HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU NA ZAECA WATAKIWA KUJITATHMINI

 


Na Alodia Dominick,Bukoba

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekerwa na kasoro zinazojitokeza mara kwa mara kwenye miradi ya maendeleo na vitendo vya rushwa na ufisadi na kuzitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi  Zanzibar (ZAECA) kujitathmini katika kazi zao.

Rais Samia ameyasema hayo Oktoba,14,2022 katika kilele cha mbio za mwenge wa uhuru na kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika Kitaifa katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

"Taasisi zetu za kuzuia na  kupambana na rushwa Tanzania bara na Zanzibar lazima tuchukue hatua hatuwezi kila mwaka kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa uhuru na kwenye taarifa ya mkaguzi mkuu wa serikali lazima ukute taarifa za maswala ya rushwa na ufisadi,hatuwezi kuendelea kulea uzembe na kutowajibika na kuendelea kwa vitendo hivyo" Amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa, TAKUKURU na ZAECA kabla hawajaenda kushughulikia mambo ya Rushwa katika taasisi nyingine wajitathmini wao kwanza kama wako sawa, kama wanaenda mwendo mmoja na lengo moja kati ya walioko makao makuu na walioko katika serikali za mitaa.


" Tungekuwa wote tunaongea lugha moja vitendo vyote vya rushwa vingeonekana mapema, taratibu zetu ni za kuzuia na kupambana na rushwa, mnachokifanya ni baada ya mwenge kuibua lakini  kwenye maswala ya kuibua bado hamjafanya vizuri niwaombe sana ongezeni jitihada katika kuzuia" Amesema Rais Samia

Amesema kuwa, katika kupiga vita vitendo vya rushwa itabidi wakae waulizane ili iwe ajenda ya kitaifa na kwa pamoja waweke mwelekeo wa kupambana na vitendo hivyo. 

Waziri ofisi ya Waziri mkuu, kazi, ajira, vijana na watu wenye ulemavu Pro.Joyce Ndalichako amesema jumla ya miradi ya maendeleo 65 katika halmashauri za wilaya 43 yenye thamani ya sh12 bilioni ilikataliwa kuzinduliwa na mwenge wa uhuru wakati wa kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi.

Alisema kuwa, Fedha za mikopo za vijana katika mfuko wa maendeleo ya vijana zaidi ya Tsh. bilioni 2.2 zimerejeshwa katika mfuko huo ili vijana waweze kupewa mikopo.


Aliongeza kuwa mwenge wa uhuru kwa mwaka 2023 utazinduliwa mkoa wa Mtwara na kilele chake kitakuwa mkoa wa Manyara.


Baadhi ya wananchi mkoani Kagera wamesema kauli ya Rais Samia kuzitaka Taasisi za TAKUKURU na ZAECA kujitathmini ni jambo jema kwani katika ujenzi wa miradi Taasisi hizo za Rushwa huwa zinashuhudia ujenzi wa miradi hivyo ni vyema zikawajibika vilivyo Kuzuia mianya ya rushwa ambayo imechangia miradi mingi kujengwa chini ya viwango licha ya miradi kugharimu fedha nyingi.

No comments