TFS : TARIME HAKUNA MISITU YA ASILI
Na Dinna Maningo, Tarime
MHIFADHI wa Misitu (TFS ) wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Charles Massawe amesema shughuli za binadamu zikiwemo za kilimo na mifugo pamoja na ongezeko la watu zimechangia kupotea kwa misitu ya asili huku jamii ikishindwa kuendeleza upandaji wa miti ya asili.
Akizungumza na Mwandishi wa DIMA Online katika ofisi ya TFS wilaya ya Tarime, Mhifadhi huyo amesema Tarime hakuna hifadhi ya msitu wa asili unaomilikiwa na Serikali kuu wala Halmashauri na kwamba misitu iliyopo ni ile iliyopandwa na binadamu ikiwemo inayomilikiwa na halmashauri.
" Wilaya ya Tarime hakuna hifadhi ya msitu wa asili unaomilikiwa na serikali kuu, kuna hifadhi za misitu iliyopandwa na binadamu ikiwemo na ile iliyopandwa na Halmashauri ya wilaya ya Tarime yenye hifadhi mbili za misitu, msitu wa Bwirege wa Hekta 87 na wa Nyabasi wa Hekta 17.
Amesema Halmashauri ya Mji wa Tarime kuna msitu wa hifadhi Bomani wa Hekta 41 na Mogabiri wa Hekta 6, miti iliyopandwa ni pamoja na Mikaratus (Ecalyptus sp) Ndege Chai (Grevillea robusta), Chapabunduki(Casuarina sp) na mti kunuka (Cedrela sp), na imekuwa ikivamiwa na watu wakikata miti ovyo.
Miti ya Kupandwa
" Eneo lilikuwa wazi kwasababu miti ya asili ilikatwa ndiyo sababu ikapandwa miti ya kisasa ili kuendeleza uhifadhi wa misitu, ni ngumu mwananchi kupanda miti ya asili kwakuwa mti wa asili kama unataka wa kupasua mbao inachukua miaka 30 hadi 40 ndiyo uvune, wengi wanakimbilia kupanda miti ya kisasa kama biashara ambayo yenyewe inachukua miaka michache kati ya 10-20 unavuna unapasua mbao zenye ubora unauza.
Amesema miti ya asili imekatwa sana kutokana na shughuli za kibinadamu kama matumizi ya mkaa, ujenzi , migodi ya wachimbaji wadogo hali ambayo imesababisha kuzidi kupotea kwa miti ya asili.
Ameshauri kuwa, ili wananchi washawishike kupanda miti ya asili ni vyema halmashauri zikawa mfano kwa kupanda miti ya asili kwakuwa miti hiyo ni muhimu na inaongeza pato la Taifa na kwamba ikipotea Taifa litapoteza mapato yatokanayo na utalii wa misitu ya asili.
Mti wa asili
" Tarime hakuna misitu ya asili ila kuna vichaka, wazee wa mila wanajitahidi kuhifadhi miti ya asili wana maeneo ambayo yamezungukwa na miti ya asili japo hata hayo maeneo ni madogo sana ambayo hayana hadhi ya kuitwa msitu , angalau wao hata kwa kile kidogo kilichopo wanakitunza na kukiendeleza, hata zile ardhi za jumla hakuna misitu ya asili amesema Charles.
" Pamoja na changamoto hizo TFS kwa kushirikiana na halmashauri tumekuwa tukidhibiti ukataji wa miti na usafirishaji usiofuata taratibu na sheria na wahusika wanawajibishwa, tunatoa elimu kuhakikisha rasilimali za Misitu zinalindwa .
Ameongeza kuwa ofisi ya TFS ya wilaya ya Tarime inakabiliwa na uhaba wa watumishi, ambapo ina watumishi watatu na haina gari na kwamba wanapotaka kufanya doria huazima gari halmashauri .
George Mwita mkazi wa Kwibanga kata ya Nkende amesema miti ya asili ina umuhimu kwakuwa inatoa mbao zenye ubora kama Muninga na Mtundu na inapoota kwenye maeneo ya visima maji hayakauki na inasaidia kuwepo kwa mvua.
John Chacha mkazi wa Kijiji cha Remagwe amesema " Tarime hakuna misitu ya asili ilikuwepo enzi hizo za mababu, watu waliivamia wakakata miti ikaisha iliyopo siyo misitu ni vichaka hata hao wazee wa mila wanatumia tu vichaka siyo misitu ,"amesema John.
>>> Kichaka ni mmea wa kudumu unaomea bila kupandwa wenye shina la ubao lakini, tofauti na mti, kuna mashina zaidi ya moja , tofauti nyingine ni urefu wake , vichaka kwa kawaida huwa na urefu wa sentimita kadhaa hadi mita 6 .Mimea mingi huweza kutokea ama kama kichaka au kama miti kutegemea na mazingira.
Kichaka
>>> Msitu ni mkusanyiko wa uoto wa asili unaojumuisha miti mingi ya aina mbalimbali, mimea na nyasi ambazo huweza kuwa fupi au ndefu.
>>> Misitu ipo ya aina mbili ya asili au ya kupandwa na Binadamu.
>>> Misitu ya asili ni misitu ambayo huota yenyewe bila kupandwa na mwanadamu.
Msitu wa asili
>>> Kwa mujibu wa Tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, inachangia asilimia 17.2 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya Mapato yote ya fedha za Kigeni.
Post a Comment