VIONGOZI, WANANCHI KWANGWA KUWASHUGHULIKIA WAHALIFU
Na Jovina Massano, Musoma
WANANCHI na Viongozi wa Kata ya Kwangwa katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamejipanga kuwashughulikia wahalifu (Vibaka) wanaopora, kuiba mali na kujeruhi watu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya soko la Kwangwa wakujadili suala la ulinzi na usalama, mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Kiara "B" Akisa Magesa maarufu kwa jina la Komesha amesema hali ya usalama kwa wakazi wa kata hiyo si shwari kwakuwa baadhi ya vijana huvamia na kuingia ndani ya nyumba za watu na kuwajeruhi kwa kuwakata mapanga.
Amesema vijana hao wamekuwa wakiiba Kuku, Bata na mali zinginezo kwakuwa baadhi yao wanalandalanda mitaani hawana shughuli za kufanya.
Akisa Magesa maarufu kwa jina la komesha
"Kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi kunasaidia kuwadhibiti na kufanya wizi kupungua, matukio ya kuvamiwa kupungua tumeazimia kuhakikisha hali inakuwa salama kwa wananchi na kila kijana anashiriki kikamilifu kwenye ulinzi kama tulivyokubaliana katika mkutano,"amesema Akisa.
Polisi Kata Lucy Mbaga amesema wameanzisha ulinzi shirikishi baada ya kuwepo matukio ya uharifu ambapo viongozi wa kata na mitaa na wananchi wameazimia kila Kaya itashiriki kwa kuchangia kiasi cha Tsh 1000 kwa ajili ya vifaa vya ulinzi na malipo ya walinzi.
Polisi Kata Lucy Mbaga
"Baada ya kuanza zoezi hili la ulinzi shirikishi uharifu umeanza kupungua, matukio yalikuwa yanaongezeka na kusababisha usalama wa wananchi kuwa hatarini.
Ameongeza kuwa Kata imeweka utaratibu wa ukusanyaji fedha hizo ambapo wajumbe wa serikali za mitaa watakuwa wanakusanya fedha kwa utaratibu uliowekwa na viongozi wa Kata lakini pia wamiliki wa vileo wametakiwa kufunga mapema ili kuepuka kufanyiwa uharifu.
Pia Viongozi wa Dini na Waumini wanaofanya ibada za usiku kutopiga miziki kwa sauti ya juu nyakati za usiku kwakuwa itasaidia kusikika kwa mtu anapokuwa anahitaji msaada pindi anapovamiwa na vibaka huku wamiliki wa vilabu vya pombe wakisisitizwa kufunga mapema katika maeneo hayo.
Diwani wa Kata hiyo Fredrick Mganga kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amewataka wenye nyumba za kupangisha kuhakikisha wateja wao wanajitambulisha kwenye uongozi wa mtaa ili kuwatambua na shughuli wanazofanya.
Diwani wa Kata ya Kwangwa Fredrick Mganga
" Nawakumbusha wenye nyumba za kupangisha kuwatambulisha wapangaji wao kwa wenyeviti wa maeneo yao ili kusaidia kupunguza uharifu kwa wananchi, unaweza ukampangisha mtu kumbe ni mwizi anasubiria nyakati za usiku avamie wananchi wetu, tutaandaa mkakati kama Kata kushughulikia hilo", amesema.
Nyagai Nkunyu mkazi wa Kwangwa "A" amewashukuru viongozi wa kata hiyo kuwashirikisha katika suala la ulinzi shirikishi kutokana na hali kubadilika baada ya maeneo mengi kuwa na vibaka, wizi umeongezeka watu hawalali jambo ambalo limepelekea viongozi kuitisha mkutano na kuelezea hali halisi na tumeamua kuanzisha ulinzi shirikishi katika kata.
Bwiso Julius Mtendaji wa Kata akizungumza
Post a Comment