nyumbani usiku wakauliza mama yako yupo ?nikasema hayupo, alikuwa ameenda Nyamongo kwenye arusi , kesho yake nilimpigia simu shangazi nikamwambia kuna watu walikuja kukuulizia, akasema atakuja , kesho yake alipokuja ndipo hao watu wakaja tena wakamuua" amesema Mophati.

Elizabeth Kambarage ni jirani wa marehemu , mwenye umri wa miaka 49 anasimulia " Mwenyekiti wa mtaa alinipigia simu ilikuwa saa mbili usiku akasema toka ndani kuna tatizo nikamuuliza tatizo gani ?akasema wewe njoo hapa kwa Mama Agata .

        Elizabeth Kambarage ni jirani wa marehemu

" Nilipofika ndani nikaona kiganja cha mkono kipo chini ila sikuona mtu nikatazama huku na kule nikaona mwili wa mama Agata upo pembeni ya kitanda chini. Sikutaka kuutazama sana maana ulikuwa unatisha amekatwakatwa sana .

" Inaumiza sana wamemuua mama Agata wakati mama wa watu alikuwa mtu mwema rafiki wa watu, hatukuwahi kusikia ana ugomvi na jirani yoyote, alikuwa na ushirikiano sana na jamii inayomzunguka.

" Ameacha mtoto mlemavu ambaye hatembei wala hazungumzi aliyekuwa akimlea kwa uangalizi mkubwa , amekufa nani atamleta yule mtoto inaumiza sana " amesema Elizabeth.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga , James Makuru Marwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa alipigiwa simu na alipofika alikuta Roda ameshapoteza maisha .

         Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege, James Makuru Marwa.

" Tukio lilitokea tarehe 23 mwezi huu majira ya saa 2 usiku . Nilipigiwa simu na mkuu wa shule ya sekondari Serengeti kuwa nyumbani kwa Injinia Wilson kumetokea mauaji .

" Nilipofika sikukuta mtu yeyote ilibidi nimpigie simu tena mkuu wa shule ,mkuu alifika akiwa na mwanafunzi aliyekwenda kumpatia taarifa , kijana akafungua geti la kwanza na geti la pili tukaingia ndani.

" Tulipoingia chumbani kwa harakahara sikuona chochote zaidi ya kuona mkono ukiwa chini, ilibidi nichukue tochi na kumulika kila sehemu ndipo nikauona huo mwili pembeni ya kitanda.

Mwenyekiti huyo amesema alichukua jukumu la kupiga simu Polisi na wakafika kwenye eneo la tukio wakaukagua mwili na kuubeba na kupeleka chumba cha kuhifadhi maiti hospitali ya wilaya ya Serengeti.

" Polisi waliwachukua maelezo wale watoto waliokuwa nyumbani. Kesho yake kuna mtu akiwa anapita barabarani akaona panga ikiwa na damu imetupwa pembeni ya barabara jirani na kulikotokea tukio .

" Nilipiga simu Polisi wakasema mtu asiguse hilo panga wakaja wakalichukua. Kwakweli kitendo hiki ni cha kinyama hakijawahi kutokea kwenye kata yetu ndio tukio la kwanza ambalo limetokea " amesema Mwenyekiti.



 
........Itaendelea


No comments