TRA : KUNA WAFANYABIASHARA WANA MASHINE ZA EFD LAKINI HAWATOI RISITI
Na Kareny Masasy, Kahama
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kodi Kahama imewataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2022 .
Akitoa elimu ya mlipa kodi kwa wafanyabiashara katika Halmashauri ya Ushetu mkoa wa Shinyanga Oktoba,28,2022, Msimamizi wa Kodi kutoka Kanda ya Ziwa Morgan Isdory amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wana mashine za risiti za kielektroniki (EFD) lakini hawatoi risiti.
Morgan amesema wapo wengine wanatoa bei pungufu kwenye bidhaa tofauti na uhalisia kitendo ambacho ni kosa na kifungo chake ni miaka mitatu jela au kulipa faini Milioni tatu.
"Nchi zilizoendelea ukwepaji wa kodi ni kosa la jinai ndiyo maana hapa Tanzania mara kwa mara kumekuwepo maboresho ya kanuni na sheria "amesema Morgan.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2022 inaeleza kodi itatozwa kwenye faida kwa mfanyabiashara awe na uwezo wa kutunza kumbukumbu.
“Uzingatiaji wa kifungu cha 35 cha sheria ya usimamizi wa kodi na utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu kwa mfanyabiashara, mfanyabiashara asiye na kumbukumbu makadirio yanaweza kuwa sahihi au yasiwe sahihi kwake" amesema Morgan.
Amesema kanuni za kodi zinaeleza gharama ya usafirishaji haitakiwi kuzidi kodi anayotakiwa kulipa mfanyabiashara.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhulia elimu hiyo Msabaha Issa na Ramadhani Ngau wamesema kodi zimekuwa nyingi kwa mfanyabiashara nakuomba zingine zipunguzwe ili wapate faida.
Post a Comment