WAMUOMBA RAIS SAMIA, SERIKALI YA MARA KUWASAKA NA KUWAWAJIBISHA WALIOMUUA MKE WA MENEJA TARURA
Na DIMA Online, Serengeti
WAKAZI wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, ndugu, wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu pamoja na Serikali ya Mara, kuwasaka na kuwawajibisha waliomuua Rhoda Jonathan kwa kukatwakatwa mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Marehemu alikuwa mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) mkoa wa Kagera , Mhandisi Wilson Charles ambaye wamefanikiwa kupata watoto watatu ,kati yao wa kike wawili na mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba ambaye ni mlemavu wa viungo.
Tukio hilo la mauaji limeelezwa kutokea siku ya alhamisi, tarehe ,23, Oktoba, 2025 majira ya kati ya saa moja na saa mbili usiku nyumbani kwa marehemu na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Serengeti.
Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia mwili wa marehemu, wamesema marehemu alikutwa amekatwa kiganja cha mkono wa kulia kilichokutwa chini ya sakafu huku mwili ukiwa chini pembeni ya kitanda ukiwa na majeraha makubwa kifuani, mkononi, mdomoni na kwenye matiti .
Wakizungumza na DIMA Online wananchi wamesema kwamba vitendo vya ukatili vinatakiwa kupigwa vita kwani visipodhibitiwa vitaendelea kushamiri na huku wakimuomba Rais Samia kuingilia kati mauaji ya mwanamke mwenzake ili haki itendeke.
Jirani mwingine amesema " Nalaani vitendo vya ukatili kama hivi . Mama Agata alikuwa mkarimu sana ulikuwa na shida ukimwendea anakusaidia , ukiwa na sherehe ukimwomba mahotipoti anakupatia , sidhani kama alikuwa na ugomvi na mtu" anasema jirani.
Joyce Maiko anaishi jirani na marehemu amesema kwamba Rhoda hakuwahi kuwa na ugomvi na mtu yeyote kwenye kitongoji hivyo wanashangaa kitendo kilichofanyika cha kikatili dhidi yake.
" Rhoda hajawahi kuwa na ugomvi na jirani yeyote wala mtu yeyote. Tunamuomba Rais Samia mwanamke mwenzetu aingilie kati ili Rhoda apate haki yake hata kama ameshakufa.
" Naiamini serikali yetu haishindwagi jambo ikiliamria, ina mbinu nyingi za kiuchunguzi , hata kama uliua watu wasikutambue serikali itakutambua kwa njia zake zote.
" Tunaiomba serikali yetu ya mkoa wa Mara ichukue hatua ifanye upelelezi wa kina kuwabaini wahusika wasifumbiwe macho wachukiliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho ,tuwajue ni akina nani waliohusika" amesema Joyce.
Petro Mrimi amesema" Sijawahi kuona tukio kama hili hapa kwenye Kata yetu , tangu hili tukio limetokea hatuna amani kabisa hapa kwenye kitongoji chetu. Tunaiomba serikali yetu ichukue hatua kukabiliana na wahalifu waliotoa maisha ya Rhoda ili tuishi kwa amani.
" Ni tukio la kwanza kutokea hapa Kitongojini lisipodhibitiwa wahusika wakachukuliwa hatua yanaweza kujitokeza matukio mengine kama hili watu wakaendelea kupoteza maisha.
" Tunaiomba sana serikali iingilie kati marehemu ameacha watoto watatu na mmoja ni mlemavu wa viungo ambaye alikuwa analelewa na mama yake " amesema Petro.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga , James Makuru Marwa amesema kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi lakini pia wao kama wanakitongoji wanaendelea kufanya upelelezi ili kubaini waliohusika na tukio hilo .
Ameliomba Jeshi la Polisi kuongeza nguvu ili wahusika watiwe hatiani " Mimi ni mkazi wa Kitongoji cha Burunga kwa miaka zaidi ya 20 sijawahi kusikia wala kupata malalamiko kama Mwenyekiti kwamba Rhoda ama mama Agata anadaiwa na mtu ama ana ugomvi na mtu .
" Rhoda alikuwa ni Katibu wa Maafa, alijitoa sana, kuna shule ya Chekechea inayojengwa na wananchi Rhoda ameshiriki vizuri mpaka darasa limejengwa.
"Tunajiuliza mara mbilimbili waliomuua Rhoda walikuwa na nia gani ? maana waliomuua hawakuchukua kitu chochote. Panga walilotumia kumkata lilikuwa kali mno lilikuwa jipya na lilikuwa limenolewa " amesema Mwenyekiti.
Mwenyekiti ameongeza " Najiuliza wale watu waliwezaje kuingia mle ndani na kufanikiwa kutoka ndani ? Maana ile nyumba ina kona kona mimi niliingia chumbani lakini wakati wa kutoka nilishindwa pakutokea kufika nje, ikabidi niombe msaada wa kuongozwa nitoke ndani kwenda nje" amesema Mwenyekiti.
Mama wa Marehemu aiangukia Serikali
Ester Jonathan Mobe mkazi wa Kijiji cha Nyangoto -Nyamongo ,wilayani Tarime ni mama mzazi wa marehemu ameiomba serikali kumsaidia ili haki ipatikane kwa mwanae kutokana na tukio la kinyama alilotendewa mwanae.
Ester Jonathan Mobe mkazi wa Nyamongo , ni mama mzazi wa Rhoda Jonathan aliyeuawa kwa kukatwakatwa mapanga nyumbani kwake wilayani Serengeti.
" Ni nani aliyemuua mwanangu ? Je alimwibia nini ? si angeniambia mimi ningewaomba msaada wanyamongo wanichangie pesa nimlipe? kwanini aniulie mwanangu" Ester amesema huku akibubujikwa machozi.
Ester amesema kwamba amejaribu kufuatilia kufahamu labda mwanae alikuwa anadai madeni na hivyo kupelekea kifo chake lakini amebaini hakuna mtu anayemdai deni lolote mwanae.
" Rais Samia nisaidie kujua nani ameniulia mtoto wangu , nisaidie kumwajibisha , Rais Samia mtoto wangu ameacha mtoto mdogo mwenye ulemavu asiyeweza kuzungumza wala kutembea.
" Hata chakula analishwa na mama yake ndo alikuwa akimsaidia , ndiye aliyekuwa akimpeleka kliniki Bugando kwenye matibabu ,sasa mwanangu kafa nani atampeleka mjukuu wangu hospitali ? nani atazoa kinyesi chake maana ana miaka 7 na hana uwezo wa kujihudumia.
" Mama Samia huwa nakuona kwenye TV unasaidia watu , mtoto wa mwenzio ni wako , wewe ni mwanamke kama mimi unaujua uchungu wa kuzaa nisaidie aliyefanya kitendo hiki awajibishwe maana amekatisha maisha ya mwanangu ,Serikali nisaidieni " amehimiza.
DIMA Online inaendelea kumtafuta Mkuu wa wilaya ya Serengeti, pamoja na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara kufahamu hatua zilizochukuliwa baada ya tukio hilo la kikatili .







Post a Comment