SABABU ZA UKOSEFU WA MAENEO YA MALISHO ZATAJWA
Na Dinna Maningo,Tarime
UKOSEFU wa maeneo ya malisho ya mifugo ni tatizo linalozidi kuongezeka siku hadi siku katika vijiji mbalimbali hapa nchini jambo ambalo limekuwa likivunja mahusiano mazuri baina ya wafugaji, wakulima na Hifadhi za Taifa na kusababisha kuibuka migogoro.
Migogoro hiyo hutokea wakati mifugo inapoingia kwenye mashamba, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwenye makazi ya watu kwa lengo la kujipatia chakula ,ambapo baadhi ya mifugo hufanya uharibifu wa mimea yakiwemo mashamba ya wakulima yenye mazao na pindi mifugo inapoingia ndani ya hifadhi.
Vijiji vilivyopo Nyamongo kikiwemo kijiji cha Matongo, Kerende, Murito na Nyabichune pamoja na vijiji Nane vilivyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambavyo ni Kijiji cha Kenyamsabi, Masanga, Masurura, Karakatonga, Gibaso,Nyabirongo, Nyandage na Kegonga Wilayani Tarime Mkoa wa Mara, vinakabiliwa na ukosefu /uhaba wa maeneo ya malisho.
Ukosefu wa maeneo ya malisho umesababisha baadhi ya wafugaji kuamka usiku kuswaga mifugo kwenda kutafuta malisho, wengine kutembea umbali mrefu zaidi ya km 5 kwenda kusaka malisho na mifugo mingine kuliwa na mamba wakati ikivuka mto Mara kwenda wilaya ya Serengeti kutafuta malisho.
Je nini sababu ya kutokuwepo maeneo ya malisho ya mifugo ? Nini kifanyike ili kupunguza tatizo la ukosefu wa malisho ? DIMA Online imezungumza na baadhi ya wafugaji nao wamesema haya ;
Sababu za ukosefu maeneo ya malisho
Mkazi wa kijiji cha Kerende Chacha Marwa anasema vijiji vilivyopo Nyamongo havina maeneo yakutosha kwa ajili ya malisho kwakuwa baadhi ya maeneo yanatumika kwa shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Anasema maeneo mengine yamechukuliwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ambao uliwahamisha baadhi ya wananchi kutoka kwenye maeneo yao ili kupisha shughuli za mgodi na kwenda kuishi kwenye maeneo ambayo awali yalitumika kuchungia mifugo hali ambayo imechangia kuwepo kwa uhaba wa ardhi yenye malisho.
Mwanaid Ally mkazi wa kijiji cha Kerende mwenye ng'ombe 26 anasema awali mifugo ilikuwa ikichunga maeneo ya mto Mara lakini eneo hilo limechukuliwa na Serikali na kupanda miti.
"Tunahangaika sana tulikuwa tunalisha mifugo kando ya mto Mara, Serikali imechukua eneo lote wameweka bikoni kwenye mashamba tuliyokuwa tumelima na kuchungia mifugo tunateseka sana.
"Kwa sasa tunachunga mifugo maeneo jirani na mlima lakini ukipeleka ng'ombe wako unaambiwa toa hili ni eneo langu unakosa pakuchungia, kijiji hakina eneo la malisho, watu wamejimilikisha kila eneo hata kwenye milima tofauti na zamani tulichunga kokote kasoro maeneo ya mashamba," anasema Mwanaidi.
Ghati John mkazi wa Kijiji cha Matongo anasema kipindi cha mvua mto hufurika na maji kuingia kwenye maeneo wanayotumia kuchunga mifugo na kusababisha kukosekana maeneo ya malisho.
" Baadhi ya wafugaji tumepakana na Mto Mara ukijaa unamwaga maji kwenye mashamba na maeneo tunayochungia mifugo inakosa nyasi "anasema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kerende Mniko Magabe anasema maeneo yamepungua kwasababu ya kuongezeka idadi ya watu inayosababisha watu kuyatumia maeneo kuishi na kulima mazao.
"Miaka ya nyuma iliyopita kijiji kilikuwa na wananchi wapatao 3,000 sasa idadi watu yapata kuwa 9200, kuna eneo hapa la mlimani angalau linatusaidia tunachunga mifugo lakini hakuna maji, ng'ombe akila nyasi anataka na maji.
"Kuna mlima kulikuwa kuna majani mazuri malaini tunaita kwa kikurya (Urunyeru) watu walikuwa wanapita kwenda kulisha mifugo, lakini ongezeko la makazi likasababisha watu kuziba njia, watu wamejenga miji imeongezeka, mashamba na uchimbaji wa dhahabu pamebanana ng'ombe hawapiti tena," anasema Mniko.
Anasema kuwa kadri siku zinavyoendelea maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu yanaongezeka na kusababisha kupungua kwa maeneo ya malisho jambo ambalo limesababisha baadhi ya watu kuacha ufugaji kutokana na changamoto ya maeneo ya malisho.
"Siku hizi ng'ombe wachache zamani miaka ya 1980 wafugaji walimiliki ng'ombe wengi,mzee Matiko Mwita alikuwa na ng'ombe zaidi ya 2,000,watu walioa kwa ng'ombe 40-60 kama ng'ombe alikuwa na kindama hiyo ndama haihesabiki kwahiyo ulijikuta unatoa ng'ombe 60 ukiongeza na ndama unakuta umetoa ng'ombe 90, siku hizi mtu anaolewa kwa ng'ombe 5 tena vindama kwa sababu ng'ombe hazipo.
" Unamwambia mfugaji afuge kisasa wakati ufugaji huo una gharama kubwa zaidi ya ng'ombe ulionao, elimu ya ufugaji bora ni nzuri endapo wataalamu wakiwafikia wafugaji kuwapa elimu, ufugaji una changamoto nyingi lakini nikama serikali haijatilia mkazo katika kutatua changamoto za wafugaji na mifugo yao,"anasema Mniko.
Ghati Chacha anasema," miaka ya nyuma ng'ombe alikuwa akimaliza mwaka anabeba mimba anazaa lakini kwa sasa anaweza kukaa miaka mitatu bila kuzaa ni kwasababu ya ukosefu wa malisho ambayo yangemwezesha afya yake kuimalika," anasema Ghati.
Marwa Matiko anasema uhaba wa maeneo ya malisho umesababisha mifugo kula mazao kwenye mashamba ya watu na kusababisha migogoro baina ya wafugaji na wakulima na kusababisha chuki dhidi yao lakini pia mifugo kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga inapokutwa kwenye mashamba ya watu.
" Shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo zimeongezeka na kusababisha maeneo ya malisho kukosekana, Serikali bado haijaipa kipaumbele mifugo ya kufugwa ni maeneo machache yaliyotengwa maeneo ya malisho ndiyo maana bado changamoto ya malisho ni kubwa," anasema Marwa.
John Mkira ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru kata ya Nyarokoba anasema wafugaji wanaopakana na Hifadhi ya Serengeti wanapata changamoto kubwa ya ukosefu wa maeneo ya malisho ya mifugo na hivyo kujikuta wakiingia mikononi mwa sheria ambapo chanzo kikubwa ni ukosefu wameneo ya malisho ya mifugo.
John anaiomba Serikali kuwamegea sehemu ya eneo la hifadhi kuwapatia wafugaji ili wachunge mifugo yao na kwamba kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza migogoro kati ya hifadhi na vijiji kwakuwa mifugo itakuwa imepata eneo la malisho, na kwamba endapo wafugaji hawatatengewa maeneo ya malisho migogoro ya vijiji na hifadhi haitakwisha.
John Marwa mkazi wa kijiji cha Nyabichune anasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yamechangia kupungua kwa malisho hasa kipindi cha kiangazi.
"Mvua isiponyesha inachangia malisho kukosekana na kupungua kwa maziwa, kiangazi kikizidi nyasi zinakauka zinakosa wanyama wanakosa chakula wanakonda na kuwa na afya mbaya akidhoofu hata nyama yake inakuwa siyo nzuri," anasema John.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanungu Waryoba Mwita anasema wananchi wanategemea kilimo na ufugaji ili walime shamba wanatumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe na kwamba katika kijiji hicho kuna eneo moja pekee la mlimani linalotumika kwa malisho.
" Hakuna eneo lingine zaidi ya mlimani tumepakana na Kenya, tulikuwa tunachunga kwenye maeneo ya Wakenya nao wanayatumia kulima mazao. Novemba,19,2021 Mwenyekiti mwenzangu wa kijiji jirani alikamatiwa mifugo yake ikichunga kwenye eneo la Ushoroba na askari wanyamapori. Hayati John Magufuli wakati wa uhai wake alisema tuendelee kutumia eneo hilo wakati huo serikali ikiendelea na mchakato wa utatuzi.
Anaongeza , " Hadi sasa serikali haijatatua kuhakikisha tunapata maeneo ya malisho mbona mikoa mingine vijiji vimepewa ardhi ambayo ilikuwa ya hifadhi lakini Tarime hakuna, ukienda kufuatilia mifugo unakamatwa unapelekwa mahakamani na unataifishiwa mifugo yako, watu wameogopa kufuata mifugo hifadhini maana wakifika watakamatwa, mifugo inakosa chakula ikifa wanaitupa," anasema Warioba.
Warioba anaiomba Serikali kutenga eneo la malisho kwakuwa vijiji vilivyopakana na hifadhi havina maeneo ya malisho na vimepakana na vijiji vya Kenya eneo la Trans Mara, eneo la Ang'ata watu wa kabila la Wakarengina (Kipsisi) na kwamba mifugo ndiyo kila kitu katika kukuza kipato cha mwananchi wa kijijini.
Daniel Charles mkazi wa Kijiji cha Matongo anasema Kijiji hicho kinategemewa kwa mazao ya chakula kwakuwa wakazi wengi ni wakulima jambo ambalo limechangia kukosekana maeneo ya malisho.
Anashauri kuwa ni vyema Serikali ikatenga maeneo rasmi kwa ajili ya malisho ili kuepusha changamoto za malisho na inapotenga iweke alama za mipaka ili kupunguza uvamizi wa maeneo ya malisho.
Ghati Marwa anasema kwakuwa maeneo yamepungua na watu wameongezeka ni vyema wafugaji wakapewa elimu ya kufuga mifugo michache itakayokidhi maeneo yaliyopo ya malisho kuliko kuwa na mifugo mingi ambayo inawapa changamoto ya malisho na hivyo kujikuta wakiingia kwenye migogoro na wakulima na hifadhi.
Patrick Rukiko ni Mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Ziwa kituo cha Mabuki kilichopo wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza, anasema uzalishaji wa wanyama umekuwa ni mdogo, kama hakuna malisho bora kwa wanyama, uzalishaji utapungua, mifugo na bidhaa zake bei kuongezeka,pato la mwananchi na Taifa kushuka, vifo, ukosefu wa bidhaa bora, kupotea kwa ajira, migogoro ya wafugaji na wakulima.
Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 inaeleza kuwa vikwazo vinavyokabili maendeleo katika sekta ya mifugo ni tatizo kubwa katika mfumo wa umilikaji wa ardhi, rasilimali za maji na malisho ni kutokuwa na utaratibu wa kutenga na kumilikisha ardhi kulingana na taratibu za sheria au kimila.
Matatizo mengine ni kupanuka kwa shughuli za kilimo katika maeneo yaliyokuwa yanatumika kwa kufuga na kichungia, kupanuliwa kwa maeneo ya mbuga za Wanyamapori na kuhamahama kwa wafugaji kunakozuia kuendelezwa kwa maeneo hayo.
Post a Comment